Wakulima Mkuranga wajipanga kwa msimu mpya wa zao korosho

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 05:05 PM Sep 30 2024
Wakulima Mkuranga wajipanga kwa msimu mpya wa zao korosho
Picha:Mpigapicha Wetu
Wakulima Mkuranga wajipanga kwa msimu mpya wa zao korosho

Wakulima wa Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, wamejipanga kwa msimu mpya wa zao la korosho 2024/2025, huku viongozi wa vyama vya msingi wakikutana katika kikao kazi kujadili jinsi ya kusimamia msimu huo ili kuinua uchumi wa wakulima.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya msimu huu, Mwenyekiti wa Correcu Mkoa wa Pwani, Mussa Mng'eresa, alisisitiza umuhimu wa kusimamia kwa umakini mfumo mpya wa mnada wa korosho. Lengo kuu la kikao kazi hicho kilikuwa kuwaelimisha wenyeviti wa vyama vya ushirika kuhusu namna bora ya kuingia katika msimu huo, ili kuhakikisha mnada wa korosho unakuwa na ufanisi na kuwafaidisha wakulima moja kwa moja.

Mng'eresa alieleza kuwa sasa mnada umeboreshwa, ambapo mnunuzi atachukua korosho ndani ya siku tano, huku wakulima wakipata malipo yao ifikapo siku ya nne baada ya mnada. “Ni muhimu kwa viongozi wa vyama vya ushirika kusimamia ubora wa korosho na kuhakikisha zinakuwa safi kabla ya kuingizwa kwenye maghala,” alisema Mng'eresa.

Hamis Mantawela, Meneja wa Correcu Mkoa wa Pwani, aliongeza kuwa maghala yanatakiwa kuwa katika hali bora, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia magunia yenye nembo ya chama. Alisema hatua hii inalenga kuhakikisha korosho zinahifadhiwa vizuri na kuepuka unyevu ambao unaweza kusababisha kuharibika kwa korosho.

1

Kwa upande wake, Mantawela alieleza kuwa katika msimu wa 2024/2025, tozo zote zitalipwa na mnunuzi. Hata hivyo, wakulima watalipia shilingi mbili kwa wadau na shilingi mbili kwa ajili ya "primary center." Aidha, waraka wa mrajisi utakuwa na ushuru wa shilingi 55 kwa kila kilo.

Akizungumzia matarajio ya msimu, Mng'eresa alisema Mkoa wa Pwani unatarajia kuvuna tani 36,000 za korosho katika msimu wa 2024/2025, ikiwa ni ongezeko kutoka tani 22,000 zilizovunwa mwaka jana. "Tunatarajia mavuno zaidi mwaka huu, hivyo ni muhimu kwa wenyeviti wa vyama vya ushirika kuendana na mabadiliko ili kusimamia uzalishaji mwingi wa zao hilo," alisisitiza.

Wakulima na viongozi wa vyama vya ushirika wametakiwa kuhakikisha wanazingatia mwongozo uliowekwa na serikali ili kuhakikisha msimu wa korosho unaenda vizuri na wakulima wananufaika moja kwa moja na juhudi zao.