KLABU ya Coastal Union inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kufanya uchaguzi mkuu ifikapo Desemba 16, mwaka huu, imeelezwa.
Uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo baada ya viongozi waliokuwepo kumaliza muda wa kukaa madarakani miaka minne.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo, Linda Lugano, ilisema mchakato wa kuchukua fomu kwa wagombea ulianza jana kwa wadau mbalimbali kusisitizwa kujitokeza kwuania nafasi za uongozi.
"Napenda kuweka wazi mwisho wa kuchukua fomu ni Jumatatu ya Novemba 18, mwaka huu saa 9:00 mchana, fomu zinapatikana katika ofisi ya klabu ya Coastal Union FC," alisema katibu huyo.
Lugano alitaja nafasi zitakazowaniwa katika uchaguzi huo ni pamoja na mwenyekiti, makamu mwenyekiti, wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.
Alisema gaharama ya kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti ni Sh. milioni moja, makamu ni Sh. 500,000 na wanaotaka kugombea ujumbe wa kamati ya utendaji watalipia fomu kwa sh. 200,000.
Wanachama wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wanafanya uchaguzi ili kujiandaa na uchaguzi wa shirikisho hilo utakaofanyika mwakani.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED