Gamondi yametimia, apigwa faini

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:07 AM Nov 16 2024
Miguel Gamondi.
Picha:Mtandao
Miguel Gamondi.

HATIMAYE yametimia, uongozi wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ya jijini, Dar es Salaam umetangaza rasmi kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu yao, ambaye ni raia wa Argentina, Miguel Gamondi, imethibitishwa.

Hadi kufikia jana, Gamondi, alikuwa  amekiongoza kikosi cha Yanga kwa muda wa msimu mmoja na nusu.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo inasema wameamua kuvunja mkataba bila kutaja sababu yoyote huku ikiongeza mchakato wa kusaka kocha mpya umeshaanza haraka.

"Uongozi wa Yanga unapenda kuutaarifu umma umevunja mkataba na Kocha Mkuu wa kikosi cha kwanza, Gamondi (Angel Miguel).

Vile vile, uongozi umesitisha mkataba wa kocha msaidizi wa kikosi hicho, Moussa Ndaw, klabu inapenda kuwashukuru na kuwatakia kila la heri katika majukumu yao mapya.

Tayari mchakato wa haraka wa kutafuta kocha mpya wa kikosi chetu unatarajiwa kukamilika hivi punde," ilisema sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.

Taarifa hiyo inakamilisha tetesi za kutimuliwa kwa kocha huyo kufuatia kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara hivi karibuni.

Yanga iliruhusu kufungwa na Azam FC bao 1-0, mechi iliyochezwa Novemba 2, mwaka huu na siku tano baadaye ikachapwa na Tabora United mabao 3-1, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mbali na vipigo hivyo, taarifa zilisema kocha huyo amekuwa akiwaamini baadhi ya wachezaji, huku wengine akishindwa kuwapa nafasi ya kuonesha uwezo wao.

Hata hivyo, Gamondi, aliitengeneza Yanga imara iliyokuwa ikicheza soka la kasi, bila kutegemea mchezaji mmoja kama awali ilipokuwa ikimtegemea zaidi mshambuliaji, Fiston Mayele.

Gamondi ambaye ameweka rekodi ya kuifikisha Yanga katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, alitua Yanga kuchukua mikoba ya Nasreddine Nabi, ambaye kwa sasa anaifundisha Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Chanzo chetu kinasema kocha raia wa Algeria, Kheireddine Madoui, anatarajiwa kuwasili nchini kesho alfajiri ili kuchukua mikoba ya Gamondi akitokea CS Constatine FC ya nchini kwao.

Taarifa zaidi zinasema, tayari uongozi wa Yanga umempa mkataba wa miaka miwili, Abdihamid Moallin, ambaye mapema wiki hii alitangaza kujiuzulu nafasi yake ndani ya klabu ya KMC kuwa Kocha Msaidizi.

Pia Mjerumani Sead Ramovic, naye anahusishwa na mchakato wa kutua Jangwani.

Wakati huo huo, Gamondi amekumbana na balaa jingine baada ya kufungiwa michezo mitatu na kupigwa faini ya Sh. milioni mbili kwa kosa la kumsukuma na kumwangusha chini kocha wa viungo wa Singida Black Stars, Sliman Marloene, baada ya kutokea mabishano baina yao, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, timu hizo zilipokutana Oktoba 30, mwaka huu.

Kamati hiyo pia imefuta adhabu ya kadi ya njano aliyoonyeshwa beki wa Yanga, Ibrahim Hamad 'Bacca', katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Oktoba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Kamati imesema imejidhihirisha kutokana na marejeo ya picha mjongeo na taarifa za wataalam kuwa Bacca hakustahili adhabu hiyo.