KATIKA makuzi yangu ya miongo kadhaa sasa, nimeshuhudia watu wakizaliwa na wengine kufa. Nimeshuhudia wanapozaliwa watu, wazazi wao huhifadhi tarehe ya kuzaliwa na hata wanapofariki dunia, pia ndugu huhifadhi tarehe.
Kwa wanaozaliwa hufanyika hilo kwa ajili ya kumbukizi ambayo huendana na sherehe au hafla, siku ambayo bahati mbaya sana imepewa jina la Kiingereza; ‘Hepi Besi Dei’ (Happy Birth Day), ambayo watu hujiandaa na kukata keki, kula na kunywa.
Siku nyingine hii isiyo na jina la Kiingereza, pengine ingeitwa ‘Happy Desi Day (Happy Death Day)’, hukumbukwa, lakini haina mashamshamu ya keki, kula na kunywa na kushangilia kama hiyo nyingine ya HBD! Kwanini? Pengine ni kutokana na majonzi. Lakini wanasema zote ni sherehe.
Watanzania tumekuwa tukiyafanya haya siku zote, tukishiriki sherehe hizo kwa namna moja au nyingine, zikitofautiana kutokana na kipato,pia mazingira na muktadha unaokuwapo wakati wa sherehe hizo, hususan ya kuzaliwa.
Mnamo Oktoba 14, 1999, Rais Benjamin Mkapa alipotangaza kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki akiwa Uingereza, nchi nzima ilizizima pamoja na majirani, pia ulimwengu wote ulishituka, kutokana na umaarufu aliyokuwa nao.
Tulimzika na kujipa pole, hata kuamua kuwa Oktoba 14 ya kila mwaka, basi iwe ni kumbukizi yake kitaifa, kwani ndiyo njia ya kumuenzi huku tukiamini na kutenda aliyoyaamini.
Ili kuongeza nguvu, tukaunganisha na kuzima Mwenge kukamilisha mbio zake nchi nzima.
Tulifanya hivyo, tukiamini kwamba kumbukizi itakuwa na nguvu, ili watu wasimsahau mapema kiongozi huyo.
Ni kwamba ikifika siku hiyo, tumkumbuke kwa sala na mengine, pia tushangilie kuzima Mwenge kwa sherehe kubwa.
Tumeendelea kufanya hivyo na mpaka siku ya Oktoba 14 mwaka huu, tukafanya hivyo jijini Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, kwa sherehe kubwa sana iliyojaza watu pomoni nje na ndani ya uwanja, mpaka mshereheshaji akasema “Mwanza imeitika.”
Kwa aliyekuwapo akishuhudia sherehe ile, bila shaka aliona jinsi siku hiyo ambayo imekuwa akiitwa ya Nyerere, ilivyogubikwa shamrashamra za Mwenge, kumbe siku ya kifo ikageuka kama ya kuzaliwa kwa Mwalimu.
Walioelewa, wakaibuka na kuhoji kwanini siku ya Nyerere isiwe aliyozaliwa yaani Aprili 13? Kwani alizaliwa Aprili 13, 1922, sasa kwanini tushangilie ‘Death Day’ badala ya ‘Birth Day’? Vinginevyo, Mwenge uzimwe siku nyingine na si Oktoba 14, hiyo aachiwe Mwalimu kukumbukwa.
Kwa mashuhuda, siku ile pale Kirumba, kilichojitokeza na kutawala ni Mwenge, isipokuwa picha moja ya Nyerere iliyobebwa na maandamano ya vijana 1,000 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama mpaka Mwanza, kukumbuka siku ya kifo cha Mwalimu Nyerere.
Kwingineko, tulishuhudia halaiki ya Mwenge, sare maalumu za Mwenge zenye picha ya Mwenge bila picha ya Mwalimu Nyerere aliyekuwa na siku yake, hotuba kuhusu mbio za Mwenge,na kauli kidogo kumhusu Mwalimu.
Kwa kuwa siku ya Nyerere, tulitazamia basi hata familia yake angalau ipate kijifursa cha kutoa salamu, lakini hatukuliona hilo, bali tukaishia maandamano ya sungusungu na nyimbo za wasanii wa kizazi kipya, ambao baadhi yao pengine hata hawakupata kumwona Nyerere.
Ni kawaida kuwa sherehe za ‘Birth Day’ huweza kufanyika kokote, iwe nyumbani au hata hotelini na kwingineko, ili mradi kuna keki, chakula na kinywaji, lakini ‘Death Day’ itafanyika kama si nyumbani, basi makaburini ambako wafiwa huenda kuzuru kaburi kuliombea na kulisafisha.
Lakini ya Nyerere hufanyikia kokote kunakozimwa Mwenge, huku kaburi lake likibaki kutembelewa na ndugu na jamaa wa karibu, sisi wengine tukisikiliza nyimbo za ‘Koma Sava (Comment ca va)’ na mengine tofauti!
Unajiuliza hivi kweli siku hiyo kama kweli tulikuwa na lengo la kumkumbuka na kumuenzi Baba wa Taifa, tulishindwa kutafuta vikundi vya bendi au kwaya vilivyotunga, kuimba na kurekodi nyimbo za kumsifu Mwalimu, badala ya ‘singeli’ zenye maneno tofauti au hazihusiani?
Yawezekana hatujipangi au tunaacha tu bora liende, ili mradi...! Hatutamuenzi Mwalimu kwa usahihi zaidi, kama tutaendelea na utaratibu wa kumpunguzia nafasi na sehemu kubwa inakuwa na Mwenge. Dawa naona ni kutenganisha siku hizo, kila jambo lifanyike siku na mahali pake tofauti.
Hiyo itatufanya tukae chini na kutafakari aliyofanya Nyerere kwa nchi hii na kuyafuata, kama kweli tunataka au tumedhamiria kwa nyoyo za dhati, badala ya kuendekeza yaliyo tofauti. Tutafakari, itakuwaje Oktoba 14 mwakani!
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED