WINGA wa Simba, Kibu Denis na Simon Msuva wa Al Tabala ya Iraq, wamerejeshwa katika kikosi cha Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), kwa ajili ya mechi za kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025), dhidi ya Ethiopia na Guinea, imefahamika.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco' ameita wachezaji 25 kwa ajili ya michezo hiyo miwili huku pia akimrejesha katika kikosi 'mama' beki wa kulia mzoefu nchini, Shomari Kapombe na aliyekuwa kipa chaguo la kwanza, Aishi Manula.
Stars itakutana ugenini dhidi ya Ethiopia Novemba 16, mwaka huu na siku tatu baadaye itakutana na Guinea.
Morocco pia amemwita kwa mara ya kwanza straika wa Mashujaa FC, Ismail Mgunda, ambaye amekuwa na kiwango kizuri katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea hapa nchini.
Nyota wengine walioitwa katika kikosi hicho ni pamoja na Zuberi Foba, Lusajo Mwaikenda, Adolf Mtasingwa, Paschal Msindo, Feisal Salum na Nassor Hamduni kutoka Azam FC, Ibrahim Hamad 'Bacca', Dickson Job, Mudathir Yahaya, na Clement Mzize (Yanga), Metacha Mnata, Habib Khalid (Singida Black Stars) na David Brayson wa JKT Tanzania.
Wachezaji wengine ni Ibrahim Ame (Mashujaa FC), Abdulrazack Hamza (Simba), Novatus Dismas(Goztepe- Uturuki), Abdulkarim Kiswanya (Azam U-20), Cyprian Kachwele (Vancouver Whitecaps- Canada) na nahodha, Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Paok ya Ugiriki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED