Rekodi na takwimu dabi ya Mzizima, Simba, Azam Z'bar

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:36 AM Sep 30 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Winga wa Simba, Kibu Denis, akipambana na kipa wa Azam FC, Mohamed Mustafa, kuwania mpira uliorudishwa vibaya na mmoja wa mabeki wa timu hiyo, na kusababisha kizaazaa langoni, ingawa baadaye mwamuzi, Elly Sassi, alidai Kibu alifanya madhambi...

BONGE la mechi lilichezwa Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, kati ya Azam na Simba.

Kwa sasa mechi inayozikutanisha timu hizo mbili inajulikana kama 'Mzizima Deby'. Ilikuwa ni mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyomalizika kwa Simba kushinda mabao 2-0.

Ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa makocha wa timu zote mbili, Fadlu Davids raia wa Afrika Kusini akiwa na kikosi cha Simba, huku cha Azam kikiongozwa na Rachid Taoussi akitokea nchini Morocco.

Mara ya mwisho zilipokutana, Mei 9, mwaka huu, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, Simba ikishinda mabao 3-0, ikiwa chini ya Juma Mgunda, na Azam ilikuwa chini ya Msenegal, Youssouph Dabo.

Katika makala haya, tumekukusanyia takwimu mbalimbali za mchezo, wachezaji pamoja na rekodi za timu hizo, tukiziwasilisha kwa mtindo wa namba, twende sasa... 

47# Dakika hii ndipo Simba alipoandika bao la pili lililowekwa kwenye kamba na Fabrice Ngoma, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa, Mohamed Mustafa kutokana na mpira wa kichwa uliopigwa na Kibu Denis, aliyeunganisha faulo ya Jean Charls Ahoua.

 14# Ni dakika ambayo straika wa Simba raia wa Cameroon, Christian Ateba, alifunga bao la kwanza katika mchezo huo.

Straika huyo aliwazidi mbio na nguvu, mabeki wa Azam ambao walikuwa wakimkimbiza, kabla ya kuanza kumsukuma, lakini hakuanguka ili timu yake ipate walau penalti, badala yake aligangamala na hatimaye kuukwamisha mpira wavuni. 

13# Hii ni namba ya jezi ya mfungaji wa bao la kwanza la Simba Ateba ambaye alisajiliwa msimu huu akitokea, USM Alger ya Algeria. 

11# Idadi hii ni ya wachezaji ambao hawakuwapo katika mchezo uliochezwa Zanzibar, lakini walicheza katika mechi ya mwisho ambayo timu hizo zilikutana Mei 9, mwaka huu.

Simba haikuwa na wachezaji sita ambao ni Ayoub Lakred, Israel Mwenda, Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute, Freddy Michael, na Ladack Chasambi, huku Azam ikiwakosa Nathaniel Chilambo, Paschal Msindo, Yanick Bangala, Yahya Zayd na Kipre Junior. 

10# Idadi hii ya wachezaji ndiyo iliyocheza mechi zote mbili za mzunguko wa pili msimu uliopita na ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.

Simba ilikuwa na wachezaji wanne tu ambao walicheza pia mechi iliyopita, nao ni Mohamed Hussein 'Tshabalala', Fabrice Ngoma, Che Fondoh Malone na Edwin Balua aliyeingia kipindi cha pili, huku wa Azam ambao walicheza mechi ya mwisho msimu uliopita wakiwa ni kipa Mohamed Mustafa, Yeison Fuentes, Feisal Salum, Gibril Sillah, James Akaminko, na Idd Selemani Nado. 

6# Namba ya jezi ya kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma, aliyefunga bao la pili katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam, Alhamisi iliyopita, Uwanja wa New Amaan, Zanzibar. 

5# Jumla ya wachezaji sita wa Simba waliugusa mpira kabla ya bao la kwanza dhidi ya Azam FC kuingia nyavuni. Ulianzia kwa Moussa Camara, akampelekea pembeni kidogo, Fondoh Che Malone, ambaye aliurudisha ndani kidogo kwa Abdulrazack Hamza, naye aliupeleka mbele kwa Joshua Mulate, ambaye alimsogezea Jean Charles Ahoua, akapiga pasi ya juu pembeni winga ya kulia ambayo ilimkuta mfungaji, Ateba aliyeanza safari ya kwenda kuuweka wavuni. 

2# Namba hii inasimama kwa Ngoma ambaye ni mara ya pili mfululizo kufunga bao dhidi ya Azam FC.

Alifanya hivyo Ligi Kuu msimu uliopita, Mei 9, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni mechi ya mzunguko wa pili. Mechi zote hizo alifunga mabao ya pili kipindi cha pili.

Alifunga bao la pili dakika ya 77, kwenye ushindi wa mabao 3-0, mengine yakiwekwa wavuni na Sadio Kanoute na David Kameta. Katika mchezo uliopita, alifunga tena bao la pili katika ushindi wa mabao 2-0 mjini Zanzibar.

 1# Ni mara ya kwanza kwa mechi ya Dabi za Mzizima ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kuchezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

 0# Azam haijapata bao lolote katika michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara ikicheza dhidi ya Simba. Alhamisi iliyopita ilichapwa mabao 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, na mechi ya mzunguko wa pili msimu uliopita, Mei 9, mwaka huu, haikuambulia kitu, ikifungwa mabao 3-0.