‘Kwa kuhifadhi misitu, uoto asilia tutaondoa maporomoko udongo’

By Dk. Felician Kilahama , Nipashe
Published at 09:40 AM Jan 07 2025
Waokoaji wakitafuta miili kwenye matope ya mafuriko na maporomoko ya udongo  Hanang', Desemba, 2023
Picha: Mtandao
Waokoaji wakitafuta miili kwenye matope ya mafuriko na maporomoko ya udongo Hanang', Desemba, 2023

WATANZANIA wanaendelea kufurahia mwaka mpya 2025, wakisubiri mvua za masika, lakini pia kutafakari vifo na hasara zinazotokana na maporomoko ya udongo kila mwisho wa mwaka.

Itakumbukwa kuporomoka kwa udongo Katesh wilayani Hanang yalitokea Desemba 2023 na mwaka huu kumeripotiwa mengine Same mkoani Kilimanjaro. 

Maporomoko  hayo ni matokeo ya  matumizi mabaya ya ardhi, yasiyoendelevu yanayosababisha misitu na uoto wa asili kutoweka kwa kasi na kuhatarisha maisha ya binadamu na viumbehai wengine.

Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye misitu na uotoasilia kwa asilimia kubwa, wakati wa uhuru karibu miaka 64 iliyopita, sehemu kubwa ilikuwa imefunikwa na misitu asili. 

Lakini taarifa iliyotolewa 2015 na Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia mradi wa kupima na kutathmini, misitu ilionyesha kuwa eneo lenye misitu Bara ni hekta milioni 48.1 (sawa na asilimia 55 ya eneo lote). 

Misitu aina ya “miombo” imetapakaa maeneo mengi nchini hususan kwenye ardhi inayomilikiwa na vijiji. Upande mwingine, kuna misitu inayofunika milima mathalan, Kilimanjaro na Meru, Livingstone na Rungwe kadhalika misitu katika hifadhi za taifa kama Ngorongoro, Uduzungwa pia mikoani Kagera, Katavi, Kigoma, Rukwa pamoja na baadhi ya maeneo kwenye mapori ya akiba.

Ingawa takwimu zinaonyesha Tanzania Bara imefunikwa na hekta milioni 48 za misitu, kiuhalisia misitu imetoweka kwa kiwango kikubwa. 

Kwa miongo minne iliyopita, kasi ya kukata miti, kufyeka misitu ya asili imekuwa ikiongezeka. Hadi sasa zaidi ya hekta 400,000 zinatoweka kila mwaka. 

Kisa ni  ongezeko la watu kutoka chini ya milioni 10 mwaka 1961 na zaidi ya milioni 60,  wanapoongezeka, mahitaji ya maeneo ya kuishi, kilimo na mifugo vinaongezeka pia. 

Kadhalika, kumekuwapo vijiji vingi zaidi ya 12,000, pia miji na majiji hupanuka wakati huduma za mipangomiji zikibaki nyuma.

 Hivyo, kusababisha baadhi ya misitu ya asili kumezwa.

Halikadhalika, mahitaji ya mazao ya misitu mathalani mbao, nguzo, mkaa  na kuni yakaongezeka kasi yake ikichochea ukataji miti. 

Ukiyajumlisha hayo pamoja na athari zinazotokana na kilimo cha kuhamahama, kuchoma mapori moto, kiangazi pamoja na misitu ya asili kutotunzwa au kutosimamiwa ipasavyo matokeo hasi yameendelea kuongezeka.

Yamesababisha sehemu nyingi kupoteza uotoasili (natural vegetation cover) hivyo ardhi kuathirika kwa kiasi kikubwa kwa vile haifunikwi na nyasi, majani, mimea, miti na misitu. 

Shughuli nyingi za kibinadamu zinapoongezeka bila kujali uwepo na umuhimu wa uotoasili kwa ajili ya kuhifadhi ardhi na udongo kutunza mazingira, wanaoathirika zaidi ni binadamu na viumbehai wengine. 

Kiikolojia, misitu pamoja na uoto asilia nyasi na majani, mimea kwenye mbuga au maeneo mengine husaidia, kwa kiasi kikubwa, kufunika ardhi au udongo ili kuzuia mmomonyoko kutokana na kasi kubwa ya upepo mkali au maji ya mvua.

KUPOROMOKA UDONGO

Maafa yanayojitokeza Tanzania mfano, kuporomoka ardhi au udongo huko Hanang, mkoani Manyara mwaka juzi na kuharibu eneo la mji mdogo Katesh na viunga vyake mathalani, Gendabi yalisababishwa na mvua kubwa.

Ikumbukwe yalikuwa maporomoko makubwa ambayo hayajawahi kutokea kwenye eneo la Mlima Hanang na kusababisha, bila kutarajia, mafuriko ya mawe, magogo na maji mengi yakitiririka kutoka milimani. 

Hali hiyo, ilizua taharuki na sintofahamu kwa wakazi wa maeneo ya Katesh, maporomoko hayo yakiharibu nyumba za wananchi zaidi ya 100 na baadhi ya watu kupoteza uhai. 

Serikali ikalazimika kutumia fedha nyingi kuwasaidia wananchi walioathirika kwa kuwajengea nyumba na kurejesha huduma muhimu za kijamii. 

