HAWAPONI, hayo ni maneno ya Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, kuelekea mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tabora United itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Kauli hiyo inatokana na hasira za kupoteza mechi dhidi ya Azam lakini pia akitaka timu yake ikae kileleni katika msimamo wa ligi hiyo.
Kocha huyo raia wa Argentina, alisema Yanga itacheza mchezo wa kasi na kushambulia muda wote na amewataka wachezaji wake kutumia kila nafasi itakayopatikana ili kupachika mabao yatakayowawezesha kupata ushindi na kuwarudishia furaha mashabiki wao.
"Mechi hii ipo mikononi mwetu, sisi ndiyo tutaamua tucheze vipi, tuwafungue vipi wapinzani wetu, nadhani wao watacheza kwa ajili ya kutuzuia na kuzima mbinu zetu, tunacheza kwa kasi na kutumia nafasi zitakazopatikana ili kuwafungua wapinzani na kuwatoa nyuma ambako watakuwa wamejazana.
Hizi timu kama hujapata bao hawaondoki nyuma, ukitaka ucheze nao vizuri funga kwanza bao, hapo wataanza kutoka na wao kuanza kushambulia, mpira utachezwa vizuri," alisema Gamondi.
Kocha huyo aliongeza katika mechi ya leo atawakosa wachezaji wake watatu nyota ambao ni Ibrahim Hamad 'Bacca', Dickson Job na Yao Kouassi kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kadi na majeruhi.
"Tulipoteza mchezo wetu waliopita, lakini huu tutafanya kila tunachoweza ili kurudisha furaha kwa mashabiki wetu, tunataka kushinda ili tuendelee kuongoza ligi wakati tunakwenda katika mapumziko ya Kalenda ya FIFA," alisema kocha huyo.
Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto, aliliambia gazeti hili wanarejea katika ligi kwa nguvu baada ya kupoteza mchezo uliopita.
"Tunataka kurejea kwa nguvu, matokeo yaliyopita yamepita, kama wachezaji tupo katika hamasa ya hali ya juu, mashabiki waendelee kutusapoti na hatutawaangusha," alisema Mwamnyeto.
Kocha wa makipa wa Tabora United, Khalfan Mbonde, amekiri watakuwa na dakika 90 ngumu dhidi ya Yanga, lakini wamejipanga kisawasawa kukabiliana nao huku Heritier Makambo na Yacouba Songne, wakitarajiwa kuongoza kikosi hicho.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED