Matumizi ya viuatilifu kiholela kwenye mazao ya chakula yanaweza kuathiri afya ya binadamu, kuleta changamoto za kimazingira, na kusababisha vifo vya baadhi ya viumbe hai.
Hayo yamesemwa leo, Novemba 6, na mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Joseph Birago, kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali wakati wa kongamano la kujadili viuatilifu vya kuulia wadudu na afya nchini na Afrika Mashariki lililofanyika MUHAS.
Birago amesema viuatilifu vina maelekezo maalum ya matumizi salama, na matumizi yasiyo sahihi yanaweza kuwa na athari kubwa kwa jamii. Alisisitiza kuwa mkutano huu utaangazia mbinu bora za kufikia jamii ili kuhakikisha matumizi salama ya viuatilifu na kujenga Tanzania yenye afya.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Appolinary Kamuhabwa, ameeleza kuwa kongamano hilo linategemewa kutoa majibu kupitia tafiti za kitaalamu kuhusu matumizi ya viuatilifu na athari zake. Kongamano pia litatathmini sera zinazofaa na elimu itakayosaidia wakulima na wafugaji kutumia viuatilifu kwa usahihi.
"Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, wadudu na magonjwa yanabadilika, na baadhi ya magonjwa yanahusishwa na matumizi mabaya ya viuatilifu," alisema Profesa Kamuhabwa. "Tunahitaji mwongozo mzuri ili kuepusha madhara yanayosababishwa na matumizi yasiyo sahihi."
Mtafiti wa magonjwa ya mimea, Vera Ngowi, ameongeza kuwa kongamano hilo litajadili madhara ya viuatilifu kwa afya ya binadamu, ikiwemo magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, na saratani, ambayo yanahusishwa na kemikali zinazopatikana kwenye viuatilifu.
"Hivi sasa, udhibiti wa viuatilifu umekuwa hafifu na sheria zimebadilika, hivyo tunaendelea kujadili namna bora ya kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti athari hizi," amesema Ngowi.
Kongamano hilo linatarajiwa kutoa mapendekezo ya sera na mikakati ambayo Wizara ya Afya inaweza kutumia kwa ajili ya ulinzi wa afya ya jamii na mazingira.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED