Oasis kuwakutanisha wafanyabiashara na TRA

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 07:15 PM Sep 30 2024
Meneja Masoko wa Taasisi ya Oasis ambao ni washauri wa kodi, Lydia Sahan, akizungumzia kuhusu kongamano la elimu ya mlipa kodi. Picha Maulid Mmbaga.
Picha: Maulid Mmbaga.
Meneja Masoko wa Taasisi ya Oasis ambao ni washauri wa kodi, Lydia Sahan, akizungumzia kuhusu kongamano la elimu ya mlipa kodi. Picha Maulid Mmbaga.

WASHAURI wa masuala ya kodi nchini wameandaa kongamano ambalo litawakutanisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wafanyabiashara zaidi ya 1,000 kutoka maeneo mikoa mbalimbali kwa lengo la kujadili matatizo ya kikodi.

Akizungumza na Nipashe Digital leo mkoani Dar es Salaam, Meneja Masoko wa Taasisi ya Oasis ambao ni washauri wa kodi, Lydia Sahan, amesema kongamano hilo ambalo litafanyika Oktoba 2, mwaka huu mkoani hapo, ni katika jitihada za kuiunga mkono serikali katika kushughulikia matatizo yanayowakabili walipakodi.
  
Pia amesema wameridhishwa na namna ambavyo TRA inashughulikia changamoto za kikodi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu na wafanyabiashara nchini.
 
“Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda amekuja na mfumo tofauti wa kutembea mikoa mbalimbali kukaa na kusikiliza changamoto za wafanyabiashara na kuzipatia suluhu, kusikilizana ni njia sahihi itakayoleta matokeo chanya kwa mfanyabiashara na taifa.
 
 “Tunaamini changamoto zilizowahi kujitokeza siku za nyuma hatutofika huko tena kutokana na muendelezo tunaouona kwa TRA, na kongamano hilo ni sehemu ya kukumbusha kwamba Tanzania ni nyumbani na sio lazima tugombe tunaweza kukaa na kuzungumza, kikubwa tutoe mapendekezo ili kuyapa mamlaka kazi ya kufanya,” amesema Lydia.
 
Ameongeza kuwa njia hiyo itawafanya TRA na Wizara ya Fedha kuona kwamba kumbe wakifanya hivi itamsaidia mtanzania na kufanikisha biashara nchini, akieleza kuwa wanataka uchumi ukuwe lakini hilo haliwezi kufanikiwa kama mfanyabiashara hayuko katika mazingira mazuri, rafiki na kufanya kazi kwa roho safi.
 
Frank Nduta ambaye ni Katibu wa Jukwaa linalotumiwa na Wafanyabiashara kujadili fursa na changamoto mbalimbali zinazowahusu katika soko la Kariakoo, amesema licha ya changamoto zilizowakuta siku za nyuma lakini kwa sasa wanamatumaini na kwa namna TRA inavyoendesha shughuli zake.
 
“Kamishna wa TRA amekuwa akifika kwa wadau wa biashara moja kwa moja ili kuhakikisha kwamba mfumo wa zamani ambao ulikuwa umeaminika kuwa TRA ni maadui wa biashara kwa wafanyabiashara, yeye amekuja kuongeza urafiki kati ya mamlaka na wafanyabiashara.
 

Ofisa Msimamizi Mkuu wa Kodi TRA, Lutufyo Mtafya, akitoa elimu ya kodi kwa mfanyabiashara.

“Lakini hata sisi wafanyabiashara tunaona ni faraja kwetu kwenda kusikilizwa kwenye mazingira ya amani kuliko ambavyo mkigombana ndo mkasikilizane, kwa sasa tusikilizane kwa wakati ambao mfanyabiashara na TRA wote tunacheka,” amesema Nduta.
 
Ametoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kufika katika mafunzo hayo na wayasikilize kwa maslahi mapana ya taifa, akieleza kuwa endapo biashara zitafanyika vizuri, nchi itapata kodi na huduma za jamii nzuri kwasababu fedha itakuwa inapatikana ya kutosha.
 
"Tuna kila nafasi ya kushiriki kwenye kujenga nchi yetu kwa kulipa kodi bila kusukumwa na mtu yoyote,” amesema Nduta.
 
Ofisa Msimamizi Mkuu wa Kodi TRA, Lutufyo Mtafya, amesema siku za nyuma mfanyabiashara akiona TRA alikuwa anafunga lakini ni tofauti na sasa, na kwamba toka wameanza kutekeleza maelekezo ya rais ya kukusanya kodi kwa kufuata utaratibu bila kuonea watu na kutobagua, mtazamo kwa wafanyabiashara umebadilika.
 
“Kwa sasa kamishna mkuu anafanya mikutano na walipa kodi anapita kila mkoa na maeneo tofauti akizungumzia suala la kuwa na mahusiano bora kati ya TRA, serikali na walipakodi kwa ujumla wake, na tumefungua njia mbalimbali za mawasiliano na wafanyabiashara.
 
“Ofisi zetu kila mkoa zina ofisa anaesimamia suala la elimu, ukienda kwenye wilaya tumeelekeza awepo ofisa ambaye yeye mlipakodi akifika au mtu anayehitaji kujua masuala ya kodi aweze kumpa taarifa zote, na kufanya kazi na Oasisi ni njia mojawapo shirikishi kwa tuliowapa leseni kusaidia kutoa elimu,” amesema Mtafya.
 
Hata hivyo, amesema mamlaka imezinagatia masuala mbalimbali ambayo yalikuwa ni changamoto kwa mlipakodi na kwamba watayazungumzia siku ya kongamano hilo litakalofanyika kesho mkoani Dar es Salaam.