JESHI la Polisi mkoani hapa linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Sagali Masanja (62) mkazi wa Kijiji cha Mahene, wilayani Nzega kisha kumkata titi na sehemu za siri na kuondoka navyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Richard Abwao, alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi, saa 7:00 usiku, huku chanzo kikitajwa ni imani za kishirikina.
Alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya mauaji ya bibi huyo wakimtuhumu kuwa mchawi akidaiwa kuhusika na tukio la kumroga mtoto aliyefia kisimani.
Kamanda Abwao alisema bibi huyo aliuawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili kisha wauaji kuondoka na titi moja, sehemu zake za siri na pia kuchukua begi lake la nguo.
“Baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa wananchi tulifika eneo la tukio na kukamata watuhumiwa watatu ambao ndio waliotuma wauaji kwenda kufanya tukio hilo,” alosema Abwao.
Aliwaja watuhumiwa hao kuwa ni Lucia Mabula (36), mkazi wa Kijiji cha Mahene anayedaiwa kuwatafuta wauaji na kuwalipa Sh. 200,000 ili kutekeleza mauaji ya bibi huyo kwa madai kuwa alimroga mtoto wake mwaka 2023 na kufia kisimani.
Watuhumiwa wengine ni Makenzi Mabula (49) ambaye ni mume wa Lucia Mabula na Ramadhani Kurwa (38) wote wakazi wa Kijiji cha Mahene.
Kamanda Abwao alisema baada ya tukio hilo, wananchi waliwakimbiza watuhumiwa hao na kuwakamata wawili akiwamo mganga wa kienyeji, Sana Maganga (66) aliyekuwa akiwapaka dawa ili wasikamatwe, ambaye pia ni mama mzazi wa Shilinde Kaseko.
Alisema wengine waliokamatwa ni pamoja na Masumbuko Ngassa (33) mkazi wa Kijiji cha Segese Wilaya ya Kahama, mkoani Sinyanga na Shilinde Kaseko (30) mkazi wa Kijiji cha Seki, wilayani Nzega.
Alisema baada ya kukamatwa, wananchi wenye hasira walijichukulia sheria mkononi na kuwapa kipigo kikali kisha kuwachoma moto na kupoteza maisha.
Alisema watuhumiwa hao baada ya kukamatwa walikutwa na viungo vya binadamu ambavyo ni titi, sehemu za siri na vitu walivyokuwa wameiba.
Kamanda Abwao alitoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kuwataka kuachana na imani za kishirikina kwa kuwa ni imani potofu na zinaongeza fitina, chuki na uhasama pia zinasababisha madhara kwa jamii.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED