Hivi ndivyo watu wasiojulikana walivyotikisa nchi mwaka 2024

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:33 PM Jan 02 2025
Abdul Nondo
Picha: Mtandao
Abdul Nondo

MWAKA 2024 umefika tamati jana saa 5:59 usiku. Leo ni siku mpya na mwanzo wa mwaka 2025. Heri na hongereni wasomaji wa Nipashe na wapenzi wa Kijarida cha Siasa.

Kama ilivyo miaka mingine iliyopita, 2024  ulijaa milima, mabonde, tambarare. Yaani kila aina ya matukio yakiwamo ya kufurahisha na pia kusikitisha ambayo huenda yamelitia taifa doa .
 
 Katika mwaka huo wa 2024, kuliibuka matukio ya kuteka watu wakiwamo wafuasi wa vyama vya siasa katika mazingira ya kutatanisha na kuzua hofu na taharuki miongoni mwa Watanzania.
 
 Utekaji watu huo uliwaibua wanasiasa, wanaharakati na wadau wa haki za binadamu na kupaza sauti wakitaka waliotekwa au kukamatwa na watu wasiojulikana wawaachie huru waseme walipowaficha.
 
 Hata hivyo, juhudi hizo hazikuzaa matunda kutokana na kile ambacho kimekuwa kikielezwa na baadhi ya wanasiasa kuwa wafuasi wao wametekwa na hadi sasa hawajulikani walipo.
 
 Wapo ambao walidai kutekwa lakini baadaye wakapatikana wakiwa hai ingawa inaelezwa kuwa walikuwa wameumizwa katika sehemu mbalimbali ya miili yao.
 
 Mtindo wa kuteka ulishuhudiwa na baadhi ya wakazi wa Kiluvya Dar es Salaam wakati mtu mmoja akitaka kutekwa, lakini bahati nzuri akawazidi nguvu watekaji wakashindwa kumuingza katika gari.
 
 Tukio hilo lilitokea Novemba mwaka huo wa 2024, lakini kutokana na ukubwa wa mwili na uzito wa mtekwaji vilisababisha watekaji kushindwa kumwingiza katika gari waliokuwa wakiitumia.
 
 Video ilirushwa katika mitandao akisikika akiomba msaada kwamba anakwenda kuuawa, akitaka wamsaidie, lakini watu waliokuwapo eneo la tukio walikuwa wakitazama bila kutoa msaada.
 
 "Nisaidieni naenda kuuawa, naenda kuuawa, siwajui hawa, naenda kuuawa" alipambanania uhai hadi akafanikiwa kuwashinda  huku wakimwachia pingu ambazo walikuwa tayari wamemfunga.
 
 Kwa mwaka huo wapo waliodai kutekwa na kubahatika kupatikana akiwamo Abdul  Dondo ambaye ni kiongozi wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT Wazalendo.

Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake CHADEMA Taifa, Aisha Machano, alidai kutekwa, kuumizwa na kutupwa porini
Juni 23 mwaka huu, Edgar Mwakabela 'Stiva' alitekwa jijini Dar es Salaam, lakini baadaye akapatikana akiwa ametupwa katika msitu  mkoani Katavi akiwa na majeraha.
 
Wengine wanaodaiwa kutekwa na watu wasiojulikana na hadi sasa hawajapatikana ni mwenyekiti wa CHADEMA wilaya Temeke, Deusdedith Soka na kabu wake Jacob Mlay.
 
Septemba 6 mwaka huu, mwanachama wa CHADEMA, Ally Mohamed Kibao alitekwa na watu wasiojulikana eneo la Tegeta Dar es Salaam, kisha siku iliofuata mwili wake ukaokotwa akiwa ameuawa.

TAKWIMU ZA TLS
 
 Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, watu 83 wanaodaiwa kutekwa au kupotea kwa miaka minane kuanzia mwaka 2016 hadi 2024.
 
 Taarifa hiyo ya TLS iliyotolewa kwa vyombo vya habari mwaka  jana, inaonyesha wazi kuwa mambo ya kuteka watu yameendelea kujitokeza kila mwaka na inawataja baadhi ya waliotekwa.
 
 Miongoni mwa wanaotajwa na Rais wa TLS na majina ya mikoa yao kwenye mabano ni Ben Saanane (Dar), Azory Gwanda (Pwani), Simon Kanguye (Kigoma) na Joshua (Iringa), Kombo Twaha (Handeni-Tanga), Kennedy Mwamlima (Mbeya),  Edger Mwakalebela (Dar), James Sije (Nyakato-Mwanza), Joseph Mnyonga (Mwanza), Dotto Kabwa (Ifunga-Iringa) na Yahya Ally (Dar).
 
 Rais huyo anawataja wengine kuwa Chande Kizega (Dar), Mzee Samuel Mkongo (Geita Mjini), Charles Mwampyate (Dar), William Herman (Kangaye-Mwanza), David Lema (Mwanza),  Jerome Kisoka (Kilimanjaro) na Ridhiwani Msangi (Iringa).
 
 Katika kundi hilo, wamo pia Benson Ishungisa (Dar), Hamza Said (Mwatulole-Geita), Yonzo Dutu (Kishapu-Shinyanga), Lilenga Isaya (Mwandiga-Kigoma), Tawafiq Mohamed (Dar), Self Swala (Dar), Edwin Kunambi (Dar), Hemed Abass (Dar) na Maseke Mwita (Mara).


 Aidha, wamo pia Rajab Mdoe (Dar), Mzee Haji Soft (Dar), Alphonce Bilasenge (Kagera), Albert Selembo na Moloimeti Saing’eu, Ndirango lazier, Joel Lessonu, Simoni Orosikiria na Damian Laizer.
 
 Katika mchanganyiko huo wa miaka ya nyuma na 2024, anawataja pia Taleng’o Leshoko, Kijoolu Olojiloji, Shengena Killeli, Malongo Paschal, Simeli Korongoi, Ingoi Kanjwei, Sangau Ngiminis, Marijoi Parmati, Morongeti Masako, Kambatai Lulu na Orias Oleng’iyo na Luacs Njausi, hata hivyo mikoa yao haikutajwa.
 
 Anaendelea kuwataja wengine kuwa ni Matthew Siloma, Wilson Kolong, James Taki, Joseph Jartan, Kelvin Nairoti, Lekerenga Orodo, Fred Ledidi, Simon Morintanti wote kutoka Loliondo, mkoani Arusha.
 
 Vilevile wamo Mohamed Kalebe (Geita), Amon Magige (Mwanza), Aziz Kinyonga na  Yusuph Dudu (Dar) Kastory Kapinga (Mbinga), Dioniz Kipanya (Rukwa), Shadrack Chaula (Mbeya) na Prosiper Mnjari (Dar).
 
 Wengine ni Thomas Ihuya (Mwanza), Dennis Kantanga (Shinyanga), Damas Bulimbe na Lucas Bulimbe (Geita), Matuki Makuru (Mara), Dastan Nestory na Adinan Mbezi wote kutoka Geita.
 
 Katika msururu huo wamo Lengaripo Lukumay (Mwanza), Akidu Salim (Dar), Enock Chambala (Tanga), Dioniz Kipanya (Katavi), Nusra Omari (Dar), Theresphora Mwakalinga (Dodoma), Donald Mboya (Kagera), Ilham Makoye, Barack Majigeh, Yusra Musa, Angel Kamugisha, Brighton Emmanuel wote wa  Dar.
 
 Taifa kama dunia limeingia mwaka mwingine wa 2025, ambao inawezekana Watanzania wengi wanatamani uwe wa amani, kusiwe na matukio ya utekaji kama ilivyotokea 2024.

HERI YA MWAKA MPYA 2025