KOCHA Mkuu wa Simba Queens, Yussif Basigi, amesema kikosi chake kipo kwenye maandalizi makali kwa ajili ya mchezo wa keshokutwa, Jumatano dhidi ya Yanga Princess, utakaopigwa Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, huku akiapa kulipiza kisasi cha kufungwa katika mechi ya Ngao ya Jamii.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Basingi kocha aliyechukua nafasi hiyo kutoka kwa Juma Mgunda, amesema hata mchezo uliopita dhidi ya Ceasiaa Queens ambao walishinda mabao 4-1, walicheza kwa uangalifu ili kutopata majeruhi ambayo yanaweza kusababisha baadhi ya wachezaji kuikosa mechi hiyo.
"Tumeshinda mchezo ule kwa mabao mengi pamoja, lakini uwanja haukuwa mzuri, hatukuweza kumiliki mpira vizuri kutokana na hali mbaya ya uwanja, nikaanza kuwatoa baadhi ya wachezaji ili wasipate majeraha kwa ajili ya kujiandaa na mchezo unaokuja," alisema kocha huyo raia wa Ghana.
Kocha huyo alisema lengo la kuwapumzisha mastaa wake ni kutaka kulipiza kisasi kwani katika mchezo huo hakuwa sehemu ya benchi la ufundi kutokana na kutokuwa na kibali yeye na baadhi ya wachezaji tegemeo wa kikosi hicho.
"Niseme kuwa mechi ya dabi haitokuwa rahisi, tuko tayari kimwili na kiakili, tumejiandaa ili kushinda kwa sababu mashabiki wetu walivunjika mioyo siku ile tulipofungwa kwenye Ngao ya Jamii, tunataka kuwafuta machozi," alisema.
Simba Queens ilifungwa kwa mikwaju ya penalti 4-3 na Yanga Princess kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii kuashiria mwanzo wa Ligi Kuu msimu huu, uliochezwa Oktoba 2, mwaka huu katika Uwanja wa KMC Complex, hatua hiyo ya matuta ilifikiwa baada ya sare ya bao 1-1.
Jumatano mchezo huo, utakuwa ni wa raundi ya nne ya Ligi Kuu, ambapo Simba Queens inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi tisa kutokana na kushinda michezo yote mitatu iliyocheza, ikifunga mabao 10 na kuruhusu mawili, ikifuatiwa na JKT Queens ambayo ina pointi saba, ikishinda mbili na sare moja, huku Yanga Princess ikiwa kwenye nafasi ya tano, ikicheza mechi tatu bila kupata ushindi wowote, ambapo imetoa sare zote na kukusanya pointi tatu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED