Guede afunguka anataka mabao 17

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 09:37 AM May 03 2024
Mshambuliaji wa Yanga, Joseph Guede.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Joseph Guede.

BAADA ya kufunga bao moja katika ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya Tabora United katika mchezo wa robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA, mshambuliaji wa Yanga, Joseph Guede, amesema atahakikisha anafunga mabao 17 kwenye michuano yote msimu huu.

Guede ambaye alianza kwa kusuasua baada ya kujiunga na Yanga, kwa sasa amekuwa 'moto', akifunga mabao muhimu kwa timu yake katika mashindano mbalimbali yanayoendelea.

Bao alilofunga nyota huyo raia wa Ivory Coast katika mchezo wa juzi dhidi ya Tabora United, limemfanya afikishe mabao nane katika mashindao yote mpaka sasa.

"Nafurahia kuifungia timu yangu, nataka niwe nafanya hivi katika kila mechi ninayopata nafasi ya kucheza, malengo yangu ni kufunga angalau mabao 17 msimu huu," alisema Guede.

Mshambuliaji huyo alisema ataendelea kushirikiana na wachezaji wenzake kuhakikisha Yanga inafikia malengo yake msimu huu kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na kutetea Kombe la FA.

"Nadhani bado tupo katika malengo yetu kama klabu na hilo ndio la muhimu, kikubwa ni kuhakikisha tunafikia malengo yetu msimu huu," alisema Guede.

Kuhusu kiwango cha mshambuliaji huyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, alisema anafurahishwa na jitihada na uwezo wa nyota wake huyo.

"Amekuwa na kiwango kizuri, anatufungia kila mechi, nafurahishwa na uwezo wake na kila anachokitoa kwa ajili ya timu," alisema Gamondi.

Kocha huyo aliongeza anaamini Guede  ataendelea kufanya vizuri na anajivunia uwezo wa wachezaji wake lakini pia akifurahia kurejea kwa, Pacome Zouazou.

"Nimefurahi sana kuingia nusu fainali, lakini sifa ni kwa wachezaji, tuna muda mchache kutoka mchezo mmoja na mchezo mwingine lakini wachezaji wangu hilo hawalijali, wanapambana uwanjani na hii ndio faida yake, nawapongeza sana," alisema Gamondi.

Aliongeza kurejea kwa nyota wake, Pacome ni jambo zuri kwake na anaamini hata mashabiki wa timu hiyo wamefurahi kumwona tena uwanjani.

"Upana wa kikosi changu unaongezeka kwa kurejea kwa Pacome, ni jambo uzri na nimefurahi, nimeanza kwa kumpa dakika 25 ili taratibu arejee kwenye utimamu wa mechi, nitakuwa nikimwongezea dakika taratibu mpaka arudi katika hali yake kiuchezaji, naamini na mashabiki wamefurahi kumwona akirejea uwanjani," alisema Gamondi.

Yanga wanaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 62 baada ya kucheza michezo 24 ikifuatiwa na Azam wakati Simba wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 15 pungufu ingawa wamecheza michezo 22.