TIMU ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), inatarajia kukutana na wenyeji Ethiopia katika mechi ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Des Martyrs, Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo).
Mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania na Ethiopia imeamua kucheza mechi zake Kinshasa kwa sababu ya kutokuwa na viwanja venye hadhi ya kutumiwa katika michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Stars inahitaji pointi tatu muhimu leo na pia kuifunga Guinea katika mechi ya mwisho ya Kundi H itakayofanyika Novemba 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco', amesema ameshawaandaa vijana wake kwa ajili ya kusaka ushindi.
"Maandalizi yameshakamilika, nimejaribu kuwaelekeza vijana wangu nini cha kufanya na kupunguza madhaifu yote yaliyoonekana katika michezo iliyotangulia, niseme tuko vizuri na lengo letu ni kupata pointi tatu ambazo zitatusogeza kwenye mlango wa kuingilia kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON)," alisema kocha huyo.
Nahodha wa Stars, Mbwana Samatta, aliliambia gazeti hili yeye na wachezaji wenzake wote wanaelewa umuhimu wa mchezo wa leo, hivyo watajitoa kupambana ili kupata ushindi kwa sababu endapo watashinda katika mchezo huo watajiweka kwenye wakati mzuri zaidi.
"Kila mchezaji anafahamu umuhimu wa mchezo huu na unaofuata, sidhani kama kuna muda wa kukumbushana tena.
Mwalimu ameshamaliza kazi yake, ametupa mbinu na mipango, ni jukumu letu sasa kuonesha uwanjani. DR Congo wameshafuzu, tunagombea nafasi moja, sisi (Tanzania) na Guinea ndiyo tunapewa nafasi kubwa, hivyo tunataka tuitumie nafasi hiyo," alisema Samatta.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Septemba 4, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.
Stars yenye pointi nne ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo nyuma ya Guinea yenye pointi sita huku Ethiopia inaburuza mkia kiwa na pointi moja.
Mechi nyingine ya kundi hilo itachezwa leo kati ya Guinea dhidi ya DR Congo ambayo tayari ina pointi 12 kibindoni.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED