"Waliotumwa na afande" wahukumiwa kifungo cha maisha jela

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:02 PM Sep 30 2024
"Waliotumwa na Afande" wahukumiwa kifungo cha maisha jela
Picha: Mtandao
"Waliotumwa na Afande" wahukumiwa kifungo cha maisha jela

Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, imewahukumu kifungo cha maisha gerezani washtakiwa wanne baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti, mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam.

Katika kesi ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 iliyokuwa inawakabili washtakiwa hao akiwamo MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo ambaye ni Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.

Kesi hiyo maarufu ‘Waliotumwa na Afande’ imesikilizwa faragha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma ambapo upande wa Jamhuri uliwasilisha Mashahidi 18 na vielelezo 12 kuthibitisha mashtaka dhidi ya Washtakiwa.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu, Septemba 30, 2024. Hata hivyo Mahakama hiyo imewataka kila mmoja kumlipa binti huyo fidia ya Shilingi milioni 1.

Washtakiwa walifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza August 19, 2024 na kusomewa mashtaka mawili ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile Binti huyo ambaye Mahakamani anatambulika kwa jila la XY ambapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule Washtakiwa hao baada ya kusomewa mashataka walikana na kutokana na unyeti wa kesi hiyo hawakupatiwa dhamana.