Kilimo cha mazoea kinavyomnyima maendeleo mkulima wa pamba

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:29 PM Nov 06 2024
Balozi wa pamba akifundisha wakulima jinsi ya kupulizia viuadudu  kudhibiti wadudu katika  pamba.
Picha: Marco Maduhu
Balozi wa pamba akifundisha wakulima jinsi ya kupulizia viuadudu kudhibiti wadudu katika pamba.

PAMBA ni miongoni mwa mazao yaliyoingizwa nchini na mkoloni lakini likifanikiwa kuendelezwa kwa namna tofauti na wakulima wa zao hilo katika mikoa mahususi yac linakopatikana ili kujikwamua kiuchumi.

Licha ya lengo hilo mahimu la kujikwamua kiuchumi na kuinua pato la Taifa lililoambatana na kuanzishwa kwa viwanda vya kuchambua zao hilo mwanzoni mwa mwaka 1930 bado limeonekana kutokuwafikisha wakulima katika malengo hitajika.

Ukiachana na zao hilo mwishoni mwa karne ya 19 kulimwa katika kanda ya Mashariki ambayo ni Morogoro, Pwani na Tanga uwanda uliongezeka na kuanza kulima katika mikoa 17, ambayo ni Mwanza,Geita,Simiyu, Mara, Shinyanga, Tabora, Singida, Katavi, Kagera, Kigoma, Dodoma, Manyara, Morogoro, Tanga, Iringa, Kilimanjaro na Pwani.

Licha ya asilimia 40 ya watanzania hunufaika na pamba katika mnyororo wa thamani kuanzia uzalishaji,ununuzi, uchambuaji, usafirishaji, mauzo nje ya nchi na uzalishaji wa nguo hapa nchini kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), bado wakulima wanalia kutokunufaika na zao hilo.

TCB inachambua kuwa Pamba inayolimwa Tanzania inategemea zaidi soko la nje kwa asilimia 60, na asilimia 40 kwa viwanda vya ndani. Sehemu kubwa ya malalamiko ya wakulima ni juu ya bei ya kununua zao hilo, kuwa ipo chini na kusababisha kushinda kuiunuka kiuchumi.

Malalamiko hayo yanamfanya mwandishi wa makala hii kufanya ufuatiliaji na kubaini kuwa sit u bei ya zao hilo iliyoposokoni inayofanya wakulima wasiendelee bali kilimo cha mazoea.

Inabainika kuwa bei ya pamba inapangwa katika soko la dunia na kisha Tanzania nayo inakuja na bei elelekezi kwa mkulima huku akiteswa na kilimo cha mazoea kinachomfanya kupata mazao ‘kiduchu’.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya pamba Tanzania Marco Mtunga, anaiambia Nipashe kuwa wakulima wengi wa pamba, bado wanalima kimazoea kwa kumwaga mbegu shambani (kusia) badala ya kupanda kwa mstari na kufuata kanuni za kilimo bora.

Anawasihi wakulima wa pamba, kwamba wakifuata ushauri wa watalaamu lazima wapate mavuno mengi na kuinuka kiuchumi.

Aidha anawatahadharisha kuwa  wanapokuwa wakivuna pamba yao waepuke pia kuweka maji au mchanga kwenye pamba ili kutoichafua hali ambayo imekuwa ikisababisha kuonekana pamba ya Tanzania haina thamani na hata bei kushuka.

Katika msimu wa ununuzi wa pamba 2023/2024, bei elekezi ambayo ilitangazwa na serikali ni Sh.1,150 kwa kilo moja, ambayo Wakulima wameilalamikia kwamba haitawatoa kwenye umaskini.

Mmoja wa wakulima, James Ally Mkazi wa Shangihilu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, anasema amezoea kila msimu analima lakini hapati faida huku akiahidi kuacha kilimo hicho kwani haoni kikimtoa katika umasikini.

Anasema licha ya kupata mavuno kidogo, bei ya kununua pamba ikiwa vizuri watapa faida ikilinganishwa na gharama ambazo wanazitumia kwenye kilimo hicho, tangu kuanza maandalizi ya shamba hadi kuvuna.

“Ukilima hekari moja unapata kilo 200, ukiuza kwa bei elekezi ya serikali sh.1,150 kwa kilo hizo 200 unapata sh.230,000, lakini mimi tangua maandalizi ya shamba hadi kuvuna nimetumia sh. 260,000 na hapo kuna gharama zingine tumeziacha, hivyo nitakuwa na hasara ya sh.30,000,”anasema James.

Mkulima  Mwingine Nicodemas Masesa, anasema wakulima wengi wameachana na kilimo hicho kwani wanaona hakiwatoi kwenye umaskini, na kwamba hata yeye yupo mbioni kuachana nacho na kukimbilia kwenye mpunga, kutokana na kuona wenzao waliolima zao hilo wameinuka kiuchumi.

“Ipo haja ya serikali kufufua viwanda vilivyokufa vya kutengeneza nguo zitokanazo za zao la Pamba hapa nchini ili bei ya Pamba iwe nzuri,, kuliko kuipeleka nje ya nchi na kufanya bei kuwa chini,”anasema Masesa.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, anawaambia Wakulima kwamba bei ya pamba siyo tatizo kubwa la kushindwa wao kuinuka kiuchumi, shida ni wao kulima kimazoea na kuacha kilimo chenye tija  ambacho unalima shamba dogo mavuno mengi.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba akifundisha wakulima wa pamba Kanuni 10 za kilimo bora cha pamba.

Anasema Mkulima akilima kimazoea hekari moja lazima apate kilo 200 hadi 300, lakini akilimia kisasa kwa kufuata ushauri wa maofisa ugani, hekari moja anaweza kupata kilo 1,800 hadi 2,000 na atapata faida.

“Mfano hekari moja ya pamba umelima kisasa na kugharamia Sh.260,000 na ukapata mavuno kilo 1,800 na ukauza kwa bei elekezi ya sh.1,150 kwa kilo utapata Sh.milioni 4.1 tayari utakuwa na faida ya sh.milioni 3.7 hapo lazima uinuke kuchumi,”anasema Macha.

Anasema msimu wa pamba 2023/2024 mkoa huo hakufanya vizuri kwenye mavuno, kutokana na wakulima kulima kimazoea na kupata mavuno kidogo, ambapo walipanga kuvuna kilo milioni 30 lakini wamekomea milioni 20.

Anataja mikakati ya serikali, kwamba katika msimu ujao wa kilimo 2024/2025, watasimamia suala la kilimo cha pamba kwa wakulima kulima kilimo chenye tija na siyo kwa mazoea tena.

Anasisitiza kwamba Rais Samia Suluhu Hassan hana mchezo na kilimo bali yupo ‘Serious”, na ndiyo maana amewapatia vitendea kazi maofisa ugani, zikiwapo pikipiki, vifaa vya kupimia ubora wa udongo, vishikwambi kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za wakulima, na sasa ameanza ujenzi wa nyumba za maofisa ugani ngazi ya vijiji ili waishi huko huko kwa wakulima.

Mbunge wa jimbo la Kishapu Boniphace Butondo, anasema umefika wakati sasa wa viongozi kulinusuru zao la pamba, kwa kutoa elimu kwa wakulima kufuata kanuni bora za kilimo hicho, kupitia kwenye mikutano na vikao mbalimbali sababu kilimo cha mazoea kilimepitwa na wakati.

Anasema lengo la Serikali kuhamasisha kilimo chenye tija na kutaka kumuona mkulima anainuka kiuchumi, sababu kilimo cha pamba kina tumia gharama kubwa tangu maandalizi yake, hivyo mkulima akilima hekari nyingi bila kufuata kanuni bora kilimo  atapata hasara kwa kuambulia mavuno kidogo.

“Lima hekari chache kitalaamu pata mavuno mengi, siyo kulima hekari nyingi kimazoea na kuambulia mavuno kidogo,”anasema Butondo.

Balozi wa pamba nchini Agrey Mwanri, anasisitiza suala la kilimo chenye tija kwa wakulima wa pamba na kwamba wamekuwa wakizunguka nchi nzima kutoa elimu ya kilimo chenye tija, pamoja na matumizi sahihi ya pembe jeo na ubora wa pamba.

Mkuu wa idara ya kilimo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Sabinus Chaula, wilaya ambayo mkoani hapa ndiyo ina wakulima wakubwa wa pamba, anaahidi kuwa wamejipanga vyema kutoa elimu ya kilimo cha kisasa kwa wakulima katika msimu ujao, na watawafikia kila eneo sababu maafisa ugani wameshapewa usafiri wa pikipiki.