KUNA upepo fulani hivi umepita ndani ya CCM, chama tawala chenye umri wa miaka 47 ya kuzaliwa, lakini 70 ya kuona dunia, ikizingatiwa kuwa kilitokana na muungano wa Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shiraz Party (ASP) ya Zanzibar.
Upepo huo umetikisa matawi ya miti iliyooteshwa ndani ya chama hicho, baada ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti , komredi Abdulrahman Kinana, kuamua kujiuzulu uongozi lakini kuendelea kubaki ndani ya chama hicho.
Ni nadra sana kiongozi hususan wa Tanzania kujiuzulu bila kutenguliwa nafasi yake maarufu kama kutumbuliwa, sijui inatokana na nini, lakini inawezekana kila mtu ana wazo lake katika hilo, ila itoshe tu kusema inahitaji roho ngumu.
Ni wachache sana katika historia ya nchi hii, walioamua kuachia ngazi wenyewe na kukaa pembeni licha ya nafasi nzuri walizokuwanazo, akumbukwe Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye mwaka 1985 aliachia urais akisema anang’atuka.
Lakini pia aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ndugu Ali Hassan Mwinyi aliyefanya hivyo mwaka 1977 mwezi mmoja tu kabla ya kuzaliwa CCM, akiguswa na mauaji ya vikongwe yaliyotokea Shinyanga.
Hebu nambieni ni nani aliye tayari kujiuzulu leo kwa matukio yaliyofanywa na watu wengine tena mkoani? Nani? Watu wanang’ang’ania madarakani mpaka wang’olewe, hata kama wamebainika kuwa na hatia katika masuala mbalimbali.
Kujiuluzu kwa ndugu Kinana, hakika kumesababisha mjadala mpana sana huku watu wakijiuliza nani atachukua nafasi yake ndani ya CCM, mjadala umegusa wana CCM, wananchi wa kawaida na hata wapinzani ambao wengine kwa vyovyote wanachekelea jino pembe.
Hakika Komredi Kinana amefanya mambo mengi katika medani ya siasa nchini, akijulikana zaidi pale alipokuwa na umri wa miaka 44 aliposimamia kampeni za ndugu Benjamin William Mkapa mpaka kuwa rais wa tatu wa taifa la Tanzania.
Alifanya hivyo tena miaka 10 baadaye na kuwezesha kuingia madarakani ndugu Jakaya Mrisho Kikwete na kuwa rais wa nne wa taifa hili, na akirudia mwaka 2015 alipomwezesha ndugu John Magufuli kuwa Rais wa awamu ya tano.
Ni nadra sana kwa mwanasiasa kufanya haya kwa miaka 30, akiwezesha wengine kukalia kilele cha taifa bila kuingiwa na inda, na badala yake kuendelea kuwasaidia kwa karibu kwa hali na vitendo, katika uongozi wao na kufanikisha nchi kutulia.
Ndugu Kinana angekuwa na uchu wa madaraka, nani angemzuia kuchukua fomu na hakika kufanya vizuri katika kinyang’anyiro hicho? Ila alitosheka na alichokuwa nacho na alipokuwa hivyo, akaendelea kusaidia chama chake kuongoza nchi.
Hivi sasa lazima chama kinabungua bongo kumpata mrithi wake, lakini kikumbuke na kuzingatia kuwa ndugu Kinana ana nyayo panana ndefu hivyo anavaa kiatu kipana na kirefu. Kwa maana hiyo atafutwe mtu atakayevaa viatu hivyo vikamtosha.
Kiongozi huyu amefanya mengi ndani na nje ya CCM na kuacha alama ambayo haitafutika, na bila shaka wana CCM watamuenzi kwa alichokifanya, ingawa naamini kamailivyo ada ya Watanzania, atasahaulika muda si mrefu.
Atasahaulika na kusubiri kukumbukwa siku atakayokuwa amemaliza mwendo wake duniani, na ndiko wengi hujitokeza ama kuonyesha ya ndani ya mioyo yetu au kuumia kwa dhati, kutokana na kuondolewa huko, lakini naomba hili lisitokee kwa Kinana.
Mimi niliyepata kufanya naye kazi ndani ya chama hicho, nakumbuka siku aliponiita ofisini kwake na baada ya mazungumzo, akanikabidhi chupa ya mvinyo akiniambia ilimpendeza kunipa, ingawa alikuwa amepelekewa yeye kama zawadi ya Krismasi. Ilinifanya kujisikia vizuri sana na kumshukuru.
Hivyo basi kwa sifa hizi na zingine, CCM ina jukumu kubwa la kumkumbuka na kumwekea alama itakayodumu milele, hata kwa vizazi vijavyo, kwamba alipata kuishi mtu anaitwa ndugu Abdulrahman Kinana ndani ya CCM na Tanzania.
Wana CCM siku anatangazwa mrithi wake, natarajia mtamke kuwa moja ya viwanja vya michezo nchini mnavyovimiliki, kitaitwa kwa jina la ‘Uwanja wa Abdulrahman Kinana’. Viwe Jamhuri Morogoro au Dodoma au iwe Mkwakwani wa Tanga. Kuna sababu gani ya kuwa na Jamhuri mbili? Mbona Liti iliwezekana? Hongera sana komredi Kinana.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED