Rekodi 5 kali Yanga ikipoteza kwa Azam

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:22 AM Nov 04 2024
Nahodha na beki wa Yanga,Bakari Mwamnyeto, akimdhibiti straika wa Azam FC,Nassor Saadun, ili kulinda lango lao wakati wa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Mchezo huo uliomalizika kwa Yanga kuchapwa 1-0.
Picha: Mpigapicha Wetu
Nahodha na beki wa Yanga,Bakari Mwamnyeto, akimdhibiti straika wa Azam FC,Nassor Saadun, ili kulinda lango lao wakati wa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Mchezo huo uliomalizika kwa Yanga kuchapwa 1-0.

MECHI ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa juzi, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, ilishuhudiwa Yanga ikipoteza kwa bao 1-0.

Yanga imepoteza mechi kwa mara ya kwanza baada ya kushuka dimbani mara nane kwenye Ligi Kuu bila kupoteza msimu huu na kuvunja rekodi iliyoiweka yenyewe msimu uliopita ilipopoteza baada ya michezo mitatu, ikifungwa na Ihefu mabao 2-1, Oktoba 4, mwaka jana katika Uwanja wa Highland Estates, Mbarali mkoani Mbeya.

Ni msimu ambao ilianza kwa kushinda mabao 5-0 dhidi ya KMC, ikashinda tena kwa idadi kama hiyo dhidi ya Tanzania Prisons, kabla ya kukutana na kipigo hicho, ambacho pia kiliweka rekodi ya kuruhusu bao kwa mara ya kwanza kweye Ligi Kuu.

Katika makala haya tunakuletea rekodi tano kali zilizowekwa  baada ya mchezo huo kutamatika. 

1# Yanga kupoteza kwa mara ya kwanza

Hatimaye Yanga imepoteza mechi yake ya kwanza msimu huu baada ya kucheza michezo minane.

Msimu huu ilianza ligi kwa kuifunga Kagera Sugar mabao 2-0, KenGold bao 1-0, ikaifunga KMC 1-0, kabla ya kuitandika Pamba Jiji mabao 4-0, Simba bao 1-0, JKT Tanzania 2-0, Coastal Union 1-0, kisha mchezo wa mwisho kabla ya kupoteza ikashinda 1-0 dhidi ya Singida Black Stars. 

2# Sillah wa kwanza kugusa nyavu za Yanga

Mchezaji wa Azam raia wa Gambia, Gibril Sillah, amekuwa wa kwanza kugusa nyavu za Yanga ambayo ilikuwa haijaruhusu bao lolote kwa michezo minane iliyopita ya Ligi Kuu.

Bao hilo la dakika ya 32, mbali na kuweka rekodi ya kuwa mchezo wa kwanza kufunga bao kwenye lango la Yanga, pia imeipa Azam ushindi wa bao 1-0 na kuchukua pointi tatu kwenye mchezo huo. 

3# Mara ya mwisho Yanga ilifungwa na Azam

Ni kama Azam FC ilianzia ilipoishia kwani mara ya mwisho zilipokutana, Machi 17, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita, ilishinda mabao 2-1.

Yanga mara ya mwisho ilifungwa mabao hayo dhidi ya Azam, na imelinda rekodi ya kutopoteza kwenye Ligi Kuu mpaka pale ilipokipiga tena kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu huu na kuchapwa bao 1-0

 4# Sillah anajua siri ya Diarra?

Hii ni mara ya tatu kwa winga wa Azam, Sillah kumtungua kipa wa Yanga, Djigui Diarra raia wa Mali, katika michezo yote  ambayo timu hizo zimekutana.

Juzi alifunga akimtungua Diarra dakika ya 32 na kuipa Azam ushindi wa bao 1-0, lakini pia alimfunga dakika ya 19 katika mchezo wa mzunguko wa pili msimu uliopita uliochezwa Machi 17, mwaka huu, Azam ikiifunga Yanga mabao 2-1, akisawazisha bao la dakika ya 10 la Clement Mzize kabla ya Feisal Salum kufunga la ushindi dakika ya 51.

Sillah, ambaye alisajiliwa na Azam, 2023 akitokea Klabu ya Raja Casablanca ya Morocco, alimfunga kipa huyo katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita, uliochezwa Oktoba 23, mwaka jana, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, japo Azam ilifungwa mabao 3-2, yote yakifungwa na Stephane Aziz Ki, lakini Sillah alimtungua Diarra dakika ya 19, na lingine likifungwa na Prince Dube kwa mkwaju wa penalti kabla ya kuhamia Yanga msimu huu.

 5# Yanga imepoteza nyumbani

Yanga imeungana na timu za Simba, Azam na Singida Black Stars si kupoteza mechi moja tu, bali kupoteza uwanja wa nyumbani.

Mechi moja moja ambazo timu hizo zimepoteza, zilicheza kwenye viwanja vyao vya nyumbani. Yanga iliutumia Uwanja wa Azam Complex juzi kama wake wa nyumbani, ikafungwa kwa mara ya kwanza dhidi ya Azam bao 1-0, ikiungana na Singida Black Stars ambayo ilifungwa kwa mara ya kwanza Oktoba 30, mwaka huu, ikiutumia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kama wake wa nyumbani dhidi ya Yanga, ikachapwa bao 1-0.

Azam, nayo iliutumia uwanja huo kuwa wa nyumbani ilipocheza dhidi ya Simba, Septemba 26 na kutandikwa mabao 2-0, huku Simba nayo ikifungwa bao 1-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya Yanga, mchezo ambao kikanuni ilikuwa ni mwenyeji.