Wasimamizi mkaa wajipanga na staili ya uvunaji mkaa endelevu

By Christina Haule , Nipashe
Published at 06:38 AM Apr 18 2024
Shughuli za ukataji kuni za mkaa zikiendelea mkoani Morogoro.
Picha: Christina Haule
Shughuli za ukataji kuni za mkaa zikiendelea mkoani Morogoro.

JUMUIYA ya Maendeleo ya nchi za Ulaya (EDF) kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha nchini, sasa zinajipanga kuwanufaika wananchi zaidi ya 58,000 kwa matumizi endelevu ya bidhaa za misitu.

Hiyo inagusa misitu aina ya miombo kutoka vijiji 13 vinavyotekeleza mradi wa Suluhisho Jumuishi la Misitu na Nishati hai Tanzania (IFBEST) katika wilaya nne za mkoa wa Tanga.

Meneja wa Mradi wa Miaka Mitatu, wenye thamani ya shilingi bilioni 5.4 ujulikanao kitaalamu ‘Integrated Forest and Biomass Energy Solutions for Tanzania (IFBEST)’ kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG) Simon Lugazo, anasema watahakikisha wanatoa elimu ya usimamizi bora wa misitu ya vijiji.

Hiyo inatajwa kama ilivyofanyika kwa vijiji 35 mkoani Morogoro, katika kuimarisha uhifadhi na kutokomeza shughuli za kibinadamu zinazosababisha uharibifu wa misitu.

Lugazo anavitaja vijiji vya mkoani Tanga vitakavyonufaika na mradi huo; wilayani Handeni, ni; Gendagenda, Madebe, Kwamsisi, Mkalamo na Lusane, Mapanga, Nghobore, Mswaki, Sagasa/Kwa Mbogo. 

Pia, anakitaja kijiji cha Mkonde wilayani Kilindi; wilayani Pangani kuna Mtango, Mseko na Kwakibuyu na vijiji kadhaa wilayani Mkinga.

 Anasema, mradi huo utashughulikia masuala ya kuleta ufumbuzi endelevu wa uzalishaji wa mkaa, ambao anaueleza kitakwimu mkaa na kuni hutoa asilimia 93 ya nishati ya kupikia nchini.

 “Mkaa huzalishwa kwa tani na kwa mwaka huzalishwa tani milioni 1.8, takriban asilimia 44.2 na hizo huwa ni changizo la Bilioni 2.1 katika idara ya misitu nchini," anasema Lugazo.

 Aidha, Lugazo anasema uvunaji mkaa endelevu unaweza kufanyika na kunufaisha serikali na wananchi, kwakuwa asilimia 90 ya misitu nchini ni aina ya miombo, ambayo ina sifa ya kuchipua inapovunwa kitaalamu.

Hivyo, anaueleza mradi huo unakusudia kuandaa mipango ya ardhi na kuweka mipaka ya eneo la msitu wa kijiji kwa kuzingatia matumizi yaliyopo.

Lugazo anasema, mkakati walio nao utagawa msitu katika maeneo na vitalu; kama vile vyanzo vya maji, ufugaji nyuki, matambiko na eneo la uchimbaji madini jambo litakalosaidia kuondoa msongamano wa mambo na kuharibu utekelezaji.

MAFANIKIO MORO

Pia anautaja mradi huo ni matokeo ya mafanikio ya TFCG katika kuhifadhi misitu aina ya miombo uliofanyika mkoani Morogoro mwaka 2019/22 ambao hekta 133,579 zimehifadhiwa katika vijiji 35 vya mkoa.

Lugazo anaeleza kwamba, ukataji ovyo wa misitu umepungua kutoka asilimia 1.31 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 0.73 mwaka 2023.

Anasema, jamii kwa sasa vijiji hivyo 35 mkoani Morogoro zimenufaika kwa kupatiwa kiasi cha shilingi bilioni 2.09 kuanzia mwezi Disemba mwaka 2019 hadi Novemba 2022, zilizotokana na uvunaji endelevu wa mazao ya misitu kwenye vitalu vyao.

Inatajwa fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye vijiji vyao, ikiwamo ujenzi wa zahanati na vyumba vya madarasa, kukata bima za afya kwa ajili ya matibabu, kufungua biashara mbadala za kukuza uchumi wao.

WAZITO WA MISITU

Mkurugenzi Mtendaji wa TFCG, Charles Meshack anasisitiza jamii kuona haja ya kuunga mkono usimamizi shirikishi wa misitu, huku akifafanua uzoefu uliopatikana.

Hapo anazitaja ni utekelezaji wa usimamizi shirikishi wa misitu ya jamii (CBFM) uliofanywa na mashirika hayo mawili kwenye mkoa wa Morogoro, inaonyesha mbinu hiyo ni dhana au rasilimali bora ya kupunguza upotevu wa miti nchini. 

"Kuendeleza misitu kwenye ardhi ya kijiji kupitia CBFM huongeza ustahimilivu wa mabadiliko ya hali ya hewa na hivyo maeneo husika kuwa matokeo sahihi ya vipindi vya mvua na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi" Meshack anasema.

Hata hivyo, anasisitiza serikali kupitia wizara inayohusika inaendelea kusimamia marekebisho ya sheria na kanuni za misitu, ili kufanya USMJ kuendelea kutekelezeka na kuleta matokeo chanya.


 Meshack anawasa wananchi kuwa wadau muhimu katika usimamizi na ulinzi wa maliasili zilizopo ambao hawana budi kuelimishwa namna ya kuzitumia kwa maendeleo endelevu.

Anasema, Shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania kwa ushirikiano wa Mtandao wa Jamii wa Kuhifadhi Misitu Tanzania (MJUMITA), wanatekeleza mradi huo kwa sasa wamejipanga kuweka dira ya kuhifadhi na kufuatilia usimamizi shirikishi ya misitu ya jamii ili kukomesha upoteza wa misitu ambao unaongezeka mwaka hadi mwaka. 

 "Kuendeleza misitu kwenye ardhi za vijiji kupitia USMJ huongeza ustahimilivu wa mabadiliko ya hali ya hewa, na hayo yatafanikiwa iwapo tu, marekebisho ya sera ya misitu kwa mujibu wa sheria na kanuni zitaendelea kuboreshwa " anasema Meshack.

 Kwa mujibu wa Taarifa ya Tatu ya Mazingira nchini ya Mwaka 2019, takribani hekta 469,420 za misitu kwa mwaka hupotea kutokana na utegemezi mkubwa wa nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.

Taarifa hiyo inasema katika kurejesha misitu hiyo inayokatwa kila mwaka nchini, wananchi wanalazimika kupanda na kutunza ukubwa wa hekta 185,000 ambayo ni sawa na miti 2,280,000 kwa mwaka kwa muda wa miaka 17 mfululizo.

Katika hotuba iliyosomwa mwaka 2022 katika Mkutano wa Wadau wa Misitu na Serikali uliofanyika jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Deusdedit Bwoyo anasema serikali ina mpango wa kusimamia halmashauri zote  kutenga fedha za kuangalia misitu.

 Anasema itakuwa katika bajeti za kila mwaka kwa ajli ya kuangalia misitu, sambamba na kutumika kwenye shughuli za usimamizi na uhifadhi wa misitu.

 Bwoyo anafafanua kuwa kutengwa fedha kunapaswa kwenda sambamba na uwezo wa halmashauri, kwa  sababu bado kuna wasiofahamu umuhimu wa misitu katika mazingira ya kawaida, wakiingia kukata kuni na wakifanya shughuli za uharibifu wa misitu zinazokatazwa.  

Anasema Tanzania ina jumla ya misitu hekta mil 48.1, yakiwamo maeneo yanayoangukia katika ardhi za vijiji hekta milioni 22, kati yake ni chache zilizokidhi kuingia katika mpango wa usimamizi shirikishi.

Anasema, serikali kupitia wizara hiyo ipo katika mkakati wa kuhakikisha misitu mingi inahifadhiwa, kwa sababu iisipohifadhiwa kisheria, inakuwa hatarini kuharibiwa.

Hivyo, anasema tayari wameshatekeleza mkakati wa Sera ya Taifa ya Misitu, ambayo ndio dira ya kuendeleza misitu katika kipindi cha miaka 10 ijayo kuanzia mwaka 2021 hadi 203,1 ikiwa ni pamoja na kutengeneza mpango kazi wa usimamizi shirikishi wa misitu hasa katika vijiji wakilenga misitu mingi kuwa katika hifadhi za vijiji na kuhifadhiwa kisheria.

Anasema uhifadhi wa misitu ni wa pamoja tika Sera ya Misitu, sio wa Wizara ya Maliasili na Utalii pekee, pia wadau wa maendeleo kama, TFCG na MJUMITA kwa ajili ya kuendeleza misitu nchini.