KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amewataka wanachama na mashabiki kuangalia mbele, na kukubali kuwa wamepoteza mchezo wao dhidi ya Azam kwani hakuna timu yoyote duniani ambayo haifungwi.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu hiyo na Azam FC, ikichapwa bao 1-0, lililowekwa ndani ya wavu na Gibril Sillah, kocha huyo alisema hakuna yeyote anayependa kupoteza mechi, lakini ni lazima kuukubali ukweli.
Yanga imepoteza kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kucheza michezo minane ikishinda yote na kutoruhusu wavu wake kuguswa, lakini rekodi zote mbili zimevunjwa kwa wakati mmoja juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
"Hakuna anayependa kupoteza, lakini inabidi tukubali, nawapa pole sana na samahani mashabiki wa Yanga, wajue huu ni mpira na siku moja timu itapoteza mechi, lazima waamini hivyo, hakuna timu yoyote duniani ambayo haipotezi," alisema.
Hata hivyo, Gamondi alisema kilichoigharimu timu yake ni kadi nyekundu aliyopewa beki wake, Ibrahim Hamad 'Bacca' kuwa iliwaathiri kwa kiasi kikubwa na kuisababisha kupoteza mchezo huo.
"Kilichotugharimu ni kadi nyekundu, kama tungekuwa sawa na wachezaji wa Azam, ingekuwa mechi nzuri zaidi. Nimemshangaa mwamuzi kwa sababu ametoa kadi nyekundu wakati tukio kama hili lilitokea katika mchezo wetu dhidi ya Simba, lakini kadi nyekundu haikutoka.
"Nilichofurahi ni kwamba pamoja na kucheza pungufu tumetengeneza nafasi nyingi, na hasa kipindi cha pili pamoja na muda wote tulicheza vizuri kuliko Azam, tukatengeneza nafasi mbili za wazi, walikuwa na bahati," alisema Gamondi.
Aliwapongeza Azam na kocha wao, Rachid Taousi, aliyesema ni rafiki yake mkubwa, wakifahamiana kwa miaka 25 wakiwa wameshawahi kufanya kazi pamoja, akiahidi watarejea wakiwa imara zaidi katika michezo inayofuata.
Kocha wa Azam, Taousi, alionesha furaha yake kwa kuifunga Yanga, akiwa kocha wa kwanza kufanya hivyo kwenye Ligi Kuu, huku pia timu yake kuwa ya kwanza kuondoa ubabe wa timu hiyo msimu huu.
"Tumekuwa timu ya kwanza msimu huu kuifunga Yanga, tumekuwa wa kwanza kufunga bao dhidi yao, na mimi nimekuwa kocha wa kwanza kumaliza ubabe wao, ushindi huu naupeleka kwa mashabiki wa Azam na mabosi wa klabu.
"Haikuwa rahisi, tumecheza na timu kubwa na wachezaji bora wenye viwango vya juu, tuliingia na mipango yetu ambayo imetusaidia sana," alisema kocha huyo ambaye naye akiri kwamba wanafahamiana vizuri na Gamondi kwa miaka mingi, wanajuana na ni rafiki yake mkubwa.
Pamoja na kupoteza, bado Yanga ipo kileleni ikiwa na pointi 24 kwa mechi tisa ilizocheza, Singida Black Stars ikirejea nafasi ya pili baada ya suluhu dhidi ya Coastal Union ikiwa na pointi 23 kwa michezo 10 iliyocheza, Simba ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake 22 kwa michezo tisa iliyocheza.
Ushindi wa juzi umeifanya Azam kufikisha pointi 21 kwa michezo 10 iliyocheza ikiwa kwenye nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED