WIKI za hivi karibuni zinafuatana na simulizi zenye mtikiso utokanao na uchaguzi kitaifa, pia matokeo yake.
Kulianza Msumbiji, Frelimo ikaendelea kukalia kiti Msumbiji baada ya mchuano mkali, katika safari kuelekea miaka 50, matokeo yakapokewa na fujo za wapinzani, Renamo waliowahi kuwa wapiganaji porini.
Nchini Botswana, mwenyeji wa Ikulu miaka 58 tangu uhuru akang’oka wiki iliyopita, akiahidi kukabidhi nchi kwa amani na akatekeleza hivyo.
Wakati mada na mshangao huo haujaisha, ukatekwa na mwingine wiki hii, mchuano mkali wa Donald Trump kurudi Ikulu baada ya kukaa ‘benchi’ na mlolongo wa kashfa kipindi kimoja, akimteka fursa mwanamama Kamala Harris, aliyetaka kuweka historia ya kijinsia katika nafasi hiyo nchini Marekani.
Daima, mzizi wa uwekezaji kisiasa kote huko haujawahi kuwa mbali na matakwa ya siasa uchumi.
KILICHOJIRI BOTWSANA
Nchi hiyo ilipata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mnamo Septemba 30, 1966 sasa ina idadi ya watu ni milioni 2,675. Hao katika hesabu ya haraka ni sawa na nusu ya wakazi wa Dar es Salaam.
Ni nchi inayofahamika kwa ustawi na uthabiti kiuchumi muda mrefu, hasa kutokana na utajiri wa almasi, huku ikiwa na idadi ndogo ya watu wanaopewa huduma za bure kama elimu na afya.
Hata hivyo, kushuka kwa bei ya almasi kwenye soko la kimataifa katika miaka ya karibuni, kunatajwa kuchangia kushuka mapato ya ndani, hata nchi hiyo sasa inaangalia sekta mbadala iwekeze.
Muda mfupi kabla ya uchaguzi mwisho wa mwezi uliopita, Rais wa Botswana anayeondoka madarakani, Mokgweetsi Masisi kutoka chama tawala- Botswana Democratic Party, akakiri almasi za nchi ‘zilidoda’ sokoni tangu mwezi Aprili mwaka huu, hata kuathiri uchumi wao.
MASISI AKIWA UN
Mnamo Septemba mwaka 2022, Rais Masisi, akahutubia mjadala Mkuu wa Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA77), akigusia mchango wa almasi katika uchumi wa Botswana.
Hapo akawa na ufafanuzi namna taifa hilo, limevuka kutoka umaskini hadi kuwa nchi ya kipato cha kati.
Masisi akawaambia viongozi wenzake kuwa:
“Hii ni hadhi ambayo tunajivunia nayo, kwa sababu tulipopata uhuru miaka 56 iliyopita (sasa 58), tulikuwa miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani.
“Lakini tulibahatika kubaini kile kilichobainika hivi sasa duniani kuwa (Botswana), ni hifadhi kubwa zaidi ya machimbo ya madini ya almasi kwenye ukanda wa Kimberley.”
Akawasifu viongozi watangulizi walioweka msingi mzuri wa kusimamia almasi yao, hapo nako akiwa na nukuu: “Viongozi wetu waliotangulia walichagua kugeuza simulizi ya kuwa na madini ya almasi kuwa simulizi ya maendeleo.”
Masisi akafafanua kwamba, Botswana isingefika iliko kimaendeleo, pasipo kuangaliwa, kulindwa, kutetewa na misingi ya demokrasia iliyojikita kwenye utawala wa sheria na utawala bora, pia ulinzi wa haki za binadamu kwa watu wake.
Hata hivyo, timu ya wanasiasa wa upinzani wakiongozwa na muungano wao chini ya mkusanyiko uitwao Umbrella for Democratic Change (UDC) au ‘mwamvuli wa mabadiliko ya kidemokrasia’ BDP, wamekuwa wakikikosoa chama tawala kubaki madarakani muda mrefu.
Hiyo wanaitaja inachangia kuvuruga uchumi wao, pia kuwapo ufisadi, madai ambayo Masisi alikanusha, wakati huo akiwa Rais.
Masisi katika uwasilisho wake, akaipongeza ajenda ya mwaka 2021, iliyozinduliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres.
Mkuu huyo wa UN, akasema Botswana inazingatia kwa makini kuhakikisha rasilimali yake adhimu ya almasi inatumiwa kwa maslahi na maendeleo endelevu kwa wananchi wake.
“Nakumbusha chombo hiki adhimu kuwa simulizi ya Botswana ni ushahidi usio na shaka na ulio hai ya kwamba almasi ikisimamiwa vizuri ni kwa maendeleo. Ni kwamba almasi ni suala makini la kujipatia kipato,” akatamka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Rais Masisi, hata hivyo akakiri namna wanavyopata changamoto kwenye kuvutia wawekezaji, kusaidia kupanua wigo wa sekta ya uchumi. Akaahidi kutumia kila jukwaa kusaka wawekezaji kwenye sekta nyinginezo.
DAI LA AJIRA UN
Mokgweetsi Masisi, katika hotuba yake hiyo kwenye mjadala, akasema marekebisho yoyote ya muundo wa Umoja wa Mataifa (UN), yatakuwa na maana kwa mataifa madogo kama Botswana, pale yatakaporuhusu kila nchi kushiriki kwa usawa bila kujali ukubwa wao.
“Mimi na serikali yangu tuna hamu ya kuona wananchi wetu wakiwakilishwa na wakiajiriwa ndani ya mfumo wa UN na kwa urais wetu wa Baraza la Uchumi na Kijamii, ECOSOC.
“Naamini Botswana imeonyesha uwezo wake, ikiwamo vijana wetu ambao wamepatiwa tathmini nzuri kutokana na usaidizi wao kwa Sekretarieti ya ECOSOC wakati wa awamu yetu,” akasema.
DIRA YA MTEULE
Huyo ni mwanasheria, Duma Boko (55), anayetasfsiriwa kisiasa mwenye kujiamini, pia ana maadili mema, huku akiwa na sifa ya kutohofia jambo.
Kitaaluma alipata elimu ya sheria nchini mwake, kisha akainakishi kitaaluma katika Shule ya Sheria ya Havard, Marekani na sasa ni mbobevu katika haki za binadamu.
Katika kijiti alichopokea, anatajwa kuwa na ‘kibarua kigumu’ kuimarisha uchumi wa nchi, pia wananchi wake ‘wanamkodolea macho’ hatima ya maslahi yao.
Elimu yake ya uanasheria ilianzia nchini mwake, hatimaye kwenda Shule Kuu ya Sheria Harvard, huko Marekani.
Hata hivyo, kisiasa ushindi wake, umeushangaza umma na dunia, kutokana na kuvunja dhana ‘wapinzani Botswana hawawezekani…’
Kwa miaka 50 upinzani wa kisiasa nchini humo, wamekuwa wakiota ndoto, kukivua madaraka chama kikuu cha Botswana Democratic Party, lakini ni Boko pekee ndiye aliyefanikisha hilo.
Maoni ya kwanza akatoa Ijumaa iliyopita, kwamba anatamka: “Ninaweza tu kuahidi (kwa watu) nitafanya kila niwezalo. Nitakaposhindwa, nitawatazama wao, waniongoze.”
Rais Boko anabainisha nchi hiyo inakopita ni changamoto za kiuchumi an anahidi kuleta mabadiliko katika ajira na mishahara serikalini.
Mbinu zake kwenye kampeni zilimbeba.
Katika muda wote wa kampeni yake, mikutano ya hadhara, Boko akawaomba wafuasi wake kuja karibu awasikilize malalamiko yao, hali iliyoonekana kuwavutia vijana.
Rais Boko, awali alikataa kuwania nafasi ya ubunge kama alivyoshauriwa, akahamisha ujasiri kuwania urais, ambako kampeni zake zilionyesha mafanikio ya awali, kutokana na kuvutia hadhira na kuwa rafiki yao.
Mzaliwa huyo wa mwaka 1969, katika mji mdogo wa Mahalapye, safari yake iliyoanzia kuongoza baraza la wanafunzi, badaaye akaibuka kuwa mwanasheria maarufu nchini, mwake, kwa mujibu wa mchambuzi wa kisiasa, Lesole Machacha.
Kisiasa, baadaye akawa kiongozi wa Chama cha Kitaifa cha Botswana (BNF) mwaka 2010, kilichotajwa kuwa na "itikadi za kikomunisti" ana kuna wakati akaongoza katika mgogoro na wahadhiri katika chuo kikuu alichofundishja akiwaambia ‘hawafai.’
Baada ya kutangazwa kushindwa wiki iliyopita, Rais Masisi kama alivyofanya Mama Harris Marekani wiki hii, akatamka ameshazungumza na kiongozi wa chama cha upinzani cha mrengo wa kushoto - UDC, Duma Boko, kupanga namna ya kukabidhi madaraka.
Zaidi ya watu milioni moja walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo kati ya raia milioni 2.6 wa taifa hilo.
Ni ni mara ya tatu kwa Boko kuwania nafasi ya urais na baada ya matokeo ya awali kupitia ukurasa wake wa ‘Facebook’ kiongozi huyo wa upinzani akandika "mabadiliko yamewadia."
* Kwa msaada wa mtandao
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED