Fadlu awalalamikia waamuzi Ligi Bara

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:49 AM Nov 03 2024
 Fadlu awalalamikia  waamuzi Ligi Bara
Picha: Mtandao
Fadlu awalalamikia waamuzi Ligi Bara

LICHA ya kupata ushindi wa jioni, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davis, amesema anashangaa kuona baadhi ya waamuzi wanaionea timu yake kwa kuinyima penalti zinazostahili na kuongeza huenda wanataka kuona wachezaji wake wakivunjwa miguu.

Fadlu alisema hayo baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu yake dhidi ya Mashujaa FC, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika na kuondoka na ushindi wa bao 1-0.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini alisema haelewi kwa nini kinatokea kwa baadhi ya waamuzi wanaochezesha michezo yao hawachuki hatua zinazostahili na hafahamu wanafanya hivyo kwa kutojua au kuna jambo lingine.

"Inawezekana Simba haistahili kupewa penalti katika Ligi Kuu kwa sababu mechi dhidi ya Yanga, Kibu alifanyiwa madhambi mara mbili ndani ya eneo la hatari mwamuzi akapeta, leo (juzi) tena, Mukwala (Steven), ameangushwa ndani ya boksi lakini hatujapewa pia, nadhani waamuzi wanataka wachezaji wangu wavunjwe miguu ndiyo waone ni kweli madhambi yamefanyika," alilalamika Fadlu.

Akizungumzia mchezo wenyewe, kocha huyo anayeifundisha Simba kwa mara ya kwanza msimu huu, alisema amefurahi kuona wachezaji wake wamecheza soka safi licha ya changamoto ya uwanja.

"Nimefurahi wachezaji wangu wamecheza soka safi kwenye uwanja ambao haukuwa rafiki. Hivi ndivyo ninavyopenda wachezaji wangu wawe, wacheze soka kwa dakika zote 90 kwa sababu bao linafungwa dakika yoyote ile," Fadlu alisema.

Naye Mukwala aliliambia gazeti hili amejisika furaha kufunga bao hilo na kuwafanya mashabiki wa Simba waliojazana kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika 'kupagawa' pia kwa furaha.

"Nimejisikia furaha sana mimi binafsi, ninacheza kwa ajili ya kuipigania nembo nimejisikia vizuri kuwapa furaha mashabiki wa Simba ambao muda wote wamekuwa nyuma yetu.

Mashujaa walikuwa wagumu kwa sababu walikuwa wanacheza kwao, lakini kilitupa nguvu wachezaji, sisi ndiyo tulikuwa tunacheza kama tupo nyumbani kutokana na umati mkubwa wa mashabiki uliokuwa unatushangilia. Mashujaa waliitafuta sare na wakaona wameipata, lakini sisi siku zote ni Simba," alisema straika huyo aliyesajiliwa kutoka Asante Kotoko ya Ghana.

Kocha Mkuu wa Mashujaa, Mohamed Abdallah 'Bares', alisema wachezaji wake walipambana, lakini mpira wa miguu una maajabu yake mpaka filimbi ya mwisho ipigwe ndipo unapokuwa umeisha.

"Mechi ilikuwa nzuri wachezaji wangu walipambana sana, mwisho wa siku tukubali huu ni mchezo kama haujaisha basi ujue mpo katika mechi. Hapa mwishoni tumeshindwa kukaba wachezaji kwa haraka kwenye kona wakaitumia, wenzetu walipiga kona upesi kama unavyojua ubora wa wachezaji wa timu hizi kubwa unaweza kukuhukumu, kilichojitokeza ni uwezo wa mchezaji mmoja umeamua mechi," Bares alisema.

Simba imefikisha pointi 22 kwa michezo tisa iliyocheza na kupaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi huku Mashujaa ikibakia na pointi zake 13 kibindoni.