Viongozi wajao serikali za mitaa wawajibike kwa wananchi ipasavyo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:28 AM Nov 06 2024
Maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaofanyika mwezi huu.
PICHA: MTANDAO
Maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaofanyika mwezi huu.

ZIMEBAKI wiki tatu kufikia Jumatano Novemba 27 siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, jukumu linalofanywa kwa mujibu wa katiba ya Tanzania na sheria namba 287 ya halmashauri wilayani na 288 kwa halmashauri za miji na majiji.

Sina wasiwasi TAMISEMI kusimamia uchaguzi hata kama ni wizara ndani ya CCM, sheria zipo kukijitokeza ‘dukuduku’ wahusika waende mahakamani ili haki itendeke, kwa misingi ya sheria.  

Tanzania yapo makabila zaidi ya 120 hivyo mitazamo au fikira tofauti kuhusu uchaguzi, usimamizi wake kadhalika, harakati zinakuwa nyingi hasa ikizingatiwa wingi wa vyama vya siasa ambavyo kisheria vinapaswa kuteua wagombea watakaochaguliwa kuongoza serikali za mitaa. 

Kwa muktadha huo, malalamiko yanakuwa mengi, kutokana na fursa zilizopo mbele ya vyama vingi na wagombea husika. Nitoe rai kuwa uchaguzi utakaofanyika Novemba 27, uwe wa mfano, Afrika na duniani kwa kuwezesha kuwapata viongozi mahiri na wenye maadili mema, wenye uchungu wa kuwaletea maendeleo wananchi na taifa kiujumla.  

Kupitia viongozi watakaopewa fursa kuongoza serikali za vijiji na  vitongoji ikiwamo wenyeviti wa mitaa kwenye manispaa na jiji. Mifumo, iliyopo ya kiutawala iwawezeshe Watanzania kuwa na matumaini ya kuharakishiwa mwendokasi upatikanaji maendeleo vijjini na kwenye mitaa mbalimbali mijini.  

Kimsingi wengi ikiwamo viongozi kisiasa, watunga sera, wafanya maamuzi na watawala serikalini, tunaishi maeneo zilipo serikali za mitaa. Wilayani, manispaa au kwenye majiji kama Dodoma, Dar-es-Salaam. 

Kadhalika, ardhi imesambaa ziliko serikali za mitaa ikiwamo kila aina ya rasilimali zinazohitajika kwa maendeleo yetu. Mfano, chemchemu za maji, mito, mabwawa, maziwa, ardhioevu na kilomita zaidi ya 1,000 ukanda wa bahari kutoka Mtwara hadi Msumbiji, kisha Tanga mpaka Kenya. 

Kwenye maeneo ziliko serikali za mitaa pia kunapatikana madini, vito vya thamani mbalimbali; misitu, mbuga, mapori ya akiba na tengefu yenye wanyamapori wengi. Vilevile, vijiji viko wilayani na baadhi kwenye maeneo ya miji na majiji ambako Watanzania wanaishi. 

Tathmini nyingine inaashiria kuwa Watanzania walio wengi wanahitaji maendeleo ya uhakika, mathalani, huduma za kijamii zilizoboreshwa na kuimarika katika vijiji, kwenye vitongoji na mitaani sehemu za mijini, manispaa na majiji. 

Hata hivyo, siyo kwamba tangu kupata uhuru hakuna maendeleo yapo lakini hayalingani na miaka 63 tangu wakoloni waondoke Desemba 9, 1961. Bado hali siyo bora  hasa kwenye vijiji na katika mitaa mingi mijijini na majiji.  

Huduma za barabara ni duni, maeneo ya makazi hayana mipangilio mizuri, nyumba zinajengwa bila utaratibu wenye taswira ya mipango miji. Ni changamoto kubwa kupata huduma kama za kiafya hususani kufikisha wagonjwa, wajawazito vituo vya afya hospitali pamoja na kuondoa takangumu. Vilevile, mifumo majitaka ni duni hivyo kutiririka hovyo mitaani. 

Nimekuwa nikijiuliza Tanzania tunakwama wapi kujiletea maendeleo? Hakuna wataalamu wa fani mbalimbali kuwezesha wananchi, kusonga mbele kimaendeleo? Iwapo rasilimali tunazo mathalani, nguvukazi ipo ardhi ya kutosha nini hasa visababishi? 

Je, ni siasa, sera, mifumo au sheria, kiutawala au kutokuwa makini au  tunakosa maarifa? Naamini shughuli za kuwaletea maendeleo Watanzania zinahitajika wananchi wanakoishi, katika vijiji, vitongoji na mitaa mijini ambako kimsingi ndiko viongozi mahiri wa serikali za mitaa wanahitajika:  

Wenyeviti wa vijiji, vitongoji, wajumbe wa mitaa ambao watapatikana baada ya uchaguzi utakaofanyika nchi nzima Novemba 27, 2024. Kwa uzoefu tulionao, na kwa kuzingatia malalamiko, mitazamo kuhusu kero mbalimbali za wananchi, inaelekea chaguzi katika serikali za mitaa, hatutilii mkazo sana kama ilivyo mkuu wa madiwani, wabunge, rais na makamu wake.  

Inawezekana, kwa kujua au kutokujua, tukajikuta tunakosa werevu mzuri kuwapata viongozi wenye uwezo wa kuongoza na kusimamia maendeleo vijijini, kwenye vitongoji na mitaa mijini.

Ukiwasikiliza viongozi walio madarakani mathalani, kwenye mitaa baadhi wamekuwa walewale bila mabadiliko kwa muda mrefu.  

Ukimuuliza Mtanzania unayomwona anafaa kuwa kiongozi mahiri katika mtaa, iwapo anaweza kugombea, anakataa. 

Sababu huenda huko hakuna mvuto au motisha kama ilivyo kwa ubunge. Kadhalika, mahala viongozi wanapofanyia kazi ofisi za mitaa ni duni, ukilinganisha na umuhimu wake kwa kuzingatia ndiko huduma za msingi kwa wananchi zinakoanzia. 

 Baadhi wanaona ni kama kufanya kazi bila malengo halisi na hawawezeshwi inavyostahili kutimiza majukumu ipasavyo. Kwa uchaguzi wa Novemba 27, mamlaka za kuteua wagombea kwa nafasi mbalimbali wateuliwe walio makini sana na wenye upeo wa kutosha kuyasukuma maendeleo mbele.

 Ni wakati muafaka wa kuwapata viongozi wazalendo, wenye maono na mioyo ya kujituma, wanaopenda kuwajali wananchi na kushirikiana nao katika kutatua kero  na wawe karibu na wanaowaongoza wakishauriana nao mara kwa mara siyo tu kujitokeza nyakati za uchanguzi lakini wakishapata nafasi ya kuongoza hawaonekani hadi uchaguzi mwingine.

 Viongozi wa aina hiyo hawana uchungu wala nia ya kushirikiana na wananchi kutokomeza umaskini, ujinga na maradhi, maadui wakubwa tangu uhuru zaidi ya miaka 63 iliyopita. 

Kwa kuzingatia sera ya kupeleka madaraka mikoani, wilayani, vijijini na katika mitaa, ifahamike kuwa Watanzania wanataka mabadiliko ya kweli, wayaone maendeleo kivitendo siyo kinadharia. Uzalendo ni kuweka maslahi ya taifa na watu kipaumbele kuliko kujali maslahi binafsi kwa kujilimbikizia mali kupindukia.

  Wagombea wajiulize kwa miaka mitano ijayo nitafanya nini kijijini ili kuinua hali ya maisha kwa wananchi? Kadhalika kwenye mitaa wana mikakati endelevu na inayotekelezeka kuhakikisha miundombinu inaimarishwa ikiwepo huduma za kijamii zilizoboreshwa na kutatua kero mitaani?

Watanzania tujiulize je, tunaielewa vizuri dhamiri ya utawala wa serikali za mitaa au wengi wetu ‘tupotupo’ ili mradi tunaishi? Ni vizuri kutambua umuhimu wa serikali za mitaa vijijini pia mijini na majijini kwa nia njema ya kufikia maendeleo endelevu. 

Ni kweli hatujafikia hali hiyo lakini ajenda ni kupunguza kama siyo kuondokana na kero zisizo za lazima kwa wananchi. Iwapo msisitizo katika mipango mikakati ni kuleta maendeleo kwa wananchi pia mkazo uwekwe kwenye kuimarisha utendaji bora katika serikali za mitaa ambako ndipo wananchi wanakoishi.

Iko haja ya kutathmini kwa kina mifumo ya kuwaletea maendeleo wananchi kama ni halisi au vipi? Kama Mtanzania anayetamani kuwaona  raia wakiishi kwenye mazingira halisia kimaendeleo. Wahenga wetu walisema yaliyopita si ndwele tugange yajayo, kwa kumaanisha kuwa tusiangalie yaliyotutangulia bali tusonge mbele ipasavyo. Kwa mantiki hiyo, tujizatiti ipasavyo ili Novemba 27, 2024 baada ya uchaguzi tuweze kuwapata viongozi bora na siyo “bora-viongozi.” Tena kufanya kosa siyo kosa lakini kukosea ni pale unaporudia kosa kwa kujua au kutokujua. 

Malalamiko yanajitokeza mara kwa mara hivyo wakati umefika yawe historia. Hivyo, baada ya uchaguzi tutarajie kuyaona mabadiliko makubwa kiutendaji.