UCHAGUZI S/MITAA: Wagombea wamemaliza kazi leo ni kupiga kura

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:50 AM Nov 27 2024
Moja ya ofisi ya serikali za mitaa jijini  Dar es Salaam.
Picha: Mtandao
Moja ya ofisi ya serikali za mitaa jijini Dar es Salaam.

KAZI ya kuwasikiliza wagombea kwenye mikutano ya kampeni imemalizika,unapoamka leo kama umejiandikisha kupiga kura kuchagua viongozi wa serikali za mitaa ndiyo siku yenyewe ya kupiga kura yako, kwa hiyo wahi kituoni.

Ukumbuke uchaguzi wa serikali za mitaa mwingine, utafanyika 2029.

Mwananchi ulitakiwa kujiandikisha  kwenye daftari la wakazi la mtaa mwezi uliopita, ili kuchagua kiongozi wa kijiji kama unaishi kijijini kadhalika na kitongoji lakini kwa wakazi wa mijini ni kuwachagua viongozi wa mitaa.

Uchaguzi huu unawahusu wananchi wa ngazi za chini ambao ndiyo wanaoutoa mamlaka kwa serikali zote za mitaa na ile kuu, mambo yakikamilika baada ya uchaguzi wa sasa wa serikali za mitaa kisha mkuu wa 2025 unaowachagua madiwani, wabunge, wawakilishi, marais na makamu wao.

Kama ulivyo uchaguzi mkuu, wa serikali za mitaa nao ni muhimu  na umepewa umuhimu mkubwa, serikali ikitangaza rasmi kuwa leo ni  siku ya kuwachagua viongozi kwa hiyo hakuna kazi za kiofisi ni  mapumziko ili kila mmoja atumie wakati huo  kupiga kura na kupunguza visingizio visivyo na sababu vya kutokuchagua viongozi wao mojawapo ikiwa kwenda kazini.

Wananchi wakumbuke kuwa vituo vya wapigakura vinafunguliwa saa 2:00  asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni, hivyo waweke ratiba na kutumia haki yao ambayo ni kuwapata viongozi bora si bora viongozi.

Kumbukeni masuala mengi yanayohusu maendeleo yanaanzia kwenye ngazi za chini mfano vijijini, mitaani na vitongojini katika kipindi hiki ndiyo wakati wa kuangalia mbivu na mbichi kuchagua walio bora.

Mfano kuna viongozi ambao katika miaka mitano hawakuweza hata kuweka wavu kwenye madirisha ya ofisi za vijiji au serikali za mitaa wala  kujenga vyoo, kuweka umeme au kuezeka ofisi, kuzikamilisha pale wenzao wa 2014 walioondoka 2019 walipoishia.

Ndiyo wakati wa wananchi kujihoji wanahitaji viongozi wa namna hiyo? Watu wasio watendaji wana sababu ya kuendelea kubaki ofisini? Ikumbukwe kiongozi anayetaka kuendeleza uzalendo wa tumbo au kusaka tonge kwenye maendeleo siyo mahala pake. Hivyo hahitajiki.

Kwa mfano huo ni lazima kuchagua viongozi wanaoweza kubadilisha fikira na kuleta maendeleo kama ambavyo wapo baadhi ya watu Goba jijini Dar es Salaam wamehamasisha wananchi kujenga vituo vya polisi, barabara za mitaa na kuboresha makazi yao.

Pamoja na kwamba si watendaji wa mitaa, lakini wamejaa hamasa ya kufikia maendeleo na maisha bora kwa wananchi.

 Kwa baadhi ya wananchi miaka mitano wanakiri  imekuwa michungu kama shubiri kutokana na kukosa huduma za kijimii lakini pia kukosekana viongozi wa kuwasemea na kutetea kwenye kuingizwa kwenye mipango ya maendeleo.

Kwa mfano kuna maeneo mengi jijini Dar es Salaam,  watu wamekosa msaada  mathalani wakazi wa Mbezi Msumi, eneo hilo linazungukwa na majirani kadhaa mfano  Mbopo, Madale na Makabe. Ni sehemu zenye majisafi na salama, lakini Msumi wanakunywa ya mabondeni na kila uchao watoto na jamii ina maradhi ya maambukizi ya njia ya mkojo au UTI. 

Wananchi wanashindwa kujua inakuwaje waishi kisiwani kwenye suala la maji wakati majirani wanaowazunguka wana maji ya kunywa safi na salama?  Kadhalika  Msumi sehemu ambayo ni karibu na Stendi ya Mbezi Magufuli haina barabara na hakuna kiongozi wa kuzungumzia kuikwangua na kuishindilia kwa katapila. Madaraja pia yamekatika ni kisiwa. 

Tangu mwaka jana mwezi Desemba daraja maarufu la Kwa Ndee lilikatika na eneo hilo kukosa mawasiliano na Madale, Tegeta Nyuki na yeyote aliyetaka kupitia darajani hapo. Kwa miaka mingi ofisi ya serikali ya mtaa haina umeme hali imebakia hivyo kwa miaka mingi.

Wapigakura wa King’azi B, Dar es Salaam, nao walikuwa kwenye uongozi legelege kuanzia 2019 hadi sasa. Wanaeleza kuwa uongozi wa serikali za mitaa ulioondoka 2019, ulijenga ofisi kumaliza boma, kuliezeka, kuweka madirisha ya chuma (grill) na kuwa na ofisi.

Hata hivyo baada ya uchaguzi wa 2019 waliochaguliwa hawakufanya chochote kukamilisha ujenzi wananchi wakawa wanahudumiwa kwenye gofu, inakuwaje kwa uongozi kama huo?  

Kuna visa vingi na masimulizi ya kila namna kuhusu uongozi wa serikali za mitaa kwenye miji mikubwa na midogo na vijiji pamoja na vitongojini.

Baadhi wanahusishwa na kuendeleza migogoro ya ardhi na wengine kuuza ardhi usiku ili wapewe hela au asilimia 10 ya gharama mnunuzi anazolipa.

Viongozi wa serikali za mitaa, baadhi wamekuwa lawamani kuwa wanachojitahidi hasa mijini na majijini ni kutafuta maslahi binafsi kama vile kuuza viwanja kwa wanunuzi zaidi ya mara mbili na wengine wakidaiwa kutishia mafundi wanaojenga ‘saiti’ na kuwalazimisha kusimamisha ujenzi ili wapate chochote kwa kutumia mgongo wa kukosa kibali cha ujenzi.   

Viongozi kumbukeni kuongoza ni kuwa mtumishi wa wengine na siyo kujinufaisha kwa mambo ambayo hayana mifugo, lakini wakishindwa kufanikisha masuala ya usalama wa mali za wananchi kwenye kupambana na wahalifu.   

 Kuwapo kwa serikali za mitaa ni kufanikisha ugatuzi yaani kupeleka madaraka kwa wananchi na kufanyakazi kwa ukaribu zaidi na wana vijiji, vitongoni na mtaa kuanzia kutoa huduma, kupanga na kutekeleza mipango ya wananchi inayoandaliwa wilayani na kwenye serikali kuu.