WAKATI ikidaiwa kocha raia wa Algeria, Kheireddine Madoui, kutua ndani ya Yanga, klabu hiyo imesema bado ina imani na Miguel Gamondi na inaendelea kumpa ushirikiano wa kutosha kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan, utakaochezwa Novemba 26, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Klabu hiyo, Alex Ngai, alisema juzi jioni kuwa tetesi za kwamba klabu hiyo itamtimua Gamondi na kumleta kocha mwingine hazina ukweli wowote na kuwataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na wasiwasi wowote kwani viongozi wa Yanga bado wana ushirikiano na benchi la ufundi.
"Yanazungumzwa mengi, lakini niwahakikishie wanachama, mashabiki wa Yanga kuwa viongozi wote wa Yanga wapo vizuri, tuna ushirikiano na benchi la ufundi, tutakaa na kufanya tathmini na tunaendelea na maandalizi ya mechi yetu dhidi ya Al Hilal ya Sudan, mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Black Stars tuliokuwa tucheze Novemba 21 imeshaondolewa kwenye ratiba," alisema Ngai.
Alisema pamoja na ukweli kwamba kuondolewa kwa kocha kwenye timu yoyote ile si jambo la ajabu, lakini kwa Yanga haiwezi kuwa hivi sasa kwani hakuna mpango huo kama inavyoelezwa.
"Kwa kweli siwezi kusema kama ni kweli, haina ukweli, Yanga ni timu kubwa, niwaondoe hofu tuko kwenye maandalizi, kama lolote litatokea basi haitokuwa ajabu lakini kwa sasa sitarajii kitu kama hicho.
"Tunamsapoti, tunaendelea kumpa sapoti," alisema.
Tetesi zinadai Gamondi anaweza kuondoka wakati wowote na kocha huyo kuchukua nafasi yake, huku mwenyewe akiwa amefuta utambulisho wake kama kocha wa Yanga kwenye akaunti yake katika mtandao wa instagram.
Taarifa zinasema kumekuwa na mgawanyiko kwa baadhi ya viongozi, wengine wakitaka aondoke na wengine wakitaka abaki ila kuna vitu virekebishwe na yeye mwenyewe ajirekebishe.
Akizungumzia vipigo viwili mfululizo ambavyo timu hiyo imevipata kutoka kwa Azam FC na Tabora United, Ngai alisema ni hali ya mchezo na watakaa sawa na kurekebisha mambo kabla ya kurejea tena kwenye reli.
"Sidhani kama tunapitia kipindi kigumu, ni hali tu ya mchezo, katika mpira wa miguu vitu kama hivi huwa vinatokea, bahati mbaya sana tumepoteza mechi mbili mfululizo, mfano kwenye mchezo dhidi ya Tabora, safu yetu yote ya ulinzi haikuwapo, wengine walikuwa na kadi za njano, wengine wamesimamishwa na baadhi majeruhi pia, hali ile ilituathiri sana mpaka ikafikia Khalid Aucho akarudishwa nyuma kwenda kucheza nafasi ya beki, hii ni changamoto tu tutarudi kwenye reli kama kawaida," alisema.
Katika mchezo dhidi ya Tabora United, Yanga iliwakosa Yao Kouassi ambaye ni majeruhi, Ibrahim Hamad 'Bacca' aliyekuwa akitumikia adhabu ya kadi nyekundu na Dickson Job aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Alisema pamoja na kupoteza, Yanga bado iko kwenye mbio za ubingwa na ni moja kati ya timu zinazojua kuchanga karata zake kuelekea kwenye mbio hizo, hivyo kuwataka mashabiki kutokata tamaa badala yake kuendelea kuisapoti.
"Yanga ni moja kati ya timu zinazojua kuchanga karata zake kuelekea kwenye ubingwa wa Tanzania Bara kwa hiyo hii wala haitusumbui, imeshatokea imeshapita, ninachowaomba wanachama na mashabiki waendelee kuisapoti timu yao," alisema Ngai.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED