UWANJA wa soka wa New Amaan Complex, visiwani hapa unatarajiwa kufungwa kuanzia kesho kwa muda ili kuruhusu mchakato wa ukarabati kufanyika, imeelezwa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF),Issa Kassim, aliliambia gazeti hili jana kufuatia uamuzi huo, mechi za Ligi Kuu zilizotarajiwa kuchezwa kwenye uwanja huo sasa zitafanyika kwenye Viwanja vya Mau.
Kassim alisema kwa upande wa Pemba, mechi za Ligi Kuu sasa zitachezwa kwenye viwanja vya Finya ili pia kuruhusu ukarabati wa Uwanja wa Gombani kufanyika.
Alisema mechi za kuanzia mzunguko wa tano wa ligi hiyo zitachezwa kwenye Uwanja wa Finya na tayari taarifa zimepelekwa kwa klabu zote.
"Uwanja wa New Amaan Complex utafungwa kuanzia Novemba 4, kuanzia sasa mechi zitachezwa kwenye viwanja viwili vya Mau A na B. Ratiba ya ligi hiyo tayari imetoka tangu Jumamosi kwa ajili ya michezo ya Jumatatu Novemba 4," alisema ofisa huyo.
Kuhusu malalamiko ya viwanja vya Mau kutokuwa na ubora, Kassim alisema kwa sasa klabu zitalazimika kucheza hapo kwa sababu ni lazima maboresho yaliyopangwa yafanyike kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.
Alisema anaamini mechi zitakazochezwa kwenye viwanja vya Mau zitakuwa chache za kukamilisha mzunguko wa kwanza na hatua ya lala salama itakayoanza Januari itafanyika New Amaan.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED