Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya elimu jumuishi, malezi

By Allan Isack , Nipashe
Published at 07:05 PM Sep 30 2024
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,Dk.Wilson Mahera,akiteta jambo na Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Ludovick Minde, wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Shule ya Sekondari ya ST. Mary Goreti.
PICHA:ALLAN ISACK
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,Dk.Wilson Mahera,akiteta jambo na Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Ludovick Minde, wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Shule ya Sekondari ya ST. Mary Goreti.

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,Dk.Wilson Mahera,amesema serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa watoto kupata elimu jumuishi pamoja na malezi bora yatakayosaidia kuboresha maisha yao.

Dk.Mahera,alisema hayo,akimuwakilisha Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Prof.Adolf Mkenda,wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa Shule ya Sekondari ya ST.Mary Goreti iliyoko wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro. 

Hata hivyo,alisema serikali chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu ikiwamo kuweka miundombinu rafiki ya wanafunzi kujifunzia na walimu kufundishia.

Alisema Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014 na toleo la mwaka 2023 imesisitiza utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi nchini.

Hata hivyo,alisema takwimu zinaonesha kuwa sekta binafsi hususani kwa shule za kanisa zina mchango mkubwa kwenye mchango wa mafanikio ya sekta ya elimu nchini.

“Ninawashukuru kwa namna ya pekee wadau wa elimu mliojumuika hapa kwa kutambua kuwa mtoto ndiyo kipaumbele cha serikali kama ilivyoelezwa kwenye Sera ya Elimu na Mafunzo yam waka 2014 na kufanyiwa maboresho mwaka 2023,”alisema Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo.

Aidha alisema serikali kupitia Wizara hiyo,inatambua uwekezaji na mchango mkubwa uliofanywa na Shirika la Masista(Watawa) wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro(CDNK),chini ya Kanisa Katoliki Moshi katika Nyanja mbalimbali hususani kwenye sekta ya elimu.

Naye Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi,Mhashamu Ludovick Minde,alisema zawadi pekee ambayo mzazi anayoweza kumpa mtoto wake ni kumpatia elimu bora.

Vilevile aliwataka wanafunzi wote waliohitimu katika shule hiyo,kuwa waaminifu,waadilifu kuwa na nidhamu,watii,wanyenyekevu na wenye hofu ya Mungu.

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,Dk.Wilson Mahera, akivalishwa skafu na kijana wa Skauti alipowasili kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Shule ya Sekondari ya ST. Mary Goreti, iliyoko Moshi mkoani Kilimanjaro,Dk. Mahera alimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo,Prof. Adolf Mkenda. PICHA:ALLAN ISACK