Mramba akaribisha Uingereza uwekezaji wa nishati jadidifu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:50 AM Sep 30 2024
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Picha:Mtandao
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amezikaribisha kampuni kutoka Uingereza kuwekeza kwenye sekta ya nishati hasa eneo la nishati jadidifu.

Amesema uwekezaji huo una azma ya kutimiza lengo la serikali la kuingiza umeme mwingi kwenye gridi ya taifa unaotokana na nishati hiyo. 

Mramba alisema hayo jana jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania ukiongozwa na Euan Davidson, Kiongozi wa Timu ya Ustawi Endelevu katika kikao kilicholenga kujadili maeneo ya ushirikiano. 

Mhandisi Mramba aliueleza ujumbe huo kuhusu mahitaji ya uwekezaji kwenye miradi ya nishati jadidifu ikiwamo umeme jua kwa ajili ya matumizi ya majumbani hasa kwenye sehemu zilizo nje ya gridi na uwekezaji mkubwa wa umeme jua utakaoingia katika  gridi ya taifa. 

Alisema tayari uwekezaji kwenye nishati ya umeme jua umeanza kupitia mradi wa Kishapu-Shinyanga wa megawati 150 na uwekezaji mwingine utafanyika kwenye maeneo mengine nchini ikiwamo mkoa wa Dodoma wenye uwezo wa kuzalisha megawati 200. 

Kuhusu uwekezaji katika umeme unaotokana na upepo, alisema maeneo tayari yameshatambuliwa ambayo yanaweza kuzalisha yakiwamo Dodoma, Singida, Mbeya, Makambako, Same, Mara na Arusha ambayo yanahitaji ushirikiano katika uwekezaji. 

“Tanzania tumebarikiwa  vyanzo vingi vya nishati jadidifu kwani pia tuna hazina kubwa ya jotoardhi katika maeneo takriban 52 ambayo yakiendelezwa yatazalisha umeme kuliko Kenya ambayo sasa inazalisha umeme wa jotoardhi takriban megawati 1000,” alisema. 

Pia alieleza nia ya Tanzania kutumia nishati safi zaidi kuzalisha umeme ikiwamo nishati ya blue hydrogen inayotokana  na gesi asilia na matumizi nishati ya kinyesi cha wanyama na mabaki ya mimea (biogas) hasa katika vijiji yenye mifugo mingi. 

Kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhandisi Mramba aliueleza ujumbe huo juhudi zinazochukuliwa na serikali kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia iliyo safi kupikia ifikapo mwaka 2034. Alisema mpango huo ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, ambao utekelezaji wake unashirikisha serikali na wadau mbalimbali ikiwamo sekta binafsi. 

Mhandisi Mramba alisema katika usambazaji wa umeme vijijini, Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye eneo hilo na asilimia 99 ya vijiji vimefikiwa na nishati hiyo huku akibainisha kuwa ifikapo Desemba, mwaka huu, kila kijiji kitakuwa kimefikiwa na huduma hiyo.