Hii miti inavyokatwa ovyo, tutalia na kusaga meno huko tunakong’ang’ania

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:28 AM Sep 20 2024
news
Mchoraji:Msamba
Katuni

KWA miaka ya hivi karibuni kumekuwa na tabia ya ukataji miti ovyo kwenye mikoa mingi ya Tanzania.

Ukataji miti huo uliokithiri umekuwa ukileta matatizo mbalimbali yakiwemo mabadiliko ya tabia nchi.

 Ndiyo maana unaweza kukuta mabadiliko ya mvua, zamani ilikuwa ikinyesha miaka fulani, lakini sasa hainyeshi. Mvua zinakuwa hazina tena kanuni, zinanyesha muda wowote, vyanzo vya maji vinakauka, wakati mwingine hata mito inabadililisha njia zake. 

Unaweza kuona unabadilisha sura yake ya zamani, badala ya kupita kushoto inapita kulia. Kikubwa zaidi ni ukame. Ukataji ovyo wa miti unasababisha ukame, mara nyingi ukame husababisha wananchi washindwe kulima hali inayosababisha njaa. 

Waswahili wana msemo wao ‘maji ni uhai’. Wako sahihi kwa sababu unapokwenda popote pale, ili ujue kuwa sehemu hiyo ina uhai, yaani watu waishi eneo hilo, ni lazima ukutane na miti au mimea iliyo na rangi ya kijani kibichi na pili ni maji.

 Kwa asilimia kubwa hapo maji na mvua ndiyo inasababisha mimea na miti iwe ya kijani. Maana yake ni kwamba mvua inanyesha eneo hilo. Na haiwezi kunyesha kama watu wanakata miti. 

Mvua hupendelea kunyesha sehemu yenye miti mingi au misitu. Hapo sasa unaweza kuona umuhimu wa kutunza miti, ambayo ndiyo inalinda vyanzo vya maji.

 Zamani miaka ya nyuma, babu zetu walikuwa na uwezo mkubwa wa kulinda vyanzo vya maji kwa kutumia plani mbalimbali, ikiwamo kuweka mila na utamaduni.

 Walikuwa wakiwaambia watoto wa vijana kuwa miti ile mikubwa ni sehemu ya matambiko ambayo hatakiwi mtu yoyote kupata miti kwani akifanya hivyo atapotea msituni. 

Wakati mwingine wanaambiwa pori lina mizimu, au joka kubwa ambalo mtu akienda kwa sababu za uovu ikiwa pamoja na kukata miti, atakufa akiwa ndani ya msimu. Ili kukata miti, wazee wenyewe waliitana na kufanya kitu kama tambiko ili kwenda kukata miti na walifanya hivi makusudi ili vizazi vijavyo viendelee na utamaduni huu.

 Walijua kama wakiacha tu bila kuweka marufuku hiyo basi vijiji na maeneo yao yatabaki jangwa kutokana na mahitaji ya miti. 

Akiwa Makete mkoani Njombe, Dk. Pindi Chana, Waziri wa Maliasili na Utalii, aliwaonya wananchi wa Wilaya hiyo kuacha tabia ya kukata miti ovyo.
 "Tusikate moto ovyo, tukikata tutakuwa jangwa, tukiwa jangwa tukakosa mvua, na tukikosa mvua tutakosa chakula," alisema Dk. Chana katika mkutano uliofanyika Kata ya Isapilano.
 
 Alichosema Balozi Chana inabidi kizingatiwe siyo na watu wa Makete, au Njombe tu, bali Tanzania nzima. Tumekuwa na kizazi ambacho kwa sasa hakina woga tena, huwezi kuwaambia kwenye msitu kuna joka, au mizimu wanakusikia.  
 Badala yake sasa kuna kizazi cha watu wanaohitaji elimu ili wafahamu madhara ya kukata miti au faida ya kutunza miti.Kinachotakiwa sasa ni serikali kuanzia kuu mpaka ya vijiji kuelekeza elimu kwa wananchi ili kuwaeleza umuhimu huo. 

Tukiwaambia mvua inayonyesha pamoja na kwamba inaletwa na Mungu, lakini inanyesha eneo ambalo misitu na miti yake imetunzwa vizuri. Miti ambayo pia inaleta vyanzo vingi vya maji, na ikijumisha hayo yote nchi inakuwa na neema ya mazao ya chakula na biashara.