MUSWADA wa Sheria ya marekebisho ya Sheria za Kazi wa Mwaka 2024 umesomwa bungeni na miongoni mwa mapendekezo ni kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa aliyejifungua mtoto njiti.
Sheria zinazopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sura ya 366, Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura ya 300 na Sheria ya Usimamizi wa Ajira za Wageni, Sura ya 436.
Muswada huo ambao umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni kwa ajili ya hatua za utungaji wa sheria, kifungu cha 33 kinapendekeza kurekebishwa ili kuongeza muda wa likizo hiyo kwa kujumuisha katika likizo yake ya uzazi muda uliobaki kufikia 36 za ujauzito.
Lengo la marekebisho hayo ni kulinda ustawi na afya za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na kuhitaji muda wa kutosha wa uangalizi wa mama.
Aidha, kifungu cha 34A kinapendekezwa kuongezwa ili kumwezesha mwajiri kumpatia mwajiriwa likizo bila malipo isiyozidi siku 30, lengo ni kuweka mazingira mazuri yatakayomwezesha mwajiriwa kupata likizo bila malipo kutokana na majanga au dharura zinazoweza kujitokeza.
AJIRA ZA MKATABA
Pamoja na hayo, kifungu cha 14 kinapendekezwa kurekebishwa ili kubainisha aina ya mikataba ya muda maalum ili kuongeza wigo wa mazingira ambayo mtu anaweza kuajiriwa kwa mkataba wa kipindi maalum, ikiwamo mikataba ambayo mwajiriwa anaajiriwa kwa muda ili kuendana na ongezeko la wingi wa kazi, kutoa fursa kwa wahitimu wa vyuo ili kuwajengea uwezo na kufanya kazi nyingine za misimu.
Kifungu cha 16A kinapendekezwa kuongezwa ili kubainisha mazingira ambayo mwajiri na mwajiriwa wanaweza kuingia katika makubaliano ya namna watakavyofanya kazi katika hali ya dharura inayoweza kuathiri uzalishaji mahali pa kazi.
Lengo ni kuhakikisha ulinzi wa ajira na usalama wa mfanyakazi mahali pa kazi, kuwezesha uzalishaji na kupunguza athari kwa waajiri wakati wa magonjwa ya milipuko na matukio ya dharura.
MIGOGORO YA KAZI
Pia kifungu cha 37 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuweka masharti yanayozuia mwajiri kutoanzisha au kuendelea na shauri la nidhamu dhidi ya mwajiriwa pale ambapo mgogoro huo upo mbele ya Tume au Mahakama ya Kazi.
Lengo ni kuzuia uingiliaji wa mchakato wa ushughulikiaji wa migogoro iliyowasilishwa kwenye Tume au Mahakama ya Kazi.
Aidha, kifungu cha 40 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuainisha fidia kulingana na aina ya mgogoro na kuweka ukomo wa juu wa fidia inayotolewa kwa mwajiriwa aliyeachishwa kazi isivyo halali.
Lengo ni kuweka mwongozo wa utoaji fidia na kudhibiti utoaji wa fidia kwa kiwango kisicho na uhalisia pale inapothibitika kuwa mwajiriwa aliachishwa kazi isivyo halali.
Kifungu cha 41A kinapendekezwa kuongezwa ili kuweka masharti kuhusu afua kwa uvunjaji wa mkataba wa ajira ya muda maalumu na lengo ni kutoa mwongozo wa utoaji wa fidia kwa mwajiriwa pale ambapo mwajiri atakiuka vipengele muhimu vya mkataba vinavyoweza kupelekea mwajiriwa kuacha kazi.
Katika kifungu cha 71 inapendekezwa kuweka masharti ya utaratibu wa kuanza kutumika kwa mikataba ya hali bora inayoingiwa na wakuu wa taasisi za umma na lengo ni kuwianisha masharti ya sheria zinazosimamia utumishi wa umma.
AJIRA KWA WAGENI
Katika Sheria ya Usimamizi wa Ajira za Wageni, Sura ya 436, kifungu cha tisa kinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka masharti ya kumtaka raia wa kigeni mwenye kibali cha kazi daraja A anayekusudia kujihusisha na kampuni nyingine anayomiliki hisa kupata idhini ya Kamishna wa Kazi.
Lengo ni kuondoa usumbufu na kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa mwekezaji ambaye ni raia wa kigeni ambapo mara baada ya kupata kibali cha kazi kwa kampuni moja hatahitajika kupata kibali kingine kwa kampuni nyingine atakayomiliki hisa.
Kifungu cha 12 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuwawezesha wakimbizi wenye hadhi stahiki kuendelea kufanya kazi bila kubanwa na sharti la ukomo wa muda wa kibali cha kazi.
Vilevile, kifungu hicho kinarekebishwa ili maombi ya kuhuisha kibali cha kazi kuwasilishwa kwa Kamishna wa Kazi angalau miezi miwili kabla ya kuisha kwa muda wa kibali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED