MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Singida, Jackson Jingu, ameshindwa kutetea nafasi yake baada ya kushindwa vibaya na Diwani wa Kata ya Ntuntu wilayani Ikungi, Omari Mohamed Toto.
Kutokana na hilo, Jingu ametangaza Uchaguzi Mkuu 2025 atawania ubunge katika Jimbo la Singida Magharibi.
Katika uchaguzi huo uliofanyika juzi mjini Singida ambao pia, ulihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, Jingu aliambulia kura 30 dhidi ya mpinzani wake, Toto aliyeibuka kidedea kwa kupata kura 52, huku nafasi ya tatu ikishikwa na Wilson Luta aliyepata kura tano.
Msimamizi wa uchaguzi huo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Patrick Ole Sosopi, akitangaza matokeo hayo alisema nafasi ya Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Singida, aliyeshinda ni Samweli Maro kwa kupata kura 58 na hivyo kufanikiwa kutetea nafasi yake hiyo.
Alisema nafasi Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) Mkoa wa Singida, ilichukuliwa na Joseph Salum huku uchaguzi wa nafasi Katibu wa BAVICHA ilishindwa kufanyika kwa sababu waombaji wote kubainika hawana sifa.
Sosopi alisema nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) ilichukuliwa na Zaitun Jumanne na Katibu wa BAWACHA alichaguliwa Beatrice Robert.
Akizungumza baada ya kutangaza matokeo, Jingu alisema pamoja na kwamba ameshindwa kutetea nafasi yake, hawezi kuhama chama kama ambavyo wengine wamekuwa wakifanya baada ya kushindwa.
"Nitabaki kuwa mwanachama mtiifu kwa chama na nitaendelea kupambana kwa maslahi ya chama," alisema.
Mwenyekiti mteule wa CHADEMA Mkoa wa Singida, Toto, alisema kazi kubwa iliyoKo mbele yake ni kuhakikisha anakiunganisha chama ili kiwe kimoja na kuendeleza mapambano kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.
"Uchaguzi umekwisha sasa tuvunje makundi libaki kundi moja tu la CHADEMA na nitahakikisha nalinda rasilimali za chama,” alisema.
Awali, Lissu aliwataka wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi kuchagua kiongozi ambaye atakuwa mstari wa mbele katika mapambano kwa ajili ya uchaguzi ujao.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED