NAHODHA wa zamani wa Yanga na kocha wa timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa, amesema kuondolewa kwa timu hiyo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kushindwa kufika hatua ya robo fainali kama msimu uliopita, kumetokana na wachezaji wa timu hiyo kutokuwa na utimamu wa mwili, kitu ambacho kimechangiwa na kutokuwa na maandalizi mazuri ya mwanzo msimu huu, 'pre season.'
Mkwasa, ambaye pia ni kocha wa Timu ya Taifa chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, alisema mwanzoni mwa msimu Yanga ilitumia muda mwingi kwenda kucheza mechi za kirafiki nchini Afrika Kusini kuliko kukaa kambini na kuwapa wachezaji wao mazoezi ya nguvu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, alisema mechi ambazo Yanga ilikuwa inashinda kwa siku za karibuni ni kujituma kwa wachezaji wenyewe baada ya maneno na malalamiko kutoka kwa mashabiki, kitu ambacho pia kimesababisha kuzalisha majeruhi wengi kwa sababu hawako fiti, wanajilazimisha tu.
"Tangu msimu ulivyoanza, Yanga haikuonekana kuwa kwenye kiwango bora ambacho ilikuwa nacho misimu miwili iliyopita, na nadhani haikufanya maandalizi ya msimu 'pre season' ya kutosha, walianza tu mazoezi, wakaenda kucheza mechi za kirafiki nchini Afrika Kusini wakashinda-shinda, lakini haikuwa na msingi wa maandalizi ya mwanzo wa msimu, ndiyo maana ilipoanza ligi ikawa inashinda bao moja moja tu, mashabiki wanalalamika maana walizoea mabao mengi," alisema.
Alisema kipindi kile kilikuwa ni cha kuwaweka wachezaji kambini na kuwafanyisha mazoezi ya kusaka fiziki badala ya mechi za kirafiki ambazo wachezaji walikuwa wanafurahia zaidi kuliko kufanya mazoezi.
"Mimi navyojua mwanzo wa maandalizi, kiasi cha wiki tatu kocha anaangalia masuala ya utimamu wa mwili tu kwanza, baadaye ndiyo yanakuja mambo ya ufundi, na timu ikikamilika kwa fiziki huwezi kukuta kuna majeruhi wengi kwenye kikosi.
"Kuna kipindi utimamu unapanda na kushuka, na wanajilazimisha kwa sababu ya presha ya mashabiki, wachezaji wanapambana, wakifanya hivyo kwa sababu wanatumia nguvu kubwa, kuna wakati wanakuja vizuri, lakini walikuwa hawawezi kucheza mechi tatu kwa kasi ile ile.
"Utakuta wanazalisha majeruhi wengi kwenye kikosi na wachezaji muhimu wanakosekana inakuwa hasara kwa timu, lakini wangekuwa na msingi wa fiziki tangu awali, wasingefika hapa," alisema.
Akiizungumzia mechi ya Jumamosi, alisema wachezaji wa Yanga walikuwa wanajazana kati ambako wenzao walikuwa wamejaa, badala ya kusambaa kila eneo, ikiwamo pembeni mwa uwanja.
"MC Alger alikuwa na plani ya kuzuia, walitaka pointi moja, walikuwa na wachezaji wengi katikati, na wengine si kiungo ni mabeki waliwaweka pale kati, tatizo ni kwamba Yanga hawakutaka kubadilika walikuwa wanataka kulazimisha kupita katikati, wangejaribu kupita pembeni na kupiga zaidi krosi, kwa sababu wako wengi wangeweza hata kufanya makosa ya kushika, au kujifunga wenyewe, mchezaji pekee ambaye nilimuona akiwa kidogo anajitahidi kwenda pembeni ni Prince Dube," alisema Mkwasa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED