Vipodozi havijaguswa lakini ni adui wa afya na mazingira

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 08:43 AM Jan 21 2025
Shehena za vipodozi zinazoingizwa nchini kila mwaka haziyaachi mazingira salama.
Picha: Mtandao
Shehena za vipodozi zinazoingizwa nchini kila mwaka haziyaachi mazingira salama.

KUJIPODOA kwa wanawake na wanaume hasa mijini na vijijini kwa kiwango kinachoongezeka kila mara ni jambo ambalo hivi sasa linazidisha changamoto kwenye mazingira na afya za watumiaji.

Hatari si kwenye kutumia vipodozi vyenye viambato vya sumu pekee lakini pia kuchafua mazingira na kutishia hatima ya viumbe majini na ardhini.

Vipodozi hutumiwa na mabilioni ya watu kuanzia wanasiasa, watu maarufu na mashuhuri duniani, wanapaka kucha rangi, dawa kwenye nywele za asilia ,mafuta na krimu kwenye ngozi,  urembo maalumu usoni, kwenye meno, manukato, rangi za midomoni na nywele bandia rasta kuvaa wigi.

Japo hakuna takwimu lakini huenda tasnia ya vipodozi ndiyo inayokua kwa kasi kuliko nyingine muhimu mijini na vijijini ikihusisha wafanyabiashara wakubwa wa nje na ndani ya nchi.

Ushuhuda uliopo kwenye majiji na miji kama  Dodoma, Mwanza, Mbeya, Moshi, Iringa  na Dar es Salaam unaonesha kwamba karibu kila kona kuna duka la vipodozi na saluni za kike na kiume.

Kadhalika stendi au vituo vingi vya mabasi vimesheheni vibanda vya vipodozi kuanzia krimu za kuchubua na kung’arisha sura, manukato au marashi, mafuta ya ngozi, nywele na rangi za aina mbalimbali kubadilisha nywele, ndevu na pia dawa za kuweka kwenye nywele hasa ‘relaksa na wevu.’

Wanapatikana pia wanaoosha na kupaka kucha rangi na zama hizi wameongezeka zaidi.

Wauza urembo kwenye pikipiki na baiskeli ni wengi mno, yote yakiashiria kuwa hiyo tasnia  ni kubwa na muhimu. 

Ni wakati sasa mamlaka za miji, majiji na vijiji zikafanya sensa ili kujua idadi au kuna maduka mangapi ya vipodozi na saluni za wanawake na vinyozi maeneo yao maana ni sekta inayokua kwa kasi na kuilazimisha kuchukua thadhari za kulinda mazingira na afya za wateja.

1

Mara nyingi wananchi wamesikia kutoka Shirika la Viwango (TBS) kuhusu kuwapo vipodozi vyenye viambato vya sumu, lakini ni vyema waende mbali na kuwaeleza wananchi kuhusu kiwango cha vipodozi vinavyoingizwa nchini na athari zake kimazingira.

Kadhalika, Mamlaka ya Mapato (TRA), halmashauri za miji, majijini na vijiji zisaidie kwa kubainisha idadi ya leseni za biashara zinazotolewa kila mwaka kwa ajili ya kuuza vipodozi na fedha zinazokadiriwa kupatikana na idadi yawatu waliojiajiri huko.

Mambo yasiishe hapo Wizara ya Fedha ione namna ya kuongeza kodi ya vipodozi katika bajeti yake ya 2025/ 26 kwa sababu sekta ya urembo inakua kwa kasi na ‘inalipa’ kwa lugha ya mijini.

HATARI ILIYOPO

Licha ya kutoa nafasi za ajira kwa maelfu ya vijana na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa Afrika yenye wasichana walimbwende na wanaume watanashati uhifadhi wa mazingira uko hatarini.

Ni kutokana na vifungashio vya vipodozi na mamilioni ya tani za nywele bandia zinazotumiwa mkwenye ulimbwende.

Sekta ya vipodozi inastahili lawama kwani ni chanzo cha kukwamisha mikakati ya kukabiliana na uchafu wa mazingira hasa kujaza vifungashio kama  makopo na mikebe ya plastiki kila mahali.

Tani za mamilioni ya mikebe ya kubebea urembo kuanzia krimu, poda, mafuta na vimiminika hutupwa kila mahali lakini mwisho zinaishia baharini au kwenye maziwa baada ya kujazwa kwenye mito na mikondo ya maji.

Athari za moja kwa moja ni vifo vya samaki na viumbe wengine wanaoishi majini na pia binadamu wanadhurika hasa kutokana na viambato vya sumu kutoka kwenye bidhaa feki za urembo.

Urembo kama nywele bandia au rasta na wigi zinatumiwa na mamilioni ya wanawake. Zinatumika mara moja na kutupwa hivyo kuongeza taka nyuzi za plastiki kila mahali.

Zimejaa ardhini, baharini na angani kwa vile zipo zinazochomwa na moshi wake mara moja unachufua anga.

2

Mabilioni ya tani za vipodozi hutengenezwa kila mwaka duniani na kuingizwa Tanzania pia na mikebe, mifuko ya nailoni, chupa na makasha yake hutupwa kila mahali kuanzia kwenye mashimo ya taka, kufukiwa ardhini, zikitoka kwenye saluni za kike na kiume, nyumbani, shuleni na popote penye watu.

Cha kusikitisha ni kwamba vifungashio hivyo vya plastiki na nywele bandia kwa kiwango kikubwa zaidi ya asilimia 70 huingia kwenye vyanzo vya maji kama maziwa na mito na mwisho hujaa baharini.

Ndiyo maana Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) linatabiri kuwa endapo mifuko, , vyombo na vifungashio vya  plastiki havitapigwa marufuku kufikia 2050, bahari na maziwa yatajaa plastiki kuliko samaki.

Aidha, UNEP mwaka  2015 ilitoa ripoti  kuwa baadhi ya vipodozi  vimesheheni chembechembe za plastiki ambazo ni hatari kwa mazingira.

Chembechembe za plastiki zinaonekana kwenye rangi za kucha, inasema UNEP.

UNEP inasema  chembechembe  za plastiki kwenye vipodozi zinajaa baharini au ndani ya vyanzo vya maji na ardhini kwa miaka mingi vikitishia ikolojia.

Pamoja na TBS kukamata vipodozi feki kila mwaka ikumbukwe kuwa bidhaa hizo ni hatari kwa afya ya wateja na kwa mazingira na sasa taifa lianze kampeni za kuamua jinsi ya kudhibiti vifungashio vya vipodozi.

Aidha, na nywele bandia nazo zisisahaulike kwa maana kila dakika zina wateja wanaofumua, kutupa na kusuka nyingine, kadhalika mawigi nayo yakitupwa au kununuliwa mapya, vyote vikiongeza taka za nyuzi za plastiki majini na ardhini. Hivyo usimamizi ni lazima  maana vinaongeza uchafuzi wa mazingira.