Al Ahli Tripoli wakodi mabaunsa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:40 AM Sep 20 2024
Al Ahli Tripoli wakodi mabaunsa
Picha:Mtandao
Al Ahli Tripoli wakodi mabaunsa

KATIKA hali inayoonesha wapinzani wa Simba, Al Ahly Tripoli wameingiwa na woga wa kufanyiwa kile walichowafanyia wekundu hao kwenye mchezo wa kwanza Libya, wamelazimika kukodi walinzi binafsi (Bodyguard) kwa ajili ya kuwalinda.

Mashabiki, wachezaji na baadhi ya Maofisa wa klabu hiyo walionekana kuwafanyia vurugu wachezaji wa Simba pamoja na waamuzi wakati na baada ya mchezo huo uliomalizika kwa suluhu.

Timu hiyo iliwasili jana jijini Dar es Salaam, tayari kwa mchezo wa marudiano, Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumapili.

Mabaunsa hao wa hapa nchini walionekana kuwalinda wachezaji na viongozi kuanzia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kwa chochote kibaya kitakachotokea, ingawa nyuso za wageni hao zilionekana kuwa bado zina hofu. 

Wakati timu hiyo ya Libya ikifanya hivyo, Kocha Mkuu wa Simba, David Fadlu, amesema ameshaiandaa vyema timu yake kwa ajili ya kuhakikisha inapata ushindi licha ya kuonekana mechi hiyo ina mambo mengi.

Fadlu, alisema matokeo ya mchezo uliopita wameyaweka pembeni na wanaelekeza nguvu na mawazo yao kwenye mchezo huo wa Jumapili huku wakijipanga kwa ajili ya ushindi.

"Tuko nyumbani, sasa tunatakiwa tuwe makini kwani tunacheza mbele ya mashabiki wetu ambao hawana wanachohitaji zaidi ya ushindi, wao (Al Ahly Tripoli) wafanye wanachotaka kukifanya, sisi tupo tayari uwanjani, lengo letu ni ushindi tu" alisema Fadlu.

Alisema pamoja na kwamba wanahitaji ushindi lakini mpango mkakati wa kulinda bado utaendelea kwani anatambua kuwa wapinzani wake watakuja kwa kushambulia sana ili wapate bao moja ambalo litawaweka salama kwenye mchezo huo.

Alisema wamejipanga kupata mabao ya mapema ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushika mchezo huo.

"Kama tukifanya makosa ya kuruhusu bao hasa tukiwa bado hatujapata mabao itatuweka kwenye presha, ni lazima sisi tuwe wa kwanza kupata goli na kuendelea kuumiliki mchezo," aliongeza kusema.

Alisema kwa sasa hana wasiwasi sana na safu yake ya ulinzi, lakini anachofanya ni kuitengeneza safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Leonel Ateba ili kuhakikisha inapata mabao mengi iwezekanavyo.

"Ili tufuzu makundi tunahitaji ushindi, na ili tushinde tunahitaji mabao, safu ya ushambuliaji ni lazima ihakikishe inafunga mabao na hilo ndilo ninalotilia mkazo mazoezini mara baada ya kumalizika kwa mchezo wetu wa kwanza kule Libya," alisema kocha huyo, raia wa Afrika Kusini.

Mchezo huo wa marudiano umepangwa kuanza saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa huku Simba ikihitaji ushindi wa aina yoyote kuweza kutinga hatua ya makundi.