Pamba Jiji FC yaitisha Simba ikiwaza rekodi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:23 AM Nov 16 2024
Pamba Jiji FC
Picha:Mtandao
Pamba Jiji FC

HUKU ikiendelea kujiimarisha, Pamba Jiji FC imewataka Simba ya Dar es Salaam kutotarajia mteremko katika mechi itakayowakutanisha ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa Novemba 22, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Mathias Wandiba, amesema Simba anakwenda Mwanza katika wakati mbaya kwa sababu malengo yao ni kushinda mechi nne zilizobaki za mzunguko wa kwanza.

Wandiba alisema Pamba Jiji inawaambia Simba wajiandae kukutana na ushindani kutokana na wao kuhitaji ushindi katika mechi zote zilizobakia za mzunguko wa kwanza ambazo watacheza nyumbani.

"Dhamira yetu ni kufanya vizuri katika michezo yetu minne iliyobaki ya mzunguko wa kwanza, michezo miwili tutacheza nyumbani  dhidi ya Simba, Ijumaa ijayo na KenGold, Desemba Mosi, hii tumejiwekea mikakati ni lazima tushinde, kwa bahati nzuri moja kati ya michezo hii mwili tunacheza na Simba, wamekuja kwenye wakati mbaya.

Unapocheza na timu kama Simba ni lazima wachezaji wawe vizuri kichwani kiakili, huwezi tu kusema tunatumia mfumo huu, sijui nini, ni lazima uwaweke wachezaji wako vizuri kisaikolojia, kwa sababu wanaweza wakaingia wakafanya kitu hicho kikawaondoa kwenye mchezo moja kwa moja," alisema kocha huyo.

Aliongeza anaamini katika mchezo huo Pamba Jiji inaweza kupata ushindi wa kwanza nyumbani kutokana na maandalizi na maboresho ambayo wamefanya ndani ya kikosi chao.

Pamba Jiji imeshinda mechi moja tu msimu huu ambapo ilikuwa ugenini dhidi ya Fountain Gate, ikiwafunga mabao 3-1, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani, Manyara.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Pamba Jiji iko kwenye nafasi ya 15, ikiwa na pointi nane, baada ya michezo 11, ikishinda mmoja, sare tano na kupoteza michezo mitano.