Huyu ndiye aliyeigiza kama mlevi, wimbo 'Whisky Soda'

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:26 AM Feb 01 2025
Huyu ndiye aliyeigiza kama  mlevi, wimbo 'Whisky Soda'.
Picha:Maktaba
Huyu ndiye aliyeigiza kama mlevi, wimbo 'Whisky Soda'.

MWANZONI mwa miaka ya 1970, kulikuwa na wimbo mmoja uliokuwa unasikika kwenye redio ulioshangaza watoto wengi wa wakati huo.

Natumai wakubwa hawakushangaa, lakini watoto wengi walionyesha kushangaa, kufurahi na kucheka kwa wakati mmoja kwani haikufanana na nyimbo ambazo wamewahi kuzisikia kabla.

Kusikia wimbo kwenye redio ambao unaimbwa na mlevi ni kitu ambacho kilionekana cha ajabu sana.

Watoto wengi walishangaa kuona mlevi anapewa nafasi ya kuimba, wakati anaimba 'kipombepombe.'

Pamoja na hayo, staili hiyo ya uimbaji iliwakosha watoto wengi na kufanya kuupenda wimbo huo.

Siyo kama walipenda maneno yake, bali aina tu ya uimbaji wa mlevi hiyo, ambaye kuna wakati kama anaimba, kuna wakati kama anafokea mtu, baadaye kama anataka kutapika, mara anamfukuza mtu au mnyama, yaani vituko baada ya vituko.

Watoto waliupenda sana na wala hawakuwa na haja ya kuuliza ulipigwa na bendi gani, ya wapi na hata mtunzi ni nani.

Watu wazima nao walitokea kuupenda sana kwa sababu ulikuwa wimbo ambao uliongeza ladha na ubunifu wa muziki, kwani ulitengenezwa tofauti na nyimbo zingine, huku katikati ya wimbo ukiimbwa na 'mlevi' huyo.

Inawezekana hadi leo hii kuna baadhi ya watu ambao wanaufahamu wimbi huo, lakini hawajajua ni bendi gani au ni mwanamuziki gani alitunga wimbo huo.

Kwanza kabisa, wimbi huo jina lake ni 'Whisky Soda.' Ulitungwa na kuimbwa na mwanamuziki raia wa Guinea, Aboubacar Demba Camara.

"Mano mambo, eeeh mano eee, mano whisky soda, mano mambo..." Ni baadhi ya maneno yaliyomo kwenye wimbo huo.

Hata hivyo zipo taarifa kuwa mtunzi halisi wa wimbo huo ni Baba Soumano, raia wa nchi hiyo, ambaye aliurekodi mwaka 1950.

Hata hivyo umaarufu wa wimbo huo, ulipatikana mwanzoni mwa mwaka 1970, Demba Camara, alipourudia akiwa na bendi ya  Bembeya Jazz National. Na yeye ndiye 'aliyeekti' kama mlevi, akiwavunja watu mbavu. Inasemekana hakuwa anakunywa pombe kabisa.

Nadhani wengi watataka kumfahamu kiongozi huyo wa bendi hiyo, ambaye mbali na wimbo huo, alijipatia umaarufu mkubwa miaka hiyo kwa nyimbo zake kama 'Mamiwata', 'Beni Barale', 'Ballake', 'Moussogbe', 'Tama Tama' na zingine nyingi.

Alizaliwa mwaka 1944 huko Conakry, Guinea ya Kifaransa katika familia kutoka Saraya. Alisoma katika shule ya msingi ya Coléa hadi mwaka 1952, alipohamia shule nyingine huko Kankan. Mnamo 1957, alirejea Conakry kumaliza masomo yake ya msingi kabla ya kurudi Kankan, ambako alijiunga na shule ya ufundi na kupata cheti chake cha useremala. Mwaka 1963, alihamia mji wa Beyla kusini mwa Guinea kwa ajili ya kazi.

Demba Camara alijiunga na bendi ya Bembeya Jazz National mwaka 1963. Alikuwa kiongozi wake, mwimbaji mkuu, na mtunzi wa nyimbo. Katika kilele cha umaarufu wake, Demba Camara alitangazwa kuwa mwimbaji bora wa Afrika na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

 Machi 1973, Bembeya Jazz National ilialikwa nchini Senegal na serikali ya Guinea kwa ajili ya ziara ya maonyesho. Bendi hiyo ilipokelewa kwa shangwe katika Uwanja wa Ndege wa Dakar-Yoff, Machi 31, ambapo waliondoka kwa msafara kuelekea mjini Dakar. Katika makutano ya barabara mbele ya Deux Mamelles, gari aina ya Peugeot 504 lililombeba Demba Camara, mpiga gitaa wake Sekou Diabate, na mwimbaji Salifou Kaba lilipata ajali. Demba Camara alinaswa chini ya mlango wa gari na akapelekwa hospitalini ya Dentec nchini humo pamoja na wenzake. Madaktari waligundua kuwa alikuwa na ufa kwenye fuvu la kichwa, kifua, na majeraha kadhaa. Licha ya juhudi za madaktari, alifariki dunia, Aprili 5, 1973, kutokana na kutokwa na damu nyingi.

Baada ya kutangazwa kwa kifo cha Demba Camara, ujumbe wa serikali ya Guinea na kamati kuu ya Parti Democratique de Guinee, ukiongozwa na Waziri wa Elimu Mamadi Keita, ulisafiri kwenda Dakar kuchukua mwili wake. Ndege yao ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Dakar-Yoff, ambako ilipokelewa na umati mkubwa wa waombolezaji na ujumbe wa serikali ya Senegal ukiongozwa na Rais wa Bunge Amadou Cisse Dia. Alisema kuwa serikali ya Senegal haikuacha juhudi zozote katika kujaribu kumuokoa Demba Camara, lakini ilishindikana.

Waguinea walitua Conakry na mwili wa Demba Camara ukapelekwa Palais du Peuple kwa lori, ambako ulipokelewa na maelfu ya waombolezaji. Rais wa wakati huo, Ahmed Sekou Toure, mke wake walipiga magoti mbele ya jeneza lake. Demba Camara alifanyiwa mazishi ya kitaifa, yaliyowakilishwa  na wanachama wa serikali za Guinea na Senegal. Watu laki moja waliovaa mavazi meupe walifuata mwili wake kwa maandamano kuelekea makaburi ya Camayenne, yakiongozwa na bendi ya jeshi la Camp Boiro iliyokuwa ikipiga wimbo wa Boloba, wa Manding unaochezwa kwa heshima ya mashujaa wa nchi tu.

 Tuma meseji 0716 350534