Zingatia haya kuandaa watoto kukurithi iwapo utatwaliwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:17 AM Jan 14 2025
Kama ni mkandarasi wa barabara watoto wako wawe sehemu ya wahandisi wajenzi.
PICHA: MTANDAO
Kama ni mkandarasi wa barabara watoto wako wawe sehemu ya wahandisi wajenzi.

MWAKA 2025 huu hapa. Wewe ni mmiliki wa migodi, viwanda, ardhi, mazao na mifugo. Ikitokea umetwaliwa je, umeandaa watoto wako kurithi na kuendeleza mali zako?

Kama hujafanya hivyo fikiria uanze sasa ikiwezekana. Ni kwa sababu kuna madai kuwa kama  wazazi na walezi wenye mali au utajiri wakifa, wameondoka na mali zao.

La msingi usiwabague watoto kijinsia wanawake na wavulana wape nafasi sawa.

Hakuna wakuziendeleza mara nyingi zitauzwa ili kugawana mali, zitafilisika na kusahaulika na migogoro mingi ya kugombania fedha, itafikishwa mahakamani kesi nyingi zikifunguliwa na kuwapo malalamiko hata ya wanafamilia kujiua.

Sababu mojawapo ni wazazi na walezi kushindwa kuwapa watoto mbinu au mikakati ili kuwaandaa kurithi na kuendeleza majukumu yao, pale  watakapofariki au kuumwa na kushindwa kuendeleza juhudi walizoanzisha.

Ni dhahiri yapo malezi kwa watoto kuwaandaa na hatima kubwa ya kuendeleza biashara au hata mali na kuiongoza familia kwenye uwekezaji.

Watanzania au ‘Wabongo’ wanafahamu na wanaona baadhi ya jamii mfano Wazungu, Waarabu na watu wengi wenye asili ya Asia kama China, India wanavyowaandaa watoto wao kuwa warithi wa biashara na miradi ya uwekezaji. 

Ni juhudi zinazofanywa mapema katika ukuaji wao. Unaweza kuwakuta watoto wakiuza madukani, au kuwa kwenye maeneo ya uzalishaji katika utoto wao ili kuelewa aina ya biashara.

Katika eneo hilo zipo pia familia zinazowaandaa watoto pengine kwa kuchagua mmoja maalum ambaye hutayarishwa kuwa kiongozi wa biashara, uwekezaji na familia nzima.

Pengine kwa Afrika hakuna juhudi kubwa zinazoonekana hivyo Watanzania wana haja ya kufanya jambo hilo ili kuendeleza na kudumisha mambo bora ya kiuwekezaji na haki za kumiliki na kutunza utajiri wa familia hata baada ya wazazi na walezi kuondoka.

Ethiopia na Somalia kuna jamii zinazofanya jambo hilo, lakini kwa Watanzania utamaduni huo haujafanikiwa na kuacha alama za watu kujifunza, japo kuna baadhi wameweza kuwaachia watoto wao biashara na urithi wa mali.

Nipashe imefuatilia kesi za mirathi mahakamani na kuona kuwa kitu kinachoshitua ni pale walezi wanapokosea katika kupenyeza maarifa, ujuzi wa biashara na usimamizi wa mali hizi kwa watoto ili kuwaandaa kuwa warithi wa sasa na miaka ijayo.

Tujiulize ni nini jamii nyingine zinafanya ambazo sisi Watanzania hatufanyi? Kwanini leo kuna biashara kubwa ambazo zinaishi karne nyingi mpaka zimesambaa dunia nzima kutoka kwa mwanzilishi, watoto na sasa ni kwa wajukuu hata vitukuu?

YAKUZINGATIA

Kuandaa kizazi chako chenye ushindi kuna vitu unatakiwa uvizingatie tangu wanapoanza kukua na kitaalamu jukumu linaloitwa ‘grooming’ ambalo linahusisha kile mtoto anachobeba tangu utotoni.

Watu wakumbuke kuwa hata kama utaacha wosia kama hujatengeneza kizazi cha ushindi mali na biashara zipo hatarini. Haziwezi kufika mbali pengine zitakwamia kizazi cha pili.

KUTAWALA PESA

Mtoto anaandaliwa kuitawala na kuiheshimu pesa na siyo pesa imtawale au kumzuzua. Katika mambo ambayo jamii ya leo yanamaliza vijana wengi ni kushindwa kuitawala pesa, ni somo ambalo halifundishwi shuleni au chuo chochote.

Inashangaza hata wanaosoma masomo ya biashara wanashindwa kuiweka chini ya miguu yao, hivyo wafundisheni watoto wakiwa na pesa wanapaswa kuzipeleka sehemu gani.

Anatakiwa kununua vitu gani vya faida gani kwake, maamuzi yake anapokuwa na pesa mkononi ni yepi? Anafanya nini na kwa wakati gani?

Katika kumwandaa mtoto mpe pesa na umuone anakimbilia kununua nini, mara nyingi wazazi na walezi wanawapa pesa watoto na wanakimbilia kununua pipi, biskuti, soda na wanataka baiskeli.

Umeshawahi kujiuliza mtoto ukimwelezea kinyume na hayo anaweza kuweka akiba yake mwenyewe, hata kama anahitaji baiskeli? Tengeneza naye bajeti mwambie tunaanza kuweka akiba ya baiskeli ashiriki na aone kuwa yeye anaweza kuitawala pesa.

Kama utashindwa kumfundisha kutawala pesa atafanya ufujaji ataona mali ni nyingi siku atakayoipokea mikononi mwake, atakimbilia kuimaliza na kuishia kufilisika.

VIKAO KUHAKIKI

Suala jingine la kumwandaa mrithi ni kuwa na  vikao vya mara kwa mara ukiwa na mtoto  kwenye usimamizi wa biashara, mali, kama mashamba, mifugo, ardhi, maduka, hospitali na viwanda au kampuni za huduma.

Mali hailindwi na mikono milegevu, kadhalika biashara hailindwi wala kutunzwa na mikono legevu, nguvu unayotumia kuwekeza katika mali zako na utafutaji wako hakikisha nguvu hiyo mtoto anaiona na unamwambukiza.

Kama ni shamba unakwenda kukagua mifugo au mazao hakikisha unakwenda naye mara kwa mara aone nini unachofanya, makubaliano unayoingia na wafanyakazi au washirika mbalimbali.

Lakini mzazi au mlezi unapomwandaa mtoto hakikisha unamwambia aangalie unachofanya na baada ya hapo ingia naye kwenye maongezi ya nini alichojifunza.

Kama ni biashara unafanya hakikisha unakwenda pamoja naye mwishoni mwa wiki na anashiriki, kama mtoto anaweza kuangalia video au katuni na akavutiwa eelewe unachomjengea pia atakishika, unatengeneza kiongozi anayejua anachofanya hata kama atapata changamoto, atakumbuka.

Mfundishe mtoto uaminifu, uthubutu, ujasiri, maadili na walezi na wazazi wengi wanawarudisha nyuma watoto kwa kuwanyima kufanya mambo ambayo wanahisi umri wao bado au wanaona ni kupoteza muda.

Hakuna sababu ya kuwakatisha tamaa watoto wanapoonyesha ubunifu na uthubutu wa aina yoyote wapewe nafasi na uungwaji mkono na kusifiwa kuwa anaweza.

Ikiwezekana shiriki naye katika anachofanya, biashara haitaki kichwa kilicholala inataka moyo wenye uthubutu na akili ambazo utaweza kukupeleka mbele.

Uthubutu ni taarifa kuwa yupo imara kwa utayari kwa mapambano mfundishe kufanya kazi kwa bidii na umfundishe kukataa uvivu, kama mzazi hukutenda kazi kwa mikono milegevu na umepitia mapito mengi mpaka kupata mali na mafanikio ni dhahiri kwamba maisha ya binadamu umefahamu kuwa sio lelemama.

Mikono milegevu huipoteza mali, watoto wafundishwe kufanya kazi na sio tu kazi ni kufanya kwa bidii na kukataa uvivu kabisa katika maisha yao.

Maisha ya vijana wengi tunayaona wanavyotaka vitu rahisi na kugubikwa na uvivu, hivyo lazima watoto wafunzwe kuweka akilini kuwa uvivu ni tatizo na ndicho kinachoangusha maisha ya wengi.

Hilo linafanikiwa kwa kushiriki naye kazi za nyumbani, kumpangia majukumu na kumwamsha mapema kwa mazoezi katika utoto wake.

NIDHAMU LAZIMA

Wazazi na walezi wafundisheni nidhamu watoto au warithi na kuachilia mbali nidhamu ya pesa fundishe mwanao nidhamu ya kujiheshimu, kumheshimu kila mmoja anayemzunguka na kujali muda, katika biashara nidhamu imebeba asilimia zaidi ya hamsini ya mafanikio.

Yeyote anayeshindwa kuwa na nidhamu mafanikio yanakuwa magumu kwake, ni nguzo ya muhimu itakayomfanya ajue namna ya kuwasiliana na jamii katika ngazi mbalimbali.

Mfundishe uvumilivu na ustahimilivu, kama wewe mzazi wakati wa kutafuta mafanikio, fedha na mali ulipitia magumu, basi vivyo hivyo uamini kuwa magumu katika maisha ni sehemu ya nyakati za wote za mafanikio ni hakika pia mwanao atapita nyakati hizi, iwe una pesa nyingi za kutosha au hauna mwandae mwano kisaikolojia azitambue nyakati hizi na aweze kuwa mvumilivu na kustahimili.

Aidha, awe na uwezo wa kufanya maamuzi ya busara katika nyakati kwani ndipo ubora wake utakapoonekana. Tengeneza mazingira ya kumfanya aweze kustahimili mambo madogo nyumbani, mpeleke kwa ndugu kijijini aone mazingira magumu na aishi usimweke ndani eti hutaki mwanao apate shida.

Wakati mwingine nafasi za Jeshi la Kujenga Taifa JKT zikitoka hakikisha mpambanie aende anachopita huko kinamjenga, anapaswa kuona pande zote za maisha.

LA MUMIHU

Kuandaa mtoto haijalishi uwe mfanyabiashara mkubwa au mdogo au mfanyakazi ni jukumu la kila mzazi au mlezi katika ngazi yoyote, mfano unaodhihirika wanaofanya hili pia na wanafanikiwa kuwapenyeza watoto wao ni wanasiasa.

Ukiwaangazia wanakupa taswira halisi nini wanafanya kwanini wewe ushindwe, tengeneza kizazi chako cha ushindi sasa, linda jasho na mali zako watoto hawatasahau njia na maarifa yako.