Kicheko mikopo ya elimu ya juu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:30 AM Sep 30 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia.

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeanza kutangaza orodha ya wanafunzi wenye sifa waliopangiwa mikopo kwa ajili ya mwaka wa masomo 2024/25, ‘kicheko’ kwa wanufaika kikiwa ni kupanda kwa kiwango cha chini cha mkopo kwa mnufaika mmoja mmoja hadi Sh. milioni tatu kutoka Sh. milioni 2.7 mwaka uliopita wa masomo.

Awamu hii ya kwanza ya wanufaika hao iliyotangazwa juzi, inajumuisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo ya shahada ya awali, shule ya sheria kwa vitendo na shahada ya uzamili.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, akizungumza na waandishi habari jijini Dar es Salaam juzi, alisema wanafunzi wote walioomba mikopo kwa mwaka 2024/25 wanaweza kupata taarifa za kina kuhusu mikopo yao kupitia akaunti walizotumia kuombea mikopo, maarufu SIPA, yaani ‘Student’s Individual Permanent Account’.

“Leo (juzi) tumeanza kutoa taarifa za mikopo kwa makundi yote, waliopangiwa mikopo, wapo ambao bado tunaendelea kufanyia kazi maombi yao kila mwombaji anapata taarifa yake kwenye akaunti ileile aliyotumia kuombea mkopo, huhitaji kufika ofisi za HESLB”, alisema Dk. Kiwia na kuongeza kuwa upangaji mikopo kwa wanafunzi wa stashahada na shahada ya uzamivu unaendelea.

Dk. Kiwia alisema kuwa HESLB imeanza kuandaa malipo ya wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo ambao ni wanufaika wa mikopo na kusema kuwa lengo ni kuhakikisha fedha zinafika vyuoni kwa wakati.

“Mwaka huu, serikali imetenga Sh. bilioni 787 kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 245,799 wakiwamo zaidi ya wanafunzi 88,000 wa mwaka wa kwanza waliotengewa Sh. bilioni 284.8, alisema Dk. Kiwia na kuongeza kuwa bajeti ya mwaka 2024/25 imeongezeka kwa Sh. bilioni 38 sawa na asilimia 5.1 kulinganishwa na bajeti ya 2023/24 iliyokuwa Sh. bilioni 749.4.

Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa mwaka huu, kiwango cha chini cha mkopo kwa mnufaika  mmoja mmoja kimepanda hadi Sh. milioni tatu kutoka Sh. milioni 2.7 mwaka jana (2023/24).

Kuhusu wajibu wa vyuo, Dk. Kiwia alikumbusha vyuo ambavyo havijawasilisha matokeo ya mitihani ya wanafunzi-wanufaika wanaoendelea na masomo, kuwasilisha ili kuwezesha HESLB kuandaa malipo kwa wakati.

“Kuna vyuo vichache ambavyo bado havijawasilisha matokeo, tumewakumbusha na tunasisitiza waharakishe kuwasilisha matokeo ili tukamilishe malipo ya wanafunzi waliofaulu kuendelea na masomo,” alisema Dk. Kiwia.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB alisema kuwa awamu ya pili ya orodha ya wanafunzi waliopangiwa mikopo kwa mwaka 2024/25 itatangazwa wiki ijayo.

Vilevile, Dk. Kiwia alieleza kuwa elimu iliyotolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kuhusu namna ya kuomba mikopo, imesaidia kupunguza makosa ya waombaji, hivyo kuharakisha mchakato wa kuwapangia mkopo.

Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu na vya Kati (TAHLISO), Zainab Kitima, alishukuru serikali kwa jitihada zake za kuongeza kiwango cha chini cha mkopo kwa mnufaika mmoja mmoja, akifafanua kuwa ongezeko hilo limepunguza mzigo kwa wazazi na wanafunzi, hasa kutoka familia zenye hali duni.

“Tunaishukuru sana serikali. Leo tumemsikia Mkurugenzi Dk. Kiwia akisema mikopo itafikishwa vyuoni kwa wakati, jambo ambalo ni faraja kwa wanufaika wa mikopo kote nchini. Hata hivyo, tunaendelea kutoa wito kwa HESLB kuzingatia changamoto zingine ambazo bado tunazo,” alisema Zainab.

Mwongozo utoaji mikopo na ruzuku ulizinduliwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda Mei 27 mwaka huu. Dirisha la uombaji mikopo lilifunguliwa Juni Mosi na kufungwa Septemba 14 mwaka huu.