Aweso awahakikishia huduma ya maji wakazi wa Dar na Pwani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:26 PM Sep 30 2024
Waziri wa Maji Jumaa Aweso.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Maji Jumaa Aweso.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso amekutana na kufanya kikao kazi na Menejimenti pamoja na timu za ufundi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kwa lengo la kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Waziri Aweso ametoa rai kwa watendaji wa DAWASA kuweka  utaratibu wa kutembelea Wananchi na kusikiliza changamoto zao ili kuweza kuzipatia majibu kwa haraka.

"Wananchi wanahitaji huduma ya maji, twendeni tukaifanye kazi kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hii, na tuweke utaratibu wa kuwatembelea kujua changamoto zao zao"ameeleza Aweso.

Waziri wa Maji ameongeza kwa kuzitaka Idara wezeshi kama vile Idara ya Uzalishaji na usambazaji Maji pamoja na Idara ya Miradi kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja Ili kuhakikisha huduma inakuwa bora wakati wote.

Kwa upande mwingine Waziri Aweso amewatoa shaka Wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam na Pwani kuwa upatikanaji wa huduma ya maji ni wa uhakika baada ya kukamilisha kwa matengenezo ya Pampu katika Mtambo wa Ruvu Juu .

1

"Tulikua na maboresho kidogo katika mitambo ya uzalishaji maji ya Ruvu Juu kwa kipindi kifupi hali iliyopunguza kiwango cha uzalishaji na hivyo kupelekea upungufu  wa huduma kwa baadhi ya maeneo. Nitoe uhakika kuwa changamoto hii imetatuliwa na tumeweka mikakati zaidi ya uboreshaji huduma itakayoleta tija zaidi" ameeleza Waziri Aweso