Kadhalika, mwezi uliopita wilayani Same, mkoa wa Kilimanjaro, yalitokea maporomoko ya ardhi na udongo kutokana na ardhi kukosa uotoasili na misitu ya kuhifadhi udongo ili ubaki mahali pake. Kiikolojia miti na uoto mwingine wa asili ni mhimili wa kuhifadhi eneo kutokana na mizizi yake kuushikilia udongo.

Kadhalika, misitu au miti husaidia kupunguza kasi au nguvu ya maji au mvua hivyo kuwezesha maji ya mvua kuingia ardhini taratibu bila kuleta madhara.

Sehemu zenye upepo mkali pia misitu na miti hudhibiti kasi na nguvu ya upepo huo mkali, na kuzuia chembechembe za udongo kupeperushwa kupelekwa mbali.

Uharibifu unakuwa mkubwa kwenye sehemu zenye miinuko na milima hasa maeneo ambayo uotoasilia hakuna na misitu imeharibiwa kiasi cha kuiacha ardhi tupu bila kufunikwa. 

Kumekuwepo mazoea ya kulima kwenye miteremko mikali bila kuchukua tahadhari ili kuzuia mmomonyoko na maporomoko ya ardhi na udongo hasa inapotokea mvua kubwa. 

Maafa yaliyotokea Katesh na Same kisababishi kikubwa ni udongo milimani kubaki bila kufunikwa na misitu au uotoasilia hivyo kukosa cha kuushikilia.

Mvua kubwa ziliponyesha maji yakawa mengi ardhini na udongo ukalegea hivyo kupelekea maporomoko makubwa yenye udongo, mawe, miti, na vingine vingi kutoka milimani kwenda yalipo makazi ya watu hadi kusabatisha hasara kubwa. 

Mathalani, hali ilivyotokea wilayani Same ikiwamo watu sita kupoteza maisha na nyumba 25 kubomolewa hivyo kuacha wengi hawana pakuishi. 

Itakumbukwa mwaka 1963 kulitokea maafa katika eneo la Shume-Manolo wilayani Lushoto baada ya aliyekuwa Waziri wa Ardhi, wakati huo kuwaruhusu wananchi walime kwenye sehemu zenye miteremko mikali. 

Kitendo cha kuifyeka misitu na kupanda mahindi hakikuwaacha salama. Iliponyesha mvua kubwa kukatokea maporomoko makubwa ya udongo, mawe makubwa na takangumu nyingine vikafunika makazi ya watu. 

Ruhusa ya kulima ilitolewa kisiasa lakini kitaaluma na kiikolojia hayakuwa maamuzi sahihi, japo yalijiri kwa nia njema ya serikali kuwasaidia wananchi lakini matokeo yakawa kilio kikubwa. Tokea hapo serikali ikakataza watu kulima kwenye miteremko ya milima.

Kwa kuwa binadamu husahau tukio hilo lilifutika kwenye kumbukumbu za walioshuhudia ajali hiyo mbaya sababu ya kufyekwa misitu kwenye milima hatarishi ili kupata chakula ambacho hakikupatikana badala yake kukatokea kuporomoka ardhi. 

Pamoja na watu kuwa wengi na mahitaji ya chakula kuongezeka, ufyekaji misitu umekithiri hadi kulima kwenye milima, miteremko hatarishi na vyanzo vya maji. 

Viongozi serikalini, nje ya serikali na wadau  tambueni kwamba rasilimali misitu, uotoasilia kwenye milima na miterenko mikali ni muhimu sana hivyo itunzwe kwa nguvu zote.

Sera za uhifadhi na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, vitekelezwe kivitendo na usimamizi wa sheria uimarishwe. 

Tukisema sehemu fulani binadamu asiingie kulima, wala kuazisha makazi, kufyeka misitu na kukata miti au kuchunga, kufuga mifuko, iwe hivyo. Vijiji viweke sheria za kuhakikisha maeneo yenye milima, miteremko na ardhioevu kama vyanzo vya maji, yatambulike vijijini na kuyahifadhi ipasavyo. 

Tusisubiri maafa yatokee, kuzua taharuki halafu ndipo tuchukue hatua: kumbuka kinga ni bora kuliko tiba, tulitambue hili na tulisimamie bila kuoneana haya hasa ndugu na jamaa kwa kufanya shughuli za kibinadamu sehemu hatarishi zitakazopelekea taifa kupatwa na maafa kutokana na maporomoko ya ardhi na/au mmomonyoko wa udongo.

Matukio kama hayo yakiendelea kutokea itadhihirisha wengi wetu kukosa maarifa stahiki na kushindwa kusimamia utekelezaji wa Sheria na Kanuni husika.

Sheria ya kutunza, kulinda na kusimamia mazingira nchini iweke mkazo kwenye kutunza na kuyasimalia maeneo yote nyeti na kuhakikisha yasiharibiwe na binadamu kwa maslahi binafsi, bali yatunzwe kwa faida yetu na vizazi vijavyo.

Tumerithi nasi tuwarithishe.

Hii ni pamoja na kuhakikisha misitu na uotoasilia kwenye maeneo hatarishi, havifyekwi wala kuchomwa moto ovyo. Sheria kali ziwekwe na watakaothibitika kufanya vitendo vya kuhatarisha mazingira kwa faida binafsi waadhibiwe vikali maana hao ni wahujumumazingira kiasi cha kusababisha binadamu kupoteza maisha au kuumizwa vibaya na maporomoko ya ardhi na udongo yanapotokea.