Bodi ya Ligi: Kagoma mali halali Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:55 AM Sep 16 2024
Yusuph Kagoma.
Picha: Simba
Yusuph Kagoma.

BODI ya Ligi imesema inamtambua Yusuph Kagoma kuwa ni mchezaji halali wa Simba kwani ana leseni ambayo imetoka kwenye mamlaka ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), ambao ndiyo wanaowaletea majina na leseni zao kuthibitisha kuwa wako halali na wanaruhusiwa kutumika kwa timu husika.

Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda, amesema changamoto kwao kama Bodi ya Ligi ingekuwa kama wamemruhusu mchezaji huyo kucheza bila ya kuwa na leseni, lakini kwa sababu anayo na inamtaja kuwa ni mchezaji wa Simba, basi ana uhalali wote wa kuichezea timu hiyo.

Amebainisha Simba haiwezi kupokwa pointi kwa kumchezesha mchezaji huyo katika michezo yake ya ligi kwa sababu anacheza akiwa amekamilisha taratibu zote, na migogoro yote huwa inatatuliwa kwenye Kamati za TFF, kabla ya wao kuletewa maamuzi yakiwa yamekamilika.

Boimbanda alisema hayo kufuatia utata uliozuka hivi karibuni kwa Klabu ya Yanga, kudai ina mkataba wa miaka mitatu na Kagoma ambaye wanashangaa kuona amesajiliwa pia na Simba, wakisema kitendo hicho kinaonesha kuwa amesajili timu mbili.

"Siamini kama kwa dunia ya sasa kuna usajili wa timu mbili, siku hizi usajili una mifumo yake, mchezaji akiingizwa kwenye mfumo ulioitwa TMS na klabu moja, hakuna namna yoyote kwa timu nyingine inaweza kuingiza tena jina la mchezaji huyo huyo. Sisi kama Bodi tunapewa majina ya wachezaji ambao usajili wao umekamilika, tunaambiwa hawa wanastahili kutumika na timu hii na ndiyo waliopewa leseni na TFF," alisema Boimanda.

Alisema kwao huwa hakuna migogoro, badala yake hupelekwa kwenye Kamati ya TFF na baada ya kumalizika wao wanachopewa ni majina tu.

"Sisi hatuna mgogoro wowote, migogoro inakuwa huko TFF ambako ndiko kuna kamati, baada ya kumalizika sisi tunapewa majina tu ya kuwaruhusu, wao ndio wanaosimamia usajili na ndio wanaotoa leseni, kwa hiyo sisi hatuna mgogoro wowote kwenye usajili, tumepewa majina na tumeruhusu," alisema.

Kutokana na hivyo alisema Kagoma anaichezea Simba kwa sababu tayari ana leseni inayomruhusu na kama ingekuwa vinginevyo wangemzuia kama wanavyozuiwa wachezaji wengine.

"Ukimwona Kagoma anacheza kwenye michezo ya ligi maana yake amepewa leseni na TFF, ambao ndio utambulisho. Mle kuna jina la mchezaji, na unaambiwa ataitumikia timu gani, ndiyo maana nasema hakuna anayelalamika kuwa Kagoma amecheza mechi za ligi akiwa hana leseni, wangesema hivyo ndiyo tungepaswa kuulizwa kwa nini tunamruhusu mchezaji aingie uwanjani ikiwa hana leseni."

Klabu ya Yanga, Mwanasheria, Simon Patrick, amesema tayari suala hilo wamelipeleka kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji na bado halijafanyiwa kazi ili kutoa uamuzi.

Alisema klabu hiyo inataka kamati hiyo itamke ni mchezaji wa Yanga, pili kamati isimamie kanuni zake kwamba mchezaji anayesaini zaidi ya klabu moja afungiwe, au klabu ilipwe fidia na wahusika kutokana na mkataba huo kuvunjwa.