ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA), Suleiman Kissoki amefariki usiku wa kuamkia leo Novemba 06, 2024 nyumbani kwake Tabata jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Nipashe Digital, Katibu Mkuu wa Shiwata, Michael Kagondela amesema hadi jana jioni, marehemu alikuwa ofisini Ilala Bungoni akiendelea na majukumu yake.
Kagondela amesema marehemu huyo amezikwa makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam saa 10 jioni ambako wadau mbalimbali wakiwemo wasanii, wanamichezo na wengineo walijitokeza kumsindikiza.
Kaka wa marehemu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA), Mussa Kissoki amesema ni jambo la kumshukuru Mungu kwa sababu kazi yake haina makosa.
Kissoki amesema kama binaadamu yatupasa tujiandae kwa ajili ya kifo kwa sababu hatujui siku wala saa mauti yatakapotufika.
Mbali ya kuwa Makamu Mwenyekiti wa Shiwata, marehemu ametumikia nyadhifa mbalimbali ikiwemo Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED