TEC yatoa tamko Uchaguzi Serikali za Mitaa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:39 AM Nov 16 2024
Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa.
Picha: Mtandao
Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa.

BARAZA la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) limesisitiza kuwapo na mfumo wa wazi, haki na unaowajibika katika kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa, alisema kuna madhara makubwa ya kukosekana kwa uchaguzi wa haki ikiwamo malalamiko kutoka kwa wananchi na wakati mwingine nchi kuingia katika vurugu.

“Sisi TEC tusingependa nchi yetu itumbukie katika vurugu zinazosababishwa na uchaguzi mbovu. Njia ya uhakika na ya kuaminika ya kuepuka suala hilo ni kupata viongozi kwa kuendesha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa njia ya haki, uhuru, uwazi, utu, demokrasia na upendo,” alisema.

Askofu Pisa alisema wananchi wameshuhudia namna uandikishwaji wa daftari la makazi ulivyofanyika kwa njia zisizo na haki ikiwamo kutokutolewa kwa vitambulisho vya wapiga kura na kuenguliwa kwa wagombea wengi kutoka vyama vya upinzani jambo lilioitia serikali doa.

“Na hata pale kiongozi mwenye dhamana alipoamua kutoa muda zaidi wa kukata rufani bado hakuondoa doa hilo kwa uchaguzi wa mwaka huu,” alisema.

Alisema ili kuhakikisha wananchi wanaitumia vizuri haki yao ya kuanzisha na kuendesha serikali ya mitaa ni lazima kuwe na mfumo wa wazi, wa haki na unaowajibika katika kusimamia mchakato wa uchaguzi wa viongozi kuanzia ngazi za chini.

Aliikumbusha serikali kutambua nafasi yake katika uchaguzi huo ya kuwawezesha wananchi katika mitaa, vitongoji na vijiji ili kuwapata viongozi halali watakaowawakilisha na wale wataoshinda kihalali ndio wanaopaswa kutangazwa.

Askofu Pisa alisema ni muhimu katika ngazi ya serikali ya mitaa kupatikana viongozi waadilifu na waaminifu, kwani ndiko sehemu ambayo raia hupata fursa ya kutathmini utendaji, uwajibikaji na uwazi wa serikali katika kutekeleza majukumu yake kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa.

Alisema kiongozi anapochaguliwa kwa kupitia ulaghai, hata uongozi wake unakuwa sio wa kiadilifu, kwani atawaongoza watu kwa kutumia nguvu katika kipindi chote cha uongozi wake.

“Na viongozi wa namna hiyo wakati mwingine  tusishangae hata baada ya kuchaguliwa wasipofika kwa watu kwa sababu wanaona hawana dhamana ya kuwaongoza watu husika,” alisema.

Rais huyo wa TEC alisema taifa linapaswa kulelewa na kufanya kazi katika ukweli na si kutengeneza jamii yenye ulaghai,  kwani Mungu hadanganyiki wala hadanganyi na angependa sasa watu wake waendelee kuishi katika misingi ya haki na ukweli.

Alisema tunapoelekea katika uchaguzi huo hawana budi kama viongozi wa Kanisa Katoliki na kiroho  kuungana na Watanzania katika upatikanaji wa viongozi kupitia uchaguzi huru na wa haki .

“Kanisa Katolini huthamini na kuenzi namna Watanzania wanavyoshikamana na kutamani kujitawala, rejea Warumi sura ya 13 mstari wa kwanza hadi wa saba,” alisema.

Aliwasihi wananchi wajitokeze kwa wingi katika kupiga kura za kuwachagua viongozi katika ngazi hizo kama walivyotangaziwa na kuiomba serikali kuhakikisha kuwa demokrasia inatawala nchini na kutuma ujumbe kwa dunia.