Mtibwa: Tutarejea Ligi Kuu mapema

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 08:35 AM Feb 06 2025
Thobias Kifaru, Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar
Picha: Mtandao
Thobias Kifaru, Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar

UONGOZI wa Mtibwa Sugar unatamba timu yao itarejea mapema katika Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na mechi nyingi 'mkononi'.

Mtibwa Sugar yenye pointi 44 ndio vinara wa Ligi ya Championship inayoendelea katika viwanja mbalimbali nchini.

Thobias Kifaru, Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, aliliambia Nipashe, wana kikosi imara na kilichojipanga vyema kuhakikisha wanatimiza mipango yao ya kurejea katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kifaru alisema wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo wanafahamu walipokosea na sasa wamejiimarisha katika kila idara ili kupata matokeo chanya.

"Tunajivunia ubora wa kikosi chetu, tuna wachezaji wenye uwezo na wanaofahamu malengo ya klabu, sisi tutarejea Ligi Kuu Tanzania Bara mapema sana, tayari tumeshaona hesabu zetu zinatuambia," Kifaru alitamba.

Aliongeza mbali na kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara, pia wanahitaji kutwaa Tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi ya Championship kwa msimu huu.

"Mshambuliaji wetu Raizin (Khalfan), amekuwa chachu katika kufikia malengo, ataendelea kutikisa nyavu za wapinzani katika kila mechi, tumecheza michezo 17 na yeye amefunga mabao 14, hii inaonyesha yuko vizuri," aliongeza Kifaru.

Nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo inashikiliwa na Geita Gold yenye pointi 36 ikifuatiwa na Mbeya City na Stand United zenye pointi 35 kila moja.