KUTAKUWA na ongezeko kubwa la makipa wa kigeni msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Inaonekana baadhi ya klabu za Ligi Kuu nchini zimeamua kusaka magolikipa kutoka nje ya nchi kutokana na sababu mbalimbali.
Hili lilianza kuonekana tangu msimu uliopita, ambapo klabu zote kubwa nchini zilikuwa na makipa wa kigeni, na msimu huu tayari wengine wameshatua nchini.
Sababu zilizotajwa ni kwamba soka hivi sasa limebadilika, ambapo umahiri wa makipa si kuruka tu na kuokoa michomo, bali kuwa na uwezo wa kuuchezea miguuni kama mchezaji wa ndani ili kuweza kuanzisha au kuandaa mashambulizi kutoka nyuma.
Makipa wengi wa nje kwa sasa wamekuwa hivyo kutokana na mafunzo wanayoyapata, tofauti na wa hapa ambao wengi hawawezi kuwa na utulivu na mpira miguuni, huku sababu nyingine ikitajwa baadhi yao kutokuwa waadilifu.
Katika makala haya Nipashe linakuletea baadhi ya majina ya makipa wa msimu uliopita na wapya, ambao watasimama langoni msimu ujao kwenye timu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara.
1. Djigui Diarra - Yanga
Anatajwa kuwa ndiye kipa bora zaidi kwa sasa katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Ubora wake si tu umahiri wake wa kudaka na kuokoa hatari kutoka kwa wapinzani, bali uwezo wake miguuni wa kuweza kuuchezea, kupiga chenga na kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma.
Pia ana uwezo mkubwa na 'taimingi', ambapo ni mara chache sana kuona amezubaa na kubaki langoni kusubiri hatima ya anayeukimbilia, badala yake amekuwa na uwezo wa kutoka na kuweza kuuwahi mpira kabla haujafikiwa na mlengwa.
Raia huyu wa Mali, ni mmoja wa makipa wageni aliyesababisha kuletwa makipa wengi kwenye Ligi Kuu msimu uliopita na utakaonza kutokana na kuwa na vitu vingine ambavyo magolipa wa Kitanzania hawana.
Alijiunga na Yanga mwaka 2021, akitokea klabu ya Stade Malien ya nchini Mali.
2. Ayoub Lakred - Simba
Ni mmoja wa makipa waliojipatia sifa kubwa msimu uliomalizika akiwa na Klabu ya Simba. Lakred, raia wa Morocco alisifika kwa uokoaji wake hasa akiwa ana kwa ana na wachezaji wa timu pinzani, akageuka kuwa mhimili mkubwa kwenye timu hiyo.
Ni mmoja wa makipa bora nchini, ambapo pia ana uwezo wa kuanzia mashambulizi kutoka nyuma.
Kutokana na umahiri wake aliouonyesha kwenye Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika, haikushangaza kuona Simba ikimwongeza tena mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kusalia.
Hata hivyo, zipo taarifa kuwa ameumia akiwa kambini nchini Misri, lakini pia ameongezeka uzito, hivyo itamchukua muda kuwa fiti na kurejea langoni, lakini anatarajiwa kuwapo msimu ujao.
3. Ley Matampi - Coastal Union
Matampi ndiye kipa aliyekaa langoni bila kuruhusu bao mara nyingi zaidi kuliko kipa mwingine yeyote kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.
Ni golikipa wa Coastal Union raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambaye amefanya vema msimu mmoja tu tangu atue kwenye kikosi hicho na kukipeleka kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Takwimu zake zinaonyesha kuwa msimu uliopita alicheza mechi 24, sawa na dakika 2160, alipigiwa mashuti 217 langoni mwake, 86 yakilenga lango, aliokoa michomo 75, huku 11 yakitinga wavuni, akiwa na 'clean sheets, 15.
Umahiri wake umesababisha timu nyingi za daraja la Coastal Union nazo kuanza kusaka makipa wageni kuelekea msimu ujao.
4. Allain Ngeleka - Dodoma Jiji
Katika kile kinachoonekana makipa wa kigeni wameanza kuwa dili nchini, Dodoma Jiji imeenda kumng'oa kipa Allain Ngeleka raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutoka Kagera Sugar.
Ni kipa ambaye kwa kiasi kikubwa ameisaidia sana Kagera Sugar kubaki Ligi Kuu kutokana na uwezo wake mkubwa aliouonyesha.
Wala haikushangaza msimu mmoja tu aliosajiliwa na Kagera Sugar kutokea Tabora United na kabla ya hapo alikuwa akikipiga katika klabu ya Lumwana Radiant ya nchini Zambia, huku pia akiwa amewahi kuzichezea Klabu za Nkana Red Devils na Buildcom zote za Zambia, Sanga Balende, Groupe Bazano na Tshinkunku zote na DR Congo, kuchukuliwa na Dodoma Jiji.
5. Mohamed Kamara - Singida Black Stars
Hivi karibuni, Klabu ya Singida Black Stars, ilimtangaza kipa raia wa Sierra Leone, Mohamed Kamara, ambaye ametokea Klabu ya Horoya ya Guinea.
Kipa huyo anatarajiwa kuleta ushindani mkali kwa makipa wa Kitanzania watakaokuwa kwenye kikosi hicho, wakiongozwa na Metcha Mnata.
Kamara anayechezea pia Timu ya Taifa ya Sierra Leone, ni mmoja wa makipa wapya wanaotarajiwa kuonyesha vionjo vipya kwenye Ligi Kuu msimu ujao.
6. Moussa Camara - Simba
Imeelezwa kuwa Klabu ya Simba ipo mbioni kukamilisha usajili wa kipa Moussa Camara baada ya kuonekana Ayoub hatopona na kuwa fiti mapema kwa hivi karibuni.
Kipa huyo raia wa Morocco ambaye aliumia akiwa kwenye maandalizi ya msimu mpya, pia ameonekana kuongezeka uzito kitu ambacho kinawatisha viongozi wa Simba na kuona anaweza kuzikosa mechi nyingi za mwanzo wa msimu, hivyo kufanya mazungumzo na kipa huyo anayechezea Timu ya Taifa ya Guinea na alikuwapo kwenye AFCON ya 2023 iliyopita nchini Ivory Coast, lakini akikipiga kwenye Klabu ya Horoya.
Chanzo kinasema huenda jina la Ayoub likatolewa kwenye orodha ya wachezaji wa Ligi Kuu na kubaki kimataifa ambako hakuna kanuni ya idadi ya wachezaji wa kigeni hadi kipindi cha dirisha dogo litakapoamua vinginevyo.
7. Fabien Mutombora - KMC
KMC nayo haiko nyuma kuelekea msimu ujao, tayari imeshusha kipa raia ya Burundi, Fabien Mutombora, aliyekuwa akiichezea Klabu ya Vital'O ya Burundi.
Atakuwa mmoja wa makipa wa kigeni ambao wameanza kumiminika kwa kasi nchini kuwapa changamoto makipa wazawa ambao wengi wao wamekuwa hawana mwendelezo katika mechi wanazocheza, baadhi wakicheza vema, lakini zingine wakifungwa mabao mepesi, huku wakifanya makosa mengi.
8. Mohamed Mustafa - Azam FC
Baada ya kuhangaika kupata kipa bora kwa muda mrefu, kipindi cha dirisha dogo msimu uliopita, Azam ilimleta golikipa Mohamed Mustafa kutoka El Merrikh ya Sudan.
Ilimuona wakati Yanga ikicheza dhidi ya timu hiyo kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo ikamchukua kwa mkopo.
Kwa nusu msimu tu aliocheza alionyesha uwezo mkubwa na kupigiwa saluti na mashabiki wengi wa soka nchini kiasi cha Azam kuamua kumsajili moja kwa moja kwa misimu miwili.
Anatarajiwa kuwa mmoja wa makipa wa kigeni watakaotikisa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED