Kinga mabadiliko tabianchi, mbegu bora, kilimo kisicho kemikali

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 09:30 AM Jan 07 2025
Mtafiti wa bayoteknolojia ya kilimo UDSM, Dk. Aneth David, akiwa katika majukwaa ya mijadala ya kisayansi
Picha: MAULID MMBAGA
Mtafiti wa bayoteknolojia ya kilimo UDSM, Dk. Aneth David, akiwa katika majukwaa ya mijadala ya kisayansi

WATAFITI wa kilimo wamebainisha kuwa matumizi ya bayoteknolojia na uhandisi jeni ni muhimu zama hizi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwenye kilimo na uzalishaji chakula.

Bayoteknolojia ni teknolojia inayotumia elimu ya baiolojia kufanya utafiti wa aina mbalimbali kuboresha maisha na sasa imeimarishwa zaidi ikifanyakazi kwenye maabara za kisasa unaohusisha utafiti wa hali ya juu zaidi.

Wakizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam, watafiti hao wanasema teknolojia hiyo ina umuhimu kwenye kuongeza tija ya kuzalisha mazao na kuwabadilisha wakulima kutoka kilimo cha kujikimu hadi cha kibiashara.

Aidha, wanashauri kuwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha madhara ya moja kwa moja kwenye uzalishaji mashambani, ni muhimu kwa sasa teknolojia mbalimbali ikiwamo ya uhandisi jeni zikapewa kipaumbele ili kupata ufumbuzi wa changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa kwenye kilimo.

Mtafiti wa bayoteknolojia ya kilimo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk. Aneth David anasema. 

Dk. Aneth akizungumzia  kuhusu bayoteknolojia anasema ni mkusanyiko wa teknolojia mbalimbali ambazo zinatumia sehemu ya viumbe hai ikiwamo vidubini au bakteria  kwa ajili ya faida ya binadamu, hususani katika kuandaa mbegu ambazo zinakuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na athari za  mabadiliko ya tabianchi. 

Anasema mazao yanayotokana na mbegu zilizofanyiwa mabadiliko ya vinasaba kwa njia ya uhandisi jeni yanaongeza tija na kumnufaisha zaidi mkulima wakati wa mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri sekta ya kilimo na uzalishaji. 

Akifafanua kuhusu bayoteknolojia anasema ni mkusanyiko wa teknolojia mbalimbali ambazo zinatumia sehemu ya viumbe hai ikiwemo nasaba ili kuongeza uhimilivu na uimara, nguvu za kukabiliana na magonjwa lakini pia kupata mazao kwa wingi.

Anasema ni kwa faida ya binadamu, hususani katika kuandaa mbegu ambazo zinakuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Dk. Aneth, anasema utaratibu wa utafiti na kuruhusu mbegu zilizofanyiwa mabadiliko ya  kijenetiki kwa ajili ya chakula unahusisha majaribio ya usalama wa chakula pamoja na kupima virutubishi.

Bingwa huyo wa bayoteknoloji ya kilimo anasema mazao yanayotokana na mbegu zilizoboreshwa kwa njia ya kijenetiki yana nafasi kubwa ya kutatua changamoto za upatikanaji wa chakula salama na cha kutosha, jambo ambalo ni changamoto katika mataifa mbalimbali ya Afrika hasa kipindi cha ukame unaotokana na mabadiliko ya tabianchi.

“Bayoteknolojia inatumika kutengeneza mbegu kwa ajili ya kutatua changamoto ambazo ni ngumu kutatulika kwa kutumia  mbegu za asili. Mfano, magonjwa, wadudu wapya vamizi wasio na suluhisho na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame na ukosefu wa virutubishi kwenye chakula, hayawezi kutatuliwa na mbegu za asili,” anafafanua Dk. Aneth.

UMUHIMU WAKE

Bingwa huyo anasema kwa kutumia sayansi ya kuboresha mbegu kijenetiki wanaweza kutengeneza mbegu na mazao yanayoweza kustahimili ukame, kuhimili magonjwa yasiyo na tiba kama ugonjwa wa michirizi ya kahawia kwenye mohogo yanayoweza kukua kwenye udongo usiofaa kwa kilimo cha kawaida ikiwamo wenye kiasi kikubwa cha chumvi.

Pia, anasisitiza kuwa teknolojia ya mbegu za kisasa inasaidia kuwa na mazao yanayoweza kupambana na wadudu waharibifu kama viwavi jeshi vamizi bila kutumia kemikali. Na kwamba mahitaji ya chakula yanazidi kuongezeka kutokana na kuwapo idadi ya watu lakini pia uzalishaji ukiathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

Anaeleza kuwa kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo ni tatizo kubwa kwenye kilimo Tanzania na Afrika, mbegu zilizoboreshwa kwa njia ya kijenetiki zinaweza kutoa suluhisho bora zaidi na la uhakika.

Akijibu suala la mbegu gani ipewe kipaumbele, anasema uamuzi kuhusu mbegu unategemea mambo mengi na hamna jibu la jumla. Na kwamba maamuzi yanatakiwa yafanyike kwa kuzingatia hoja kwa hoja kutegemea na mahitaji ya wakati, mahali na malengo.

Dk. Aneth anashauri kuwa ni muhimu kwa serikali na wadau wengine wa kilimo kuweka kipaumbele zaidi kwenye teknolojia mbalimbali zinazolenga kuleta suluhisho la kudumu kwenye ulinzi wa chakula na kilimo, ikiwamo bioteknolojia.

Anasema jamii ina nafasi kubwa ya kushirikiana na wataalamu na serikali katika kutatua changamoto za kilimo na uzalishaji wa chakula. Ila jukumu kubwa zaidi ni kwa watunga sera na inawekeza rasilimali kwenye tafiti za kilimo na maendeleo ya mbegu na kuhakikisha usalama wa chakula.

“Kama nchi hatuwezi kubaki nyuma, ni muhimu kujijengea uwezo wa kutafiti na kufikishia walaji mbegu zilizoboreshwa kwa teknolojia za kisasa kama bioteknolojia ya uhandisi jeni ili kufanikisha utatuzi wa changamoto za kilimo na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao,” anasema Dk. Aneth.

INAZUIA UHARIBIFU

Anasema kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ni muhimu kuipa kipaumbele bayoteknolojia katika kuendeleza kilimo kwasababu inasaidia mimea kujilinda yenyewe dhidi wa magonjwa na wadudu vamizi waharibifu.

Anafafanua kuwa inatumika kuandaa au kutengeneza vinasaba vinavyotumika kusaidia mmea kupambana na magonjwa mbalimbali ya moja kwa moja, pamoja na kuchanganya vinasaba vya mimea zaidi ya mmoja ila kutoa mazao bora.

“Kwenye kilimo tunatumia teknolojia hii kutengeneza mbolea hai (organic fertilizers) na katika utafiti, tumeona tunaweza kuchukua vidubini au bakteria wanaoweza kuchukua hewa ya nitrojeni wakaitengeneza ili kutumiwa na mimea.

“Kwahiyo badala ya kutumia mbolea ya kemikali ambazo zina madhara, tunatumia bakteria wanaosimama kama mbolea mbadala na kuwezesha mimea kufyonza madini kama salfa na salfeti kutoka kwenye udongo kuupa mmea nguvu na uimara,” anasema Dk. Aneth.

SULUHU YA UHAKIKA

Meneja wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Mikocheni Dar es Salaam, Dk. Fred Tairo, anasema kuna umuhimu mkubwa wa kutumia bioteknolojia kwenye kilimo kwa sababu inawawezesha  wakulima kupata mbegu zenye ufanisi na kutatua kwa haraka changamoto zinazowakabili.

Vilevile, anasema teknolojia hiyo na njia mbalimbali za kiasili inawezesha kupata dawa za haraka hasa katika kukabili magonjwa mapya yanayoibuka na kupata urahisi wa kutambua mdudu wa aina gani anashambulia mazao ya chakula na kumkabili asilete madhara.

“Kwa kutumia bayoteknolojia na matokeo ya kiutafiti tunampatia mkulima suluhu ya haraka, na teknolojia hii ina sifa nzuri kwenye mimea mfano migomba na mahindi inachochea kuongeza ufanisi.

“Teknolojia hiyo pia inatusaidia kuboresha mbegu kutoka kwenye mimea mingine, kwa ujumla ukitumia bayoteknolojia inatupa mwongozo wa kutatua matatizo yanayowakabili wakulima kwa ufanisi na haraka,” anasema Dk. Tairo.