Machungu wanayopitia wanafunzi wanaoishi 'gheto'

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:36 AM Sep 30 2024
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Isagenhe,wilayani Nzega mkoani Tabora wakionesha bango kufikisha ujumbe kuhusu vikwazo wanavyopitia kufikia ndoto zao.
PICHA:ELIZABETH ZAYA
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Isagenhe,wilayani Nzega mkoani Tabora wakionesha bango kufikisha ujumbe kuhusu vikwazo wanavyopitia kufikia ndoto zao.

NDOTO za wanafunzi wa Shule ya Sekondari Isagenhe, wilayani Nzega, mkoani Tabora kufika katika hatua nzuri kielimu, zinasongwa na vikwazo lukuki.

Kutokana na kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shuleni, wanafunzi hao waliamua kupanga vyumba, maarufu ghetto, katika kijiji cha Isagenhe, kilichoko karibu na shule yao.

Kwa nyakati tofauti, wanafunzi hao wanaelezea hali halisi ya maisha ya gheto kwa mwandishi wa habari wa Nipashe aliyeko katika ziara ya wadau wa Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN) waliofika katika kijiji hicho kutoa elimu ya namna ya kupambana na ukatili na ndoa za utotoni ili kumpa fursa mtoto wa kike kutimiza ndoto zake.

Wanafunzi hao wameelezea namna ambavyo maisha ya gheto yamegeuka kuwa mzigo kwao, hata kutamani kurudi kuishi nyumbani kwa wazazi wao, lakini wanawaza madhila ya kutembea umbali mrefu waliyopitia kabla ya kuamua kuishi maisha hayo ya ghetto.

Lengo la kuingia katika maisha hayo ya ghetto lilikuwa jema - kupunguza umbali ambao wamekuwa wakitembea kwenda shuleni na kurejea nyumbani, huku wakikumbana na vikwazo katika safari zao za kila siku, ikiwamo kunusurika kuliwa na wanyama wakali.

Si tu wanyama wakali, kutembea umbali mrefu kwenda shule na kurejea nyumbani, kuliwaweka katika hatari ya kubakwa na watu wasio na nia njema.

Wakati mwingine, walifika shuleni kwa kuchelewa na kukosa baadhi ya vipindi vya masomo yao.

Kama hiyo haitoshi, madarasa yenye mitihani wanaotakiwa kurudi shuleni kwa ajili ya masomo ya ziada jioni kutokana na umbali wanakoishi walishindwa kuhudhuria.

Sasa wameamua kusogea karibu na shuleni ili kupunguza hatari zilizopo katika kutembea umbali mrefu, lakini bado ni kama shida zimeongezeka, wanakumbana na maisha magumu ya kuishiwa chakula na kushindwa kumudu pango la nyumba.

Wanajitwisha mzigo wa kujilea kwa kufanya vibarua mbalimbali vya muda mfupi, ili wapate fedha kwa ajili ya mahitaji ya kulipa pango la nyumba wanakoishi wakati wanaendelea na masomo, kununua chakula na mahitaji mengine kama madaftari.

Vibarua wanavyofanya ni pamoja na kazi za ndani kwenye nyumba za watu, kulea watoto na hata kufanya shughuli za shambani na siku wanazofanya hivyo mara nyingi ni zile za mapumziko, Jumamosi na Jumapili.

Na pale inapobidi, baadhi hutoroka vipindi shuleni, hata katikati ya wiki, muda wanaotakiwa kuwa darasani na kwenda kufanya vibarua hivyo, ili wapate fedha ya chakula na pango au kulipia mahitaji mengine hasa kunapokuwa na uhitaji wa haraka.

Ujira wa kazi hizo za vibarua kwa siku huanzia Sh. 2,000 hadi 4,000 kulingana na aina ya kibarua chenyewe.

Baadhi ya wanakijiji wanaelezea kwamba pamoja na wanafunzi hao kufanya vibarua kwa ajili ya kujitafutia fedha ya kujikimu, kumekuwa na 'mitego' inayowaweka kwenye hatari kubwa wanafunzi wa kike ya kushawishika kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na hata kupata ujauzito.

Neema Julius ni miongoni mwa kinamama wanaoishi katika kijiji hicho anayesema wapo baadhi ya wanafunzi wa kike waliowahi kuishi maisha ya gheto, lakini walipewa ujauzito na wanaume walikokuwa wanafanya vibarua.

"Waliwahi kuja hapa wanafunzi wakapanga kama hivyo vyumba vyao kwa sababu walikotoka ni mbali, lakini wengi wao huwa wazazi wao hawawatumii fedha ya kujikimu, kwa hiyo wanalazimika kufanya vibarua lakini isivyo bahati wanakutana na kinababa wengine si watu wazuri, wanawarubuni kimapenzi kwa kuwapa fedha kidogo lakini mwisho wa siku wanaishia kupata mimba," anasema Neema.

 WANAFUNZI

Mmoja wa wanafunzi wa kike anayesoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondaeri Isagenhe, anayeishi maisha hayo ya ghetto (jina linahifadhiwa), anasema pamoja na kukosa fedha ya pango, chakula na mahitaji mengine ya shule, baadhi ya vijana pamoja na kinababa kijijini huko huwavizia kwenye ghetto mara kwa mara wakiwataka kimapenzi.

"Dada sijui nikwambieje... hapa si kukosa fedha tu, lakini kila siku tunaishi maisha ya kuviziwa, wanaweza kukufuata unapoishi au wakakutegea wakati unakwenda kwenye masomo ya 'prepo' au wakati unarudi. 

"Unakuta vijana wamekaa kwenye vikundi, ukipita wanakufuatilia nyuma, wanakutongoza na ukikataa sasa, hayo matusi wanayokutukana kuna wakati unatamani uache na shule yenyewe urudi kijijini kwenu," anasema.

Anasema kuwa kwa sasa wanafunzi wote wanaopanga wameanzisha utaratibu wa kutembea kwa makundi wanapokwenda shuleni na kurejea, hasa wanapokwenda kwenye vipindi vya masomo vya usiku 'prepo'.

"Kuna mwenzetu mmoja naye alikuwa anapanga kama sisi, mwaka jana alikuwa kidato cha pili, lakini yeye amepata ujauzito na ni kwa sababu ya maisha magumu ya kuhangaika kutafuta fedha ya kujikimu na vishawishi vya kimapenzi, alishindwa kuvishinda.

"Vyumba tunavyopanga sisi kodi ni Sh. 5,000 au 10,000 kwa mwezi, kwa hiyo mzazi anaweza kukulipia ya mwezi mmoja au miwili lakini miezi inayofuata halipi na wala hajali kufuatilia unaishije, kwa hiyo kuna wakati unachanganyikiwa, unajikuta kila kitu kimeisha, huna fedha, pango, chakula, madaftari yameisha, darasani hapakaliki inabidi utoroke ukatafute kibarua na wengine ndio kama hivyo wanaona watafute wanaume wawasaidie ndio hao sasa wanapata mimba," anasimulia.

MKUU WA SHULE

Mkuu wa Shule ya Sekondari Isagenhe, Jumamne Shaban, alisema moja ya changamoto kubwa wanazokutana nazo ni wanafunzi kutembea umbali mrefu; wapo wanaosafiri umbali wa kilomita 20 kwenda shuleni, hivyo kwa siku moja anatembela kilomita 40.

"Chukulia mtoto huyu kama hana baiskeli, atafika saa ngapi shuleni akiwa anatembea kwa miguu? Maana si wote wenye hizo baiskeli na ndio maana huwa tunawashauri wazazi wawapangie vyumba maeneo ya karibu na shuleni wakati tukisubiri na kuweka tumaini kwamba mabweni yatajengwa," anasema Shaban.

Mwalimu huyo anabainisha kuwa mwaka 2017 hali ilikuwa mbaya zaidi na kwamba kutokana na wanafunzi wengi kutembea umbali mrefu, wapo waliokata tamaa na kukatisha masomo na ni wanafunzi wa kike wanne pekee ndio walifanikiwa kuhitimu kidato cha nne.

Anasema kuwa sasa wanapata hamasa kidogo kwa sababu wamesaidiwa baadhi ya mahitaji na Shirika la Msichana Initiative, zikiwamo baiskeli, sare za shule na daftari japo si wote ambao wamepata.

 SERIKALI

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Isagenhe, Bajati Kalamu, alisema mwaka jana waliwakamata na kuwachukulia hatua baadhi ya watu waliobainika kuwashawishi wanafunzi wanaopanga mtaani kuanzisha nao uhusiano wa kimapenzi.

Mwaka jana tulibaini kwamba wapo baadhi ya watu wanaanzisha uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi waliopanga mtaani na tuliwakamata, tukachukua hatua. 

"Kwa sasa tumeomba walimu wawe na rekodi ya watoto waliopanga ili kuwafuatilia zaidi na kufahamu maendeleo yao," anasema Kalamu.

Anasema mpango wa serikali ni kujenga mabweni ili wanafunzi wote waishi shuleni badala ya kukaa mtaani na kwamba uhitaji uliopo ni mabweni manne.

"Na tumeomba wenyeviti wote wa vijiji wa kata hii, waitishe vikao na wananchi ili wenye uwezo wa kuchangia wachangie, ili tuanze ujenzi haraka, angalau tuanze na mabweni mawili ya wanafunzi wa kike halafu tutamalizia hayo mawili mengine baadaye," anasema Kalamu.

ASASI

Ofisa Miradi kutoka Shirika la Msichana Initiative wilaya ya Nzega, Rose Batoba alisema wamebaini kwamba kuna changamoto kubwa ya wazazi wa eneo hilo kutokuwapatia watoto wao mahitaji ya msingi, wakiaamini kwamba kutokufanya hivyo ndio njia nzuri ya kuwakatisha tamaa wasiendelee na shule ili wapate mwanya wa kuwaozesha.

"Mwamko wao wa kumpatia elimu hasa mtoto wa kike ni mdogo, wanaamini ni wa kuolewa tu, na ndio maana hawawapi mahitaji ya msingi ili watoto wakate tamaa wenyewe na waache kabisa kwenda shuleni. 

"Na ndio maana sisi tuliliona hilo tukaamua kuanzisha utaratibu wa kuwasaidia baadhi ya mahitaji, zikiwamo baiskeli, madaftari na sare za shule," anasema.

Kwa mujibu takwimu za Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mwaka 2019, miongoni mwa sababu zilizochangia wanafunzi wa kike 5,398 kukatisha masomo kwa kupata mimba ni pamoja na kutembea umbali mrefu wanapokwenda shuleni.