TIMU ya soka ya Matuli kutoka Kata ya Ngerengere Wilaya ya Morogoro, mkoani hapa, imejinyakulia kitita cha Sh. milioni tano baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kiroka kwenye mchezo wa fainali wa michuano ya 'Samia Cup', uliopigwa katika Tarafa ya Ngerengere juzi, Jumamosi.
Kombe hilo la Samia Cup lililoanzishwa na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale maarufu kama Babu Tale, lilihusisha timu zote kutoka kwenye Kata 14 jimboni hapo lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kusaka vipaji vipya.
Mshindi wa pili ambayo ni timu ya Kiroka, ilijinyakulia Sh. milioni tatu, huku ya tatu timu ya Gwata ikizawadiwa Sh, milioni mbili wakati Kinole ikiambulia Sh. milioni moja kwa kushika nafasi ya nne katika michuano hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi kombe pamoja na fedha hizo kwa washindi, Babu Tale alisema mashindano hayo yamegharimu zaidi ya Sh. milioni 45 ikijumuisha na kila timu kupewa Sh. 500,000 na jezi za kisasa jozi mbili, maandalizi ya michuano hiyo pamoja na zawadi kwa washindi na wafungaji wa 'Goli la Mama'.
“Katika mashindano haya yaliyohitimishwa leo [juzi] ya Samia Cup, yalichezwa kwenye kata zote 14 za tarafa tatu za Jimbo langu la Morogoro Kusini Mashariki, na kila timu zilipewa jezi jozi mbili, Sh. 500,000 na mipira, na michuano hiyo ilifanyika kwa mtindo wa nyumbani na ugenini," alisema.
Hata hivyo, Babu Tale alisema malengo ya mashindano hayo yamefikiwa kama ilivyopangwa ikiwa ni pamoja na wananchi kuhamasika kwa wingi kwenda kujiandikisha, lakini pia wameibua vipaji vya zaidi ya wachezaji watano kutoka kata mbalimbali na tayari ameshawasiliana na timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ajili ya kuwafanyia majaribio.
Alisema baada ya kumalizika michuano hiyo, anatarajia kuanzisha ligi nyingine itakayoanzia ngazi ya kila kijiji kilichopo kwenye Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ili kuendelea kuibua vipaji na kuleta furaha kupitia michezo.
Akikabidhi Kombe hilo, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Morogoro, Solomoni Kasaba, alipongeza jitihada za mbunge huyo kwa kuwaunganisha wananchi kupitia michezo.
Katibu huyo, alisema michezo hiyo ilikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho na kumtaka Babu Tale kuendelea kueneza michezo katika Jimbo hilo kila wakati ili kuvumbua vipaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED