Jafo na mchakamchaka wa maagizo 2 ya Rais kazini Viwanda, Biashara

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:08 AM Sep 20 2024
Siku Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alipotembelea Soko la Kariakoo, Dar es Salaam.
PICHA: MTANDAO.
Siku Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alipotembelea Soko la Kariakoo, Dar es Salaam.

ILIKUWA mwezi Julai mwaka huu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alipomuapisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo na wenzake, akimuagiza “asiwe mtu wa kukaa ofisini pekee, bali kufika kwa wananchi kukagua kinachoendelea.”

“Nianze na Jafo, ulikuwa Ofisi ya Makamu wa Rais umefanya vizuri! Lakini, nimeona nikutoe nikupeleke biashara kwa sababu biashara pilika ni nyingi mno na kuanzia sasa pale ofisini mwenzio alipokuwa anakaa sitaki ukae.

“Namuelewa Waziri kwanini alikuwa haendi huko kwa kazi ninayotaka kukupa, kwa mtoto wa kike sio rahisi, kushinda Kariakoo juu chini, chini juu sio rahisi, hiyo kazi nataka uifanye wewe.” 

Akaendelea: “Kariakoo ni eneo zuri sana la biashara na eneo muhimu sana la biashara na ndio linalofanya Dar es salaam iitwe ‘kitovu cha biashara’, kwa sababu mataifa yote yanakuja Kariakoo. 

“Lakini, Kariakoo tumeweka pesa nyingi sana kujenga yale masoko ya Kariakoo na masoko yakimalizika nataka biashara zifanyike saa 24 kwa hiyo, mtakaa vipi na Jeshi la Polisi mtajipanga vipi, hiyo ni kazi yako.

“Nataka Kariakoo pawe na Soko la Biashara la Kimataifa na kwa sababu mwaka huu ‘mwisho mwisho’ tunamaliza yale majengo, Wamachinga na wengine walioko pale wataingizwa ndani ya soko.”

Hadi sasa, baadhi ya wafanyabiashara wa kigeni Waafrika wanaopatikana Kariakoo kufuata bidhaa ni kutoka nchi kama Malawi, Zimbabwe na Zambia, huku kukiwapo uwekezaji biashara kimataifa kutoka wageni wa nchi kama China.

Pia, Rais Dk. Samia akaisisitiza hoja yake aliyotoa siku chache kabla ya tukio hilo, akitamka: “Pia ukarejee Ilani yetu ya Uchaguzi  inayozungumzia Sekta ya Biashara na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukua.

“Ukarejee kauli yangu kwenye ufunguzi wa maonyesho ya Sabasaba nimesema, serikali itafanya kila linalowezekana kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini na ndio maana nakuambia uwe juu chini Kariakoo”

Baada ya uteuzi, uliobeba magizio makuu mawili, uihuishaji wa biashara Karikaoo na kufanya biasahra ya ushindani kitaifa, siku iliyofuata Julai 6, Waziri Jafo akaanza kazi ya ukaguzi na kushughulilikia agizo la Rais, hatua yake ya kwanza ni sokoni Kariakoo.

Hapo azma kubwa ilikuwa kupata undani wa shida zao na akakutana na viongozi wa wafanyabiashara waliomjibu kuona dalili za afueni.

AKIWAJIBIKIA MAELEKEZO

Ndio imekuwa staili ya kazi, akizuru na kukagua maeneio ya kazi, huku akisafiri na ajenda mbili za rais.

Waziri Dk. Jafo akiwa bungeni mwezi uliopita, akabainisha hatua za serikali katika kusimamia ushindani wa haki na kuwalinda watumiaji bidhaa na huduma nchini, kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani ya Mwaka 2003, inayotarajiwa kufanyiwa marekebisho karibuni ya tija  kumlinda mlaji. 

Jafo akasema dhana ya ushindani na kumlinda mlaji zina uhusiano mkubwa na sababu kuwapo ushindani wenye afya katika soko.

Hivi sasa, Waziri Dk. Jafo yuko mkoani Mtwara na jana alikuwa wilayani Liwale.  Alipotembelea mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa, ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa hatua za serikali za kuimarisha miundombinu ya sekta ya uvuvi  nchini.
 
“Huu ni uwekezaji wa kwanza mkubwa katika bandari hii kubwa nzuri ya uvuvi, ambayo itabadilisha kabisa uchumi wa taifa letu hili katika sekta ya uvuvi. 

“Ndani ya muda mfupi tukumbuke Mheshimiwa Rais ametoa (shilingi) bilioni 266 kwa ajili ya mradi huu na tunaona utekelezaji wake unakwenda vizuri." anasema Waziri Jafo, akipataja patafungua fursa za biashara nchini na kuongeza thamani ya mazao bahari.
 
Mkuu wa Mkoa wa Lindi,  Zainab Telack akaishukuru serikali kuiwezesha Halmashauri ya Kilwa kuwa kitovu cha bandari ya kwanza ya uvuvi ya kisasa na kueleza kuwa fursa hiyo itwapatia wavuvi soko la uhakika la Samaki la Pamoja, kuwawezesha wajasiriamali na wawekezaji kupata eneo maalumu la kupata malighafi. 

RAIS & BIASHARA KIMATAIFA

Siku moja baada ya kutangaza mabadiliko ya nafasi katika wizara inayochukuliwa na Waziri Jafo, kwenye ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa, Rais Dk. Samia akatamka:

 “Dk. Ashatu Kijaji ambaye nilimbadilisha kazi jana tu kabla ya leo, lakini natambua kazi kubwa aliyoifanya katika kutayarisha maonesho haya na kazi kubwa aliyoifanya katika kujenga Wizara ya Viwanda na Biashara...” 

 “Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini. Kwa mfanyabiashara yeyote mwenye maoni ya kuboresha, kujenga na kuisadia nchi, milango ipo wazi.

“Waendelee kuwasiliana na mamlaka zetu mbalimbali ikiwamo wizara yenye dhamana ya biashara, bila kusahau taasisi yake ya TanTrade,” akasema.

Maonyesho ya Sabasaba mwaka huu yamekutanisha kampuni 3,486, Rais akitaja ni ishara ya kukua na mvuto mkubwa wa biashara kimataifa, unaochangiwa na usimamizi thabiti wa serikali, ikiwamo sekta za Biashara, Viwanda na Uwekezaji.

 “Ni ukweli usiopingika kuwa njia mojawapo ya kufikia azma hii ni uendelezaji na uimarishaji wa ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa, hivyo kufungua fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji. Matunda ya kuimarika kwa ushirikiano tumeshaanza kuyaona. 

“Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwa maana ya TIC kimesajili miradi 504 mwaka jana, yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.68. 

“Hii ni kwa sababu watu wanakuja Tanzania, wanaona fursa, wanashiriki maonyesho, wanatembelea mabanda mengine na kuona fursa zilizopo Tanzania na kuvutika kuja kuwekeza,” anasema. 

Rais akataja tamwimu, kwamba mauzo ya nje ya bidhaa yalipanda kutoka shilingi trilioni 12.3 mwaka 2019 hadi kufikia shilingi trilioni 17.38 sawa na Dola za Marekani Bilioni 6.57 mwaka jana.

“Niwahakikishie kuwa tunaendelea kujenga, kuboresha na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya miundombinuili kuhakikisha tunaongeza tija kwa uzalishaji, kwa wingi na sifa ‘quality’ (ubora) na ‘standards’ (viwango).

“Vilevile, tuhakikishe kwamba tunakamilisha miradi ya miundombinu ili bidhaa zinazozalishwa ziweze kinasafirishwa kirahisi kufika kwenye masoko yanayokusudiwa. 

“Vilevile, kazi hii tunayoifanya itaendelea kuwawezesha majirani zetu kunufaika kwa kutumia miundombinu hii katika kuchochea maendeleo ya ukuaji wa nchi zao. Ni kwa namna hii tutaendelea kuifanya Tanzania kuwa mahali sahihi pa Biashara na Uwekezaji,” akatamka Rais.

RAIS NA BIASHARA

Akiwa mwaka mmoja tu madarakani, Rais Dk. Samia, moja ya ajenda zake ‘alizozifungia kibwebwe’ ni kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia sera, sheria na taratibu.

Hadi kufika mwaka 2022, Rais akatangaza salamu za tabasamu, kuongezeka pato la taifa kutoka shilingi trilioni 39.9 za mwaka 2021 hadi shilingi trilioni 45.2 mwaka 2022.

Ilikuwa katika hotuba yake akifungua Mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Ikulu, Dar es Salaam, akiitaja baraza hilo litaendelea kuwa moja ya vyombo rasmi vya kuishauri serikali kuhusu hatua za kuimarisha biashara, lengo ni kujenga uchumi shirikishi nchini.

Rais akaihimiza TNBC kufanya mashauriano yatakayoimarisha uwezo wa sekta binafsi nchini, kuzalisha bidhaa za huduma zitakazopunguza uagizaji na kuongeza mauzo katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Vilevile, akaitaja kuwa ni hatua wezeshi nchini kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kuongeza mapato, hata kuimarisha uchumi wa nchi.

Rais Samia akasema serikali inaendeela kuweka mkazo katika kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwamo miundombinu, nishati na Tekinaljia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), inayowezesha kukua biashara.