Waziri ashauri Magereza kuchangamkia fursa za kilimo

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:09 PM Sep 30 2024
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akisalimiana na baadhi ya Maofisa wa Jeshi la Magereza baada ya kufika katika Gereza la Kilimo na Ufugaji Kitai, Mbinga, Mkoani Ruvuma.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akisalimiana na baadhi ya Maofisa wa Jeshi la Magereza baada ya kufika katika Gereza la Kilimo na Ufugaji Kitai, Mbinga, Mkoani Ruvuma.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ametoa wito kwa magereza ya uzalishaji mali nchini kuchangamkia fursa za kilimo cha mazao ya nafaka kwa kutanua maeneo ya mashamba ili kuendana na jitihada za serikali katika kuinua sekta ya kilimo.

Waziri Masauni aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na maofisa wa Gereza la Kilimo na Mifugo Kitai, Mbinga Mkoani Ruvuma ambapo alisema Jeshi la Magereza lazima likubaliane na maboresho ya kimfumo, kimuundo na kitaasisi ambayo yatakwenda kuongeza uwezo wa uzalishaji mazao ya kilimo nchini. 
 
Pia alisema miongoni mwa maboresho hayo ni kutenganisha mamlaka ya kiutawala ya Jeshi la Magereza na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi hilo (SHIMA), akisema maboresho yatakwenda kuleta ufanisi wa usimamizi wa masuala ya kiutawala na biashara. 
 
"Serikali imetanua fursa ya soko la mazao ya nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ambayo imepewa uwezo wa kununua mazao kwa bei kubwa lakini mpaka sasa bado hakuna jitihada zilizofanywa na Jeshi la Magereza kuchagamkia fursa hii,” alisema Mhandisi Masauni. 
 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akisalimiana na baadhi ya Maofisa wa Jeshi la Magereza baada ya kufika katika Gereza la Kilimo na Ufugaji Kitai, Mbinga, Mkoani Ruvuma. Picha Mpigapicha wetu.

Sambamba na hilo, alisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuacha na matumizi ya kuni na mkaa katika magereza ili kuendana na ajenda ya Afrika na dunia katika kutunza mazingira. 
 
Awali Waziri Masauni alitembelea Gereza hilo mwaka 2019 akiwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo ambapo amesema licha ya kuwa sasa kuna mabadiliko lakini alitarajia kuona mabadiliko makubwa zaidi ya kilimo katika gereza hilo